1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Duru ya pili ya Kombe la dunia imemalizika:

30 Juni 2010

Spain imeitoa Ureno 2:1 na Paraguay imeirudisha japan nyumbani kwa mabao 5-3.

https://p.dw.com/p/O6aM
"Nyota nyeusi" yan'gara Afrika nzima.Picha: DW

Kwa ushindi wa hapo jana wa Paraguay dhidi ya Japan, katika changamoto za mikwaju ya penalty na wa mabingwa wa ulaya-Spain dhidi ya jirani yake Ureno, duru ya pili ya kutoana imekamilika na leo na kesho ni mapumziko katika kombe la dunia 2010.

Timu 8 zitazoani nafasi ya nusu-finali kuanzia keshokutwa Ijumaa pale Ghana itakapochuana na Uruguay, zinajulikana:1 inatoka Afrika-Ghana.Tatu zinatoka ulaya:Ujerumani,mabingwa wa ulaya Spain na Holland.4-moja zaidi kuliko bara lolote, zinatoka Amerika Kusini:Brazil,Argentina,Paraguay na Uruguay.

Kutoka kambi ya Black Stars-Ghana, imefahamika kwamba, Isaac Vorsah, atakuwa fit kuteremka uwanjani Ijumaa hii dhidi ya Uruguay. Wasi wasi pia umeondoka juu ya mastadi wengine wa Ghana walioumia kama vile stadi wa kiungo-Kevin -Prince Boateng,nahodha John Mensah na hata mshambulizi wao Asamoah Gyan. Hatahivyo, Ghana, itabidi kucheza bila ya Andre Ayew-mtoto wa Abedi Pele,nahodha wao wa zamani,lakini stadi wa Inter Milan, Sulley Muntari, anatazamiwa kujaza pengo lake.

Taarifa kutoka kambi ya Black Stars,zinasema Asamoah Gyan anataka kuhamia Premier League-ligi ya Uingereza kutoka clabu yake ya Ufaransa ya Rennes.

Kutoka kambi ya Ujerumani, yenye miadi Jumamosi hii na Argentina,taarifa zinasema stadi wao wa kiungo Mesut Özil,anasakwa na FC Barcelona,ili kucheza bega klwa bega na Lionel Messi.

Barcelona, itayari kumuajiri Özil hivi sasa lakini , itamuachia kuendelea kuichezea klabu yake ya Werder Bremen kwa mwaka mmoja zaidi hadi 2011. Bremen, imekuwa ikijitahidi kurefusha mkataba wa chipukizi huyo mwenye umri wa miaka 21,lakini , hadi sasa hakuitikia.

Kutoka Kambi ya Ujerumani, huko Afrika Kusini, imefahamika kwamba, Jumamosi hii,Kanzela Angela Merkel, ameamua kufunga safari kwenda Afrika Cape Town,Kusini kuiangalia Ujerumani ikimenyana na Argentina uwanjani kuania tiketi ya nusu-finali.

Wakati FIFA ikiionya serikali ya Ufaransa, kutoingilia shughuli za Shirikisho la dimba la Ufaransa,kocha wa Les Blue,timu ya Taifa aliefedheheka Raymond Domenech na rais wa zamani wa Shirikisho la dimba la Ufaransa, Jean-Pierre Escalettes wanafika leo mbele ya wabunge kujieleza ilikuaje mambo yakaenda kombo kwa makamo hao wa Kombe la dunia ?

Wakati bado haijulikani Kombe la dunia Julai 11, litakwenda wapi,wevi wameiba vikombe 7-bandia vya FIFA karibu na uwanja utakaochezewa wa finali Julai 11.

Katika mkutano na waandishi habari jana, Kamishna wa polisi wa Afrika Kusini, Bheki Cele, amearifu kwamba wizi wa vikombe hivyo 7 vinavyofanana na Komb lenyewe la dunia huko Johannesberg, ni kazi ya ndani na inachunguzwa.

Mwandishi: Ramadhan Ali/AFPE

Mhariri: Abdul-Rahman Mohammed