1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wawili watashindana katika duru hiyo ya pili

20 Oktoba 2017

Katika uchaguzi uliofanyika Oktoba 10, Weah alipata asilimia 38.4 ya kura na mpinzani wake Boakai alipata asilimia 28.8 ya kura hizo

https://p.dw.com/p/2mEkL
Wahlen in Liberia 20.12.2014
Picha: AFP/Getty Images/Z. Dosso

Licha ya  vyama vikuu vitatu vya upinzani nchini Liberia kulalamika kuwa kulifanyika mchezo mchafu wakati wa uchaguzi, Tume ya uchaguzi nchini humo imetangaza matokeo ya uchaguzi uliofanyika Oktoba 10 yakibainisha kuwa mwanasoka wa zamani, George Weah na Makamu wa rais wa nchi hiyo, Joseph Boakai, watachuana katika uchaguzi wa  duru ya pili mnamo Novemba.

 Katiba ya nchi hiyo inasema kuwa ili mgombea wa urais atangazwe mshindi, ni lazima awe amepata angalau asilimia 50 ya kura zote hata hivyo, hakuna mgombea yeyote kati ya 20, aliyefikisha kiwango hicho.

Akisoma matokeo hayo jana, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi nchini humo, Jerome Korkoyah ametangaza kuwa Weah alipata kura 596,037 ikiwa ni asilimia 38.4 ya kura zote na Makamu wa Rais wa sasa, Boakai amepata kura 446,716 ikiwa ni asilimia 28.8 kati ya kura 1,641,922  au asilimia 95 ya kura zote.

``Kama mlivyosikia, hakuna mgombe yeyote aliyepata zaidi ya asilimia 50 ya kura zote, na kutokana na katiba inatakiwa kuwepo kwa mchuano kati ya wagombea wawili, hivyo tunatangaza uchaguzi wa wa mara ya pili utakaofanyika Novemba 7,. Utakuwa kati ya George Weah  wa chama cha CDC na Boakai wa chama cha Unity.`` amesema  Korkoyah

 Mwenyekiti huyo  alitangaza rasmi  kuwa kampeni za uchaguzi zimeanza na zitahitimishwa usiku wa Jumapili ya Novemba 5.

 Boakai na Weah washawishi vyama viwape ushirikiano

 Awali kabla ya kutangazwa kwa matokeo ya mwisho ya uchaguzi huo, Boakai wa chama cha Unity, kilichopo madarakani kwa sasa na George Weah wa chama kikuu cha upinzani cha Democratic Change, walijaribu kuvishawishi vyama vingine vya upinzani ili viwape ushirikiano katika duru hiyo ya pili.

 Wakati Weah na Boakai wamejikita zaidi katika mbinu na mipango ya kupata ushindi katika duru ya pili ya Novemba, kiongozi mkuu wa chama cha Liberty Party, Charles Brumskine anayewania urais kwa mara ya tatu sasa  anataka uchaguzi huo urudiwe.

 Tangu matokeo hayo yaanze kutangazwa, Brumskine alilalamika kuwa kulikuwa na mchezo mchafu na kuwa ameibiwa kura zake katika uchaguzi huo uliomalizika hivi karibuni na kugubikwa na malalamiko lukuki.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa kampuni ya Coca Cola, anayetajwa kama ´mgeni katika siasa za Liberia´´, Alexander Cummings, wa chama cha ANC, pamoja na mshirika wa aliyekuwa Rais wa nchi hiyo, Charles Taylor,  Benon Urey, wao pia wanamuunga mkono Brumskine.

 Malalamiko  yao ni kuwepo kwa udanganyifu mkubwa na wakiitaka tume ya uchaguzi kuzingatia malalamiko yao na kuchukua hatua au wataipeleka mahakamani tume ya uchaguzi.

 ``Chama cha Liberty ni chama kinachozingatia sheria ndiyo sababu ya sisi kuchukua uamuzi wa kwenda mahakama iwapo malalamiko yetu hayatafanyiwa kazi`` amesema Brumskine katika mkutano na waandishi wa habari jana.

 Mwenyekiti wa tume hiyo, Korkoya hata hivyo hakuzungumzia chochote kuhusu malalamiko yanayotolewa na vyama hivyo.

 Wakati huo huo, Rais wa nchi hiyo, Ellen Johnson Sirleaf anatarajiwa kulihutubia taifa leo baadaye ikiwa ni saa chache baada ya tume ya uchaguzi kutangaza matokeo ya mwisho.

 Mwandishi: Florence Majani

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman