1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Dr.Rice Mashariki ya Kati

26 Agosti 2008

Waziri wa nje wa Marekani akosoa ujenzi wa maskani za wayahudi.

https://p.dw.com/p/F4wQ
Dr.C.Rice (M.Kati)Picha: AP

Waziri wa nje wa Marekani Dr.Condoleeza Rice akiwa katika ziara yake nyengine ya Mashariki ya kati, leo aliitaka Israel kujiepusha kuchafua juhudi za amani kati yake na wapalestina.Hii imefuatia kutoka taarifa kwamba Israel imekaribia kuongeza mara 2 maskani za wayahudi katika ardhi za wapalestina.

►◄

Dr.Condoleeza Rice akiwa katika ziara yake nyengine Mashariki ya kati kwa shabaha ya kufikia suluhisho la amani kati ya Israel na wapalestina hadi mwishoni mwa mwaka huu,alikariri wakati wa mkutano wa pamoja na waziri wa nje wa Israel,bibi Tzipi Livni tuhuma zake za muda mrefu juu ya ujenzi wa maskani za wayahudi.

Alisema,

"Nadhani si siri na nimewaambia wenzangu wa israel kuwa sidhani ujenzi wa maskani unasaidia kitu."

Akaongeza,

"Kile tunachohitaji sasa ni hatua zinazoimarisha imani kati ya pande husika na chochote kile kinachochafua imani hiyo chapaswa kuepukwa."

Alisema Dr.Rice.

Wapalestina kwa upande wao, wanadai ujenzi wa maskani za wayahudi katika ardhi zao kunawanyima wao ardhi wanayopanga kuunda dola yao ya wapalestina.

Njia ya kuelekea amani inayoungwamkono na Marekani-Road map- inaitaka Israel kukomesha ujenzi wa maskani Ukingo wa Magharibi na wapalestina nao wawazuwie wakereketwa wao kutumia nguvu.

Israel inadai inakusudia kuendelea kujenga majumba ambayo inapanga kubakia nayo katika mpango wowote ule wa amani kati yao na wapalestina.

Nae waziri wa nje wa Israel bibi Livni amesema na ninamnukulu,

" Utaratibu wa amani hauathiriki na usiathiriwe kwa aina yoyote ya ujenzi wa maskani za wayahudi."

Akaonya vishindo vya darini visiachiwe kuchafua mazungumzo ya amani.

Dr.Rice akiwa katika ziara yake ya 7 Mashariki ya kati mwaka huu,amesema kwamba yungali anatumai mapatano yaweza kufikiwa hadi Januari mwakani, pale Rais george Bush atakapoondoka madarakani.

Lakini ni wachambuzi wachache tu wanoamini kuwa dr.C.Rice aliekutana pia na waziri mkuu wa Israel Ehud Olmert kabla kuonana na bibi Livni,ataweza kuleta mapatano makubwa.

Maendeleo ya kufikia mapatano ya amani yamekwamishwa tangu na machafuko ya wapalestina ,ujenzi wa maskani za wayahudi na waqsi wasi wa kisiasa ulioibuka Israel kutokana na kashfa ya rushua iliomkumba waziri mkuu Olmert.Katika juhudi ya kujenga imani na wapalestina wasi na siasa kali,Israel jana iliwaacha huru wafungwa 200 wa kipalestina.Msemaji wa Israel alisema,

"Leo tutawaachia huru wafungwa 200 wa kipalestina ili kujenga imanik na wapalestina wenye siasa wastani."

Waziri wa nje Bibi Livn, anapigiwa sana upatu katika chama cha Kadima kuchukua wadhifa wa Bw.Olmert na kuwa waziri mkuu mpya.olmert amearifu atajiuzulu baada ya mrithi wake kuchaguliwa.

Baadae hii leo, waziri wa nje wa Marekani anatazamiwa kufanya mazungumzo na rais Mahmud Abbas wa Palestina huko Ramalłlah, Ukingo wa magharibi.