1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaEcuador

Ecuador yapiga kura ya maoni kupambana na uhalifu wa magenge

Bruce Amani
21 Aprili 2024

Raia wa Ecuador wamepiga kura ya maoni leo iliyopigiwa debe na kiongozi wa nchi hiyo kama njia ya kukabiliana na magenge ya uhalifu yanayohusishwa na wimbi kubwa la machafuko nchini humo.

https://p.dw.com/p/4f1Gh
Ecuador / Kura ya Maoni
Raia wa Ecuador akipiga kuraPicha: Boris Romoleroux/Agencia Prensa-Independiente/IMAGO

Maswali mengi kati ya 11 yaliyoulizwa wapiga kura yanalenga katika kuimarisha hatua za usalama. Mapendekezo hayo ni pamoja na kulitumia jeshi katika mapambano dhidi ya magenge hayo, kulegeza vikwazo vya kuwarejesha nyumbani watuhumiwa wa uhalifu na kuongeza muda wa vifungo vya jela kwa wanaopatikana na hatia ya ulanguzi wa dawa za kulevya.

Ecuador, ambayo kwa muda mrefu imezingatiwa kuwa mojawapo ya nchi zenye amani zaidi za Amerika Kusini,imetikiswa katika mwaka wa hivi karibuni na wimbi la machafuko, kwa kiasi kikubwa yakisambaa kutoka nchi jirani ya Colombia, ambayo ni mzalishaji mkubwa zaidi duniani wa dawa za kulevya aina ya kokeini.

Mwaka jana, kiwango cha mauaji nchini humo kilifikia hadi vifo 40 kwa kila watu 100,000. Rais Daniel Noboa mwenye umri wa miaka 36 amepata uungwaji mkono wa wananchi kwa kukabiliana vikali na magenge ya uhalifu.

Mnamo Januari mwaka huu, watu wenye silaha waliojifunika nyuso zao, baadhi yao wakiamriwa na walanguzi wa dawa za kulevya waliofungwa gerezani, waliwatia hofu wakazi na kuchukua udhibiti wa kituo cha televisheni wakati kikiwa hewani katika tukio ambalo halijawahi kushuhudiwa.