1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Dubai. Kimbunga chaua watu 12.

7 Juni 2007
https://p.dw.com/p/CBuB

Kimbunga Gonu kimepungua nguvu na kuwa upepo mkali kidogo tu wakati kikipita katika njia kuu za kusafirisha mafuta kuelekea Iran leo, lakini kimesababisha vifo vya watu 12 nchini Oman na kusitisha mauzo yote ya nje ya mafuta na gesi kwa siku ya tatu.

Wataalamu wamesema kuwa kimbunga Gonu ambacho kilikuwa katika kiwango cha tano cha kimbunga juzi Jumanne na kufikia katika kiwango cha kwanza jana , hivi sasa ni kimbunga cha kawaida tu cha maeneo ya tropiki.

Kasi ya upepo hivi sasa wa kimbunga hicho ni kiasi cha kilometa 45 kwa saa, kituo cha pamoja cha tahadhari kuhusu vimbunga cha jeshi la Marekani kimesema , na kuongeza kuwa hivi sasa kinaelekea kupungua zaidi.

Kimbunga hicho ambacho hivi sasa kinaelekea Iran kilisababisha mawimbi makubwa baharini, mvua, na upepo pamoja na mafuriko kwa jumla.