1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Dortmund yaiduwaza Bayern katika Super Cup

14 Agosti 2014

Borussia Dortmund wamepata hadhi kabla ya kuanza msimu mpya, kwa kukichapa kikosi dhaifu na cha majaribio cha Bayern Munich magoli mawili kwa sifuri. Pep amesema anahitaji muda wa kujiandaa kwa msimu mpya

https://p.dw.com/p/1Cumi
Supercup 2014 Borussia Dortmund - FC Bayern München
Picha: Reuters

Henrikh Mkhitaryan na Spiderman, Pierre Emerick Aubameyang walitikisa nyavu. BVB walitwaa kombe la SuperCup la Ujerumani katika uwanja wa nyumbani.

Matokeo hayo yalidhihirisha kilichoendelea uwanjani, huku Bayern wakionekana kukosa maarifa, katika safu ya ulinzi na kukosa ubunifu katika safu ya kiungo kutokana na mfumo wao wa 3-4-3. Dortmund walicheza kwa kasi na kufanya mashambulizi ya mara kwa mara hali iliyozusha maswali mengi kuhusiana na mabeki wa Bayern.

Vijana wa kocha Jügne Klopp walibisha katika lango la BAYERN mara 22 ikilinganishwa na mashambulizi manne pekee waliyoyafanya vijana wa Pep guardiola. Matatizo ya ulinzi ya Bayern yaliongezeka hata zaidi katika kipindi cha kwanza baada ya Javi Martinez kulazimika kuondoka uwanjani kutokana na jeraha.

Katika msimu uliopita, Dortmund iliizaba timu ya majaribio ya Bayern Munich – iliyokuwa ikijifunza mbinu mpya za kocha Pep Guardiola – 4-2 katika kombe la Super Cup. Bayern hata hivyo walishika kasi na wakashinda mataji mawili ya nyumbani na kuweka rekodi mpya ya kushinda taji la ligi mapema kabla msimu kukamilika. Klopp na wenzake watatumai kuwa ushindi wao wa mwaka huu wa ishara halitakuwa taji lao pekee msimu huu.

Mwandishi: Bruce Amani/DPA
Mwandishi: Sekione Kitojo