1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Matokeo yanaashiria huenda uchaguzi ukaenda duru ya pili

Amina Mjahid
12 Machi 2018

Mgombea wa urais kutoka upande wa upinzani amechukua uongozi akiwa mbele ya mgombea wa chama tawala hali inayoonesha hakuna mgombea wa wazi aliyefanikiwa kupata asilimia 55 ya kura kushinda duru ya kwanza.

https://p.dw.com/p/2u8og
Sierra Leone  Wahlen 2018
Picha: DW/Abu-Bakarr Jalloh

Tume ya uchaguzi nchini humo imetangaza kuwa mgombea wa upinzani Julius Maada Bio amejipatia asilimia 43.6 ya kura, huku mgombea wa chama tawala Samura Kamara aliyewahi kuwa waziri wa mambo ya nje wa Sierra leone akijikusanyia asilimia 42.6 ya kura katika kura jumla ya asilimia 75 zilizokwisha hesabiwa hadi kufikia sasa.

Mgombea mwengine anayetokea muungano wa kitaifa aliyekuwa mwanadiplomasia wa Umoja wa Mataifa Kandeh Yumkella, amejipatia asilimia 6.69 ya kura, huku Samuel Sam-Sumana akipata asilimia 3.4 ya kura. Katika uchaguzi huu wagombea 12 wakiwemo wanawake wawili wanawania kiti cha urais. 

Matokeo kamili yanatarajiwa kutolewa katika siku chache zijazo lakini duru ya pili ya uchaguzi huenda ikafanyika kutokana na kwamba mpaka sasa hakuna mgombea aliyepata asilimia 55 ya kura inayohitajika ili kutangazwa mshindi. 

Wahlen in Sierra Leone  2018
Picha: DW/A.-B. Jalloh

Kwa upande wake rais Ernest Bai Koroma, hawezi tena kugombea baada ya mihula yake miwili ya miaka mitano mitano kumalizika, lakini alimteua Samura Kamara kama mrithi wa kiti chake hicho kwa tiketi ya chama tawala cha All Peoples Party (APC). 
Chama hicho cha APC na kile cha Bio cha Sierra Leone Peoples Party vimekuwa vikipokezana kuiongoza Sierra Leone tangu nchi hiyo ijipatie uhuru wake kutoka kwa Uingereza mwaka 1961. 

Huku hayo yakiarifiwa siku ya Ijumaa waangalizi wa kura kutoka Umoja wa Ulaya waliuelezea uchaguzi huo kuwa wa wazi, kuaminika na uliyopangwa vizuri. Lakini pia walielezea wasiwasi wao juu ya visa vya vurugu na kutishwa vilivyoangaziwa na shirika la kimataifa la la kutetea haki za binaadamu na maendeleo lililo na makaazi yake mjini Freetown. 

Hata hivyo duru ya pili ya uchaguzi inatarajiwa kufanyika wiki mbili baada ya matokeo kamili kutangazwa. Sierra leone taifa linalotegemea mauzo ya nje na lililo tajiri kwa madini lakini ni moja ya mataifa masikini Magharibi mwa Afrika, lipo katika hali mbaya kiuchumi kufuatia ugonjwa wa Ebola uliolikumba kuanzia mwaka 2014 hadi mwaka 2016, hali iliyosababisha bidhaa zao kutonunuliwa na kuwafukuza wawekezaji wa kigeni.

Aidha mshindi wa uchaguzi huu atakuwa na kibarua kigumu cha kuufufua uchumi wa nchi hiyo ambapo baada ya kumalizika kwa mapigano ya wenyewe kwa wenyewe miaka ya 90 limekumbwa na kushuka bei ya madini yake ya chupa cha pua ambayo ndio bidhaa yake inayoiuza nje kwa wingi. 

Mwandishi: Amina Abubakar/Reuters/AFP  
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman