1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa Afrika Mafgharibi wako Gambia

Admin.WagnerD20 Januari 2017

Viongozi wa Afrika Mafgharibi wako Banjul Gambia kumpa kiongozi wa nchi hiyo nafasi ya mwisho kujiuzulu kwa hiyari  kabla vikosi vya kanda hiyo ambavyo vimeingia nchini humo kumuondowa madarakani kwa nguvu. ­­­­­­­­­­

https://p.dw.com/p/2W6lT
Senegal Gambia Panzer vor Grenze
Picha: picture-alliance/AP Photo/S. Cherkaoui

Viongozi wa Afrika Mafgharibi leo hii wako Banjul mji mkuu wa Gambia kumpa kiongozi wa nchi hiyo nafasi ya mwisho kujiuzulu kwa hiyari  kabla vikosi vya kanda hiyo ambavyo tayari vimeingia nchini humo kumuondowa madarakani kwa nguvu. ­­­­­­­­­­

Vikosi kutoka jumuiya ya kanda  hiyo ya ECOWAS vikiongozwa na Senegal na Nigeria vimeingia Gambia hapo jana kufuatia ombi la rais mpya mteule Adama Barrow ambaye imebidi aapishwe katika ubalozi wa Gambia nchini Senegal hapo jana wakato Jammeh akiendelea kun'gan'gania madaraka .

Majeshi hayo ya Afrika magharibi yamempa Jammeh hadi mchana huu kun'gatuka kabla ya kuendelea ya kusonga mbele katika mji mkuu wa nchi hiyo Banjul.

Mji huo ulikuwa kimya wakati wa usiku baada ya mamia ya wananchi wa Gambia kusheherekea kuapishwa kwa Barrow na kupelekwa kwa vikosi vya Jumuiya ECOWAS nchini mwao ambayo ni kituo mashuhuri kwa watalii wa Ulaya na iliyotawaliwa na Jammeh kwa mkono wa chuma.

Aliou Souane mfuasi wa Barrow amesema "Ilikuwa ni rais Jammeh aliyeandaa uchaguzi awali alikubali na kumpongeza mshindani wake. Kutenguwa utambuzi wake wa kukubali kushindwa kunaonyesha kwamba ni dikteta anayeamuwa kila kitu."

Suala la kubakia madarakani halipo

Senegal Gambias neuer Präsident Adama Barrow
Rais mpya wa Gambia Adama Barrow akiapishwa nchini SenegalPicha: picture-alliance/AP Photo

Marcel de Souza mkuu wa kamisheni ya jumuiya ECOWAS amesema Rais Alpha Conde wa Guinea amekwenda Banjul na viongozi wenzake wa Mauritania na Liberia kujaribu kumshawishi Jammeh kwenda Guinea kabla ya kuamuwa nchi ya kwenda kuishi uhamishoni.de Souza amesema suala la kubakia madarakani halipo.

Jammeh awali alikubali kushindwa na Barrow katika uchaguzi wa mwezi wa Disemba kabla ya kutenguwa uamuzi wake huo kwa kusema uchaguzi huo ulikuwa na mapungufu na kwamba ataendelea kubakia madarakani hadi hapo utakapoitishwa uchaguzi mpya.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hapo jana limeelezea kuunga mkono kwao mataifa ya Afrika Magharibi kuhakikisha kwanza kwa njia ya kisiasa kuheshimiwa kwa matakwa ya wananchi kuhusiana na uchaguzi wa rais wa hivi karibuni nchini Gambia.

Barrow ametambuliwa kama rais mpya wa Gambia na mataifa makubwa duniani na Jammeh anazidi kutengwa nchini mwake wakati mawaziri wakiitelekeza kambi yake.

Mwandishi : Mohamed Dahman/Reuters

Mhariri: Yusuf Saumu