1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Dunia yamlilia Stephen Hawking

Mohammed Khelef
14 Machi 2018

Dunia ya wataalamu wa sayansi na wavumbuzi inaomboleza kifo cha mmoja wa wanafizikia wakubwa wa anga wa zama hizi, Stephen Hawking, aliyefariki dunia nyumbani kwake Cambridge, Uingereza, akiwa na miaka 76.

https://p.dw.com/p/2uHz5
Britischer Wissenschaftler Stephen Hawking ist tot
Picha: Getty Images for Breakthrough Prize Foundation/B. Bedder

Mnamo mwaka 2014, Kituo cha Anga za Juu cha Marekani (NASA) kilizungumza na Profesa Hawking juu ya maisha ya angani, naye akasema kuwa anakhofia mustakabali wa wanaadamu kwani sayari ya dunia inatishiwa sana na majanga mengi, yakiwemo ya kimazingira na ongezeko kubwa la idadi ya watu, sambamba na kumalizika kwa rasilimali zake.

"Tuna wajibu wa kuchukuwa hatua za mapema na lazima tuwe na Mpango B," alisema wakati huo, ikiwa ni miaka kumi tangu yeye binafsi kupanda chombo cha angani ambako kwa dakika kumi nzima alielea kwenye anga za ajuu, tukio alilokuja kuliita kuwa kipimo cha ladha ya uhuru ambayo hasa ndiyo mwanaadamu anayopaswa kuwa nayo.

Mpango B alioutaja hapa ni imani yake kwamba ili wanaadamu waweze kukabiliana na changamoto kubwa zinazoikabili sayari hii ya dunia, basi ni lazima wazitawale sayari nyengine zilizomo kwenye mzunguko wa jua, kama ile ya Zuhra.

Profesa Hawking aliamini kuwa maisha yanapaswa kuendelea kwenye sayari nyengine.

Mapema alfajiri ya leo, mauti yaliyachukuwa maisha ya mwanasayansi huyo wa miaka 76 na kuizima ndoto yake ya Mpango B, lakini si kabla ya kujenga misingi imara ya kufikiwa kwa ndoto hiyo siku moja, alitangaza msemaji wa Chuo Kikuu cha Cambridge, ambako Profesa huyo alikuwa mwalimu kwa zaidi ya miongo mitatu.

Dunia yamlilia

Kikiomboleza kifo cha mwanasayansi huyu, kituo cha NASA kimeandika kwenye mtandao wake wa Twitter kwamba nadharia za mwanasayansi huyo ziliufungua ulimwengu wa uwezekano wanaoutafiti.

"Nauendelee kuruka kama superman kwenye anga za juu kama ulivyowaambia wanaanga wetu mwaka 2014," ilisomeka kauli ya NASA.

Karikatur von Vladdo, Stephen Hawking: Die letzte Reise

Hawking atakumbukwa daima kwa maandishi yake ya kusisimua kuhusu mafumbo ya anga za juu, wakati na kile alichokuwa akikiita 'mashimo meusi'.

Kitabu chake alichokiita "Muhtasari wa Wakati" kilikuja kuongoza kwa mauzo duniani, na kumfanya kuwa mmoja kati ya wanasayansi waliotukuzwa kote duniani baada ya Albert Einstein.

Kwenye tamko lao, wanawe watatu - Lucy, Robert na Tim - wamesema kuwa baba yao alikuwa mwanasayansi mkubwa kabisa na mtu asiye wa kawaida ambaye kazi na kumbukumbu zake zitaishi kwa miaka mingi ijayo.

Kauli kama hiyo imetolewa na Waziri Mkuu wa Uingereza, Theresa May, ambaye amemsifu Hawking kuwa fahari ya ufalme huo.

Nchini China, ambako profesa huyo anachukuliwa kama mungu wa fizikia, mamilioni ya watu wamejitokeza mitandaoni kuomboleza kifo chake.

Miaka miwili iliyopita, Hawking alifungua akaunti kwenye mtandao wa kijamii wa Weibo, ambapo alikuwa akituma taarifa zake kwa Kiingereza na Kichina.

Akaunti hiyo ilipata mashabiki milioni moja ndani ya masaa machache tu tangu kuifungua na kufikia sasa ina mashabiki milioni tano, ambao wanamuita kwa jina la Hawking Dada, au Mjomba Hawking. 

Tangu kifo chake kitangazwe, akaunti yake ina zaidi ya maoni 200,000 kutoka China, wengi wakizungumzia kile wasemacho ni kuanguka kwa nyota kubwa kutoka angani, wakisema kuwa ugonjwa wake wa kulemaa viungo vyote vya mwili tangu akiwa na miaka 21, kamwe haukuwa kikwazo kwake cha kusonga mbele na kuutafiti ulimwengu wa angani. 

Mwandishi: Mohammed Khelef/AP/Reuters
Mhariri: Iddi Ssessanga