1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Dortmund sare na Madrid, Leverkusen yatamba

Bruce Amani
8 Desemba 2016

Marco Reus alirejea katika kikosi cha Dortmund kwa bao la kusawazisha katika dakika za mwisho dhidi ya Real Madrid. Leverkusen iliizaba Monaco

https://p.dw.com/p/2Twkp
Champions League  Real Madrid v Borussia Dortmund
Picha: Reuters/S. Vera

Real Madrid 2-2 Borussia Dortmund
(Benzema 27', 52' - Aubameyang 60', Reus '88)

Dortmund ilisafiri kwenda Madrid ikiwa bila shinikizo, lakini wangefuzu wakiwa vinara wa kundi lao kama wangetoka sare. Katika mchuano huo wa kusisimua, Real walionekana kuwa katika usukani. Timu zote mbili zilikuwa na nafasi chungu nzima za kufunga bao lakini Karim Benzema aliweza kutikisa lango la wenyeji mara mbili na kuwaweka kifua mbele. Benzema sasa ana mabao 50 katika Champions League – idadi sawa nay a Thierry Henry, zaidi kuliko wachezaji wengine isipokuwa tu Cristiano Ronaldo na Lionel Messi.

Dortmund ilijiimarisha katika kipindi cha pili na kupata bao la kwanza kupitia Pierre-Emerick Aubameyang. Baadaye katika dakika za mwisho mwisho, Marco Reus alifunga bao safi baada ya kupata pasi safi kutoka kwa Aubameyang.

Bayer Leverkusen 3-0 Monaco
(Yurchenko 30', Brandt 48', de Sanctis '82 OG)

Leverkusen pia walifahamu kuwa wangefuzu katika hatua ya 16 za mwisho bila kujali matokeo ya mchuano huo. Walichezesha kikosi imara hata hivyo, na kuwaduwaza wageni Monaco. Bao la kwanza lilifungwa na mtu ambaye hakutarajiwa kufunga na lilikuwa kombora kutoka kwa Vladen Yurchenko. Julian Brandt alfunga la pili muda mfupi baadaye kabla ya Beki wa kushoto Wendell kumalizia shughuli kwa kufunga mkwaju wa penalti.

Matokeo mengine ya Champions League, Desemba 7:

Tottenham 3-1 CSKA Moscow
Lyon 0-0 Sevilla
Porto 5-0 Leicester City
Juventus 2-0 Zagreb
Legia Warsaw 1-0 Sporting
Brugge 0-2 Copenhagen

Mwandishi: Bruce Amani/DW
Mhariri: Daniel Gakuba