1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Dunia yaahidi kuisaidia Iraq

Mohammed Khelef15 Septemba 2014

Wanadiplomasia wa ngazi za juu duniani wameahidi kuisaidia Iraq katika kupambana na kundi linalojiita "Dola ya Kiislamui" kwa njia yoyote itakayowezekana, ukiwemo msaada wa kijeshi.

https://p.dw.com/p/1DCXR
Viongozi wa mataifa ya Magharibi na Arabuni walioshiriki kongamano la Paris juu ya waasi wanaojiita "Dola la Kiislamu."
Viongozi wa mataifa ya Magharibi na Arabuni walioshiriki kongamano la Paris juu ya waasi wanaojiita "Dola la Kiislamu."Picha: Michel Euler/Reuters

Wawakilishi kutoka takribani nchi na mashirika 30 ya kimataifa, zikiwemo Marekani, Urusi na China, walikusanyika mjini Paris huku taswira ya mateka wa tatu na wa hivi karibuni kabisa akikatwa kichwa ikitawala akili za washiriki wa kongamano hilo.

Mbele ya washiriki hao wa kongamano, ombi la Iraq lilikuwa ni msaada wa kupambana na "Dola la Kiislamu". Rais Fouad Muassem, ambaye kwa pamoja na Rais Francoise Hollande wa Ufaransa, walisimamia mkutano huo wa siku moja.

"Tunachoomba ni operesheni za anga kuendelea kama kawaida dhidi ya maeneo ya kigaidi. Hatupaswi kuwaruhusu kujenga sehemu za kujifichia, lazima tuwafate kokote waliko. Lazima tuwakatie vyanzo vyao vya fedha." Alisema Muassem.

Kwenye taarifa ya pamoja iliyotolewa baada ya mazungumzo, wanadiplomasia walionekana kwa kiasi kikubwa kukubaliana na ombi la Rais Muassem kwa namna ambavyo itaonekana inafaa.

Msaada wa kijeshi

Miongoni mwa yaliyotajwa kwenye msaada huo ni ule wa kijeshi, ambao wamesema "utakwendana na mahitaji yatakayoelezwa na mamlaka za Iraq na kwa mujibu wa sheria za kimataifa na bila kuhatarisha usalama wa raia." Kwa pamoja, washiriki wa kongamano hilo wamekubaliana kimsingi kwamba kundi la Dola la Kiislamu, ambalo kwa sasa linadhibiti asilimia 40 ya Iraq, linapaswa kung'olewa huko.

Konferenz in Paris sucht Wege im Kampf gegen IS-Terror 15.09.2014
Rais Francoise Hollande wa Ufaransa akizungumza kwenye kongamano la Paris juu ya waasi wanaojiita "Dola la Kiislamu."Picha: picture-alliance/dpa/Yoan Valat

Rais Hollande aliwaambia washiriki kwamba dunia haina njia nyengine zaidi ya kulishinda kundi la Dola la Kiislamu. "Vita vya watu wa Iraq dhidi ya magaidi ni vita vyetu pia, na tunapaswa kushirikana na hili ndilo lengo la jumla la kongamano hili. Tunapaswa kusimama pamoja na serikali ya Iraq, kwa uwazi, kwa utiifu, na kwa umadhubuti, na hakuna wakati wa kupoteza" Alisema Hollande.

Muda mchache kabla ya kuanza kwa kongamano, Ufaransa ilikuwa imetangaza kutuma ndege zake za kijeshi kuungana na zile za Uingereza kwenye kampeni inayoongozwa na Marekani dhidi ya kundi la Dola ya Kiislamu.

Syria haikujumuishwa

Hata hivyo, kongamano hilo lililofanyika baada ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry, kumaliza ziara yake ya Ghuba na Mashariki ya Kati kusaka uungwaji mkono wa kimataifa, halikuitaja kabisa Syria, ingawa nayo kama ilivyo Iraq, robo ya ya ardhi yake imetekwa na inakaliwa na kundi hilo la kigaidi.

Rais Francoise Hollande wa Ufaransa akimkaribisha mwenzake wa Iraq, Fouad Muassem, kwenye kongamano la Paris juu ya waasi wanaojiita "Dola la Kiislamu."
Rais Francoise Hollande wa Ufaransa akimkaribisha mwenzake wa Iraq, Fouad Muassem, kwenye kongamano la Paris juu ya waasi wanaojiita "Dola la Kiislamu."Picha: Reuters/John Schults

Iran imeukosoa mkutano huo ikisema kwamba hakuna suluhisho lolote dhidi ya tatizo la Dola la Kiislamu litakalofanikiwa bila ya ushiriki wa serikali ya Syria. Kama ilivyo Syria, Iran nayo haikualikwa kwenye kongamano hilo.

Kongamano la leo limefanyika wiki moja kabla ya mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, na kwa mujibu wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Frank-Walter Steinmeier, mikutano mingine itafanyika hivi karibuni kwa ajili ya kuyaimarisha maazimio yaliyotolewa leo, ukiwemo ule utakaozungumzia vyanzo vya kifedha ya kundi la Dola la Kiislamu utakaoitishwa na Bahrain.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/AP
Mhariri: Saumu Yusuf