1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Dubai iko kwenye shida. jee falme nyingineza Kiarabu zitaisaidia?

Miraji Othman27 Novemba 2009

Dubai: mikopo inarefushwa muda wa kulipwa

https://p.dw.com/p/KjjV
Majengo marefu katika DubaiPicha: picture-alliance/ ZB

Hadi karibuni, neema ya ufalme wa Dubai, katika Umoja wa Falme za Kiarabu, ilionekana kama hadithi ya alfu uleyla uleyala na usiku alfu moja na nusu; nchi iliong'ara, mbali na dunia yetu hii. Lakini sasa Dubai iko karibu ya kufilisika, kutoka ilivokuwa kama malkia, inaweza ikabadilika kuwa kama msichana maskini.

Kwa miaka, ufalme wa Dubai ulikuwa ni anwani ya kwanza katika eneo la Ghuba ya Uarabu, Majengo marefu na mipango ya fahari, ikiwa na huduma zinazotegemea mapato ya mafuta, yalizistaajabisha nchi za zamani za kiviwanda, au angalau kutoa heshima kwa ufalme huo. Lakini sasa ni wazi. Dubai haiwezi kuyafikia yale mambo yaliojipangia. Ulrick Rathfelder ni bingwa wa kutoka benki kuu ya mikoa ya Hesse na Thüringen hapa Ujerumani anayeshughulikia masuala ya eneo la Ghuba:

" Naam bila ya shaka kulikuweko na miradi ya fahari. Dubai ina uwanja mkubwa kabisa wa ndege katika eneo hilo, pia ina bandari kubwa kabisa. Na pia wakati huo huo inatakiwa Dubai iwe ni kituo cha kitamaduni na cha michezo. Pia katika ujenzi wa majumba iwe inaoongoza katika eneo hilo. Lakini biashara ya ujenzi wa majumba ni kinyume na vile ilivotarajiwa, na sasa biashara hiyo lazima itathminiwe upya."

Kutathminiwa upya maana yake ni kwamba dhamana za serekali za ukopeshaji , Dubai-World, si kwamba zitapigwa jeki bila ya masharti na falme nyingine za umoja huo ili kujikwamua kutoka hali ngumu. Hapo kabla, falme hizo ndugu zilitoa misaada mara nyingi. Dubai ni sehemu ya Umoja wa falme za Kiarabu na ambayo benki yake kuu katika majira ya kiangazi ilitoa dhamana za ukopeshaji zenye gharama ya mabilioni ili kuituliza hali ya mambo. Hata katika siku chache zilizopita, Abu Dhabi, mji mkuu wa Umoja huo wa falme za Kiarabu, ulitoa mikopo. Sasa kuna alama. Mikopo irefushwe muda wake wa kulipwa. Hiyo ina maana Dubai-World lazima izungumze na walioikopesha juu ya muda wa kurefushwa ulipaji wa madeni. Ulrich Rathfelder anaamini kwamba tatizo hilo linaweza kutanzuliwa.

Wiki zijazo zitaonesha vipi mashauriano yatakavokwenda. Serekali ya Umoja wa falme za Kiarabu, bila ya shaka, inazingatia kuibakisha sifa yake nzuri, na pia Dubai. Serekali ya Dubai huenda isisimamishe ulipaji wa madeni.

Hata hivyo, kuna bado raha ya utajiri kuweza kuisawazisha bajeti ya ufalme huo. Mafuta polepole yanapungua huko Dubai, lakini katika falme nyingine utajiri huo bado ungaliko, na mwishowe falme hizo zitaweza kusaidia. Kwanza dhamana za mikopo za Dubai-World zitahitaji ziwekwe katika hali ya nidhamu, ambapo sio msaada wa papo kwa papo utahitajiwa, lakini kwamba kutapendekezwa mikope ipewe muda mrefu zaidi wa kulipwa.

Katika masoko ya hisa hapa Ujerumani,. somo hilo baya la Dubai limekuja katikati ya kipindi cha kuweko imani katika masoko. Makisio ya mwishoni yalikuwa mazuri sana na mwishoni mwa mwaka bei za hisa zilikuwa zinakwenda vizuri. Hivi sasa wanabiashara wengi wa hisa wanaangalia namna ya kuwang'ang'ania sehemu kubwa ya wawekezaji wa Kiarabu katika makampuni ya Kijerumani. Haifikiriwi kwamba wawekezaji hao wa Kiarabu watauza hisa zao walizowekeza hasa katika makampuni ya magari ya Ujerumani.

Katika eneo la Ghuba, kwa ujumla, kuna fedha nyingi, kuweza kufanya mawimbi ya mstikisiko huo yasifike katika nchi nyingine za eneo hilo. Hata hivyo, tatizo la Dubai linaonesha kwamba mzozo wa kifedha duniani hauwezi kwa urahisi kutanzuliwa, kama vile walivofikiria wiki chache zilizopita watu walio na matumaini makubwa yanayopindukia mipaka. Kwa mujibu wa makisio ya mabingwa ni kwamba isikatalike kwamba mtetemeko mwíngine mkubwa katika mfumo wa fedha duniani unaweza ukatokea eneo la Ghuba.

Mwandishi: Buhrs, Hendrik/Othman, Miraji/ZP

Mhariri: Mohammed Abdulrahman