1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Dunia yaahidi kuiokoa "mama dunia"

Sekione Kitojo
3 Juni 2017

China na Ulaya zimeahidi Ijumaa (02.06.2017)kuungana na kuokoa kile kansela  Angela Merkel alichokiita "mama yetu dunia", akisimama imara dhidi ya uamuzi wa rais Donald Trump kuiondoa Marekani kutoka mkataba wa Paris.

https://p.dw.com/p/2e4YY
Brüssel China-EU-Gipfel | Tusk & Li Keqiang & Juncker
Viongozi wa Ulaya na China wakubaliana kuhusu mkataba wa kulinda mazingiraPicha: Reuters/O. Hoslet

Mkataba  wa  Paris ni  makubaliano  ya mabadiliko ya tabia  nchi. Hatua  ya  Trump  ilikuwa "makosa  makubwa", amesema  Donald Tusk , mmoja  wa  maafisa wa  ngazi  ya  juu  wa  Umoja  wa  Ulaya.

Mataifa  mengine , ikiwa  ni  pamoja  na  India, yameonesha  ishara ya  kuendelea  na  mkataba  huo . Rais  wa  Urusi Vladimir Putin amesema  kwamba  wakati  Marekani  ilipaswa  kubakia  katika mkataba  huo  uliofikiwa  mwaka  2015 , hatamhukumu Donald Trump.

USA Trump verkündet Ausstieg aus Pariser Klimaschutzabkommen
Rais wa Marekani Donald TrumpPicha: Reuters/K. Lamarque

Trump  alitangaza  kujitoa  kutoka  mkataba  huo  siku  ya  Alhamis , akizungumzia  kuhusu  matamshi  yake  wakati  wa  kampeni  ya urais  nchini  Marekani  ya  "Marekani  kwanza". Alisema  kushiriki katika  mkataba  huo  kutakandamiza  uchumi  wa  Marekani, kupoteza  fursa  za  ajira, kudhoofisha  uhuru  wa  nchi  hiyo na kuiweka  nchi  hiyo  katika  hali  ya  kudumu  ya  kutoweza  kufanya chochote.

Maafisa  katika  utawala  wake, ikiwa  ni  pamoja  na  makamu  wa rais Mike Pence na  mkuu wa  idara  ya  ulinzi  wa  mazingira Scott Pruitt, wamesema  siku  ya  Ijumaa  kwamba  makubaliano  ya  Paris yanaweka  mzigo wa  ziada  kwa  Marekani. "Ni kuhamisha  utajiri kutoka  katika  uchumi  imara  kabisa  duniani  kwenda  katika  nchi nyingine  duniani", Pence alisema  katika  televisheni. Kulikuwa  na mchanganyiko wa  mshangao duniani  kote.

USA Pressesprecher - Scott Pruitt und Sean Spicer
Msemaji wa Ikulu ya Marekani Scott Pruitt (kulia)Picha: picture alliance/AP/dpa/P. Martinez Monsivais

Ufaransa  na  majimbo ya  Marekani

Ufaransa  imesema  itafanya kazi pamoja  na  majimbo  nchini Marekani  pamoja  na  miji  kuendelea  kupambana  dhidi  ya mabadiliko  ya  tabia  nchi. Magavana  wa  mji  wa  New York , Califonia na  Washington  wametangaza  kuunda  kile kitakachofahamika  kama "Muungano  wa  mazingira" ambao utatumia  malengo  ya  mkataba  wa  Paris.

Tasnia yenye  nguvu  ya  viwanda  vya  magari  nchini  Ujerumani imesema  Ulaya  itahitaji  kutathmini  upya  viwango  vyake  vya mazingira kuweza  kuendelea  kuwa  katika  ushindani  baada  ya uamuzi  wa  Marekani , ambao umeuita  kuwa  ni  "wa kusikitisha".

USA New York - Governeur Andrew Cuomo
Gavana wa mji wa New York Andrew CuomoPicha: picture-alliance/AP Photo/A. Harnik

Shirika  la  utabiri  wa  hali  ya  hewa  duniani  linakadiria  kwamba kujitoa  kwa  marekani  kutoka  katika  mkataba  huo  wa  kupunguza utoaji  wa  gesi zinazoharibu  mazingira  kunaweza  kuongeza  ujoto kwa  nyuzi  joto 0.33 Celsius  ifikapo mwishoni  mwa  karne  hii katika  hali  ambayo  itakuwa  mbaya  zaidi.

Kansela  wa  Ujerumani Angela  Merkel , binti  wa  mchungaji ambaye kwa  kawaida huweka imani  yake mbali kidogo  na  umma, amesema  mkataba  huo  ulihitajika "kuhifadhi kuumbwa  kwetu".

"Kwa  kila  mtu  ambaye  hali  ya  baadaye  ya  sayari  yetu ni muhimu, Nasema  tuendelee katika  njia  hii  ili tufanikishe kwa  ajili ya  mama yetu dunia", alisema  huku  alishangiriwa  na wabunge.

Mjini  Paris  rais Emmanuel Macron  aligeuza  kauli  mbiu  ya  rais Trump  ya "Ifanye Marekani kuwa imara  tena",  na  kusema  kwa lugha  ya  Kiingereza  kwamba  muda  umefika  "kuifanya  sayari yetu kuwa imara  tena".

Mwandishi: Sekione  Kitojo / rtre

Mhariri: Bruce Amani