1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ECOWAS yawapa wanajeshi wa Mali siku tatu

30 Machi 2012

Jumuiya ya Uchumi ya Afrika Magharibi ECOWAS imetoa saa sabini na mbili kwa wanajeshi waliofanya mapinduzi nchini Mali kurejesha utawala wa kidemokrasia vinginevyo itaiwekea vikwazo vikali vya kiuchumi nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/14VAP
Mwenyekiti wa ECOWAS, Rais Allassane Ouattara wa Cote d'Ivoire.
Mwenyekiti wa ECOWAS, Rais Allassane Ouattara wa Cote d'Ivoire.Picha: Reuters

Vikwazo vya kiuchumi dhidi ya Mali kutoka kwa mataifa jirani ni moja kati ya hatua kali zinazochukuliwa kujaribu kuurejesha utawala wa Kidemokrasia uliopokonywa toka mikononi mwa Rais Amadou Touman Toure wa nchi hiyo wiki mbili zilizopita.

Jumuiya hiyo inatarajia kufunga mipaka yake yote ambayo hutumiwa na Mali katika shughuli za kiuchumi pamoja na kutimiza azma yake ya kuzifunga akaunti za nchi hiyo kama wanajeshi hao hawatatii amri ya kuachia madaraka jambo ambalo litadhoofisha kwa kiasi kikubwa uchumi wa nchi hiyo ambayo hupitisha mafuta yake katika nchi jirani ya Cote d`Ivoire.

Mali kuzuiwa kutumia bandari

Rais wa Kamisheni ya ECOWAS, Kadre Desire Ouedrago, aliwaambia waandishi wa habari katika mjini Yamoussoukro, Cote d'Ivoire, kuwa pamoja na kuifungia nchi hiyo mipaka, nchi zote 15 za jumuiya hiyo zitaizuia Mali kutumia bandari zake isipokuwa matumizi ya kupitisha misaada ya kibinadamu pekee.

Kikundi cha wanajeshi wa Mali kilichomuondoa madarakani Rais Amadou Toure.
Kikundi cha wanajeshi wa Mali kilichomuondoa madarakani Rais Amadou Toure.Picha: Reuters

Rais huyo anasema kuwa mpango wa benki kuu ya jumuiya hiyo kuzifunga akaunti za Mali, tayari umeshaanza kufanya kazi kwa kutolewa amri kwa benki hiyo kutopeleka fedha katika akaunti za benki za kibiashara za umma nchini humo.

Jumuiya hiyo ilisimamisha uwanachama wa Mali wiki iliyopita muda mfupi baada ya wanajeshi kuupindua uongozi wa kidemokrasia nchini humo kwa madai kuwa umeshindwa kutimiza matakwa ya wananchi wa Mali.

Jumuiya za kimataifa zaiwekea vikwazo Mali

Hadi sasa Jumuiya na taasisi za kimataifa duniani tayari zimekwishaiwekea nchi hiyo vikwazo vya kiuchumi. Umoja wa Ulaya na Marekani tayari zimesitisha utoaji wa fedha za miradi yote ya maendelo nchi humo na kubakisha misaada ya kiutu pekee. Benki ya Dunia na Benki ya Maendeleo ya Afrika pia zimo katika taaisisi za kimataifa zilizoiwekea vikwazo nchi hiyo.

Rais wa Mali aliyeondolewa madarakani, Amadou Toumani Toure.
Rais wa Mali aliyeondolewa madarakani, Amadou Toumani Toure.Picha: AP

Uamuzi huo wa ECOWAS wa kuwapa siku tatu wanajeshi wa Mali kurejesha demokrasia nchini humo ulifanywa na marais watano wa nchi mwanachama wa jumuiya hiyo ambao hapo kabla walikuwa wakutane katika mji mkuu nchi hiyo Bamako siku ya Alhamis.

Viongozi hao walilazimika kubadili njia na kukutana nchini Cote d´Ivoire baada ya kiongozi wa mapinduzi hayo kapteni Amadou Haya Sanogo kukataa viongozi hao kutua katika uwanja wa ndege mjini humo kitendo ambacho ECOWAS imekichukulia kama ukaidi na hivyo kumweka katika kundi la mtu asiyestahili kufanya nae majadiliano.

Mwandishi: Stumai George/APE/DPAE
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman