1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

El Baradei asisitiza diplomasia juu ya Nuklia

20 Aprili 2009

Iran na Korea Kaskazini zatolewa mwito kuacha ubishi kuhusu miradi yao ya Nuklia

https://p.dw.com/p/Hapj
Mkuu wa shirika la kimataifa la nishati ya Nuklia IAEA Mohamed El-BaradeiPicha: AP

Mkutano wa siku tatu wa kimataifa juu ya Nuklia unaendelea huko Beijing China ambako mkuu wa shirika la kudhibiti technologia ya nishati hiyo la IAEA Mohammed El Baradei amesisitiza juu ya haja ya kufanyika mazungumzo zaidi na kuwepo hali ya kuaminiana katika kuitatua migogoro ya Nuklia na Korea kaskazini pamoja na Iran.

Shirika hilo la Kimataifa kwa upande mwingine limetoa mwito kwa Marekani kubakia katika mazungumzo ya kidiplomasia na nchi hizo mbili.

Mkurugenzi mkuu wa shirika la kimataifa la kudhibiti technologia ya Nuklia IAEA Mohammed El Baradei amesema katika kikao kinachoendelea huko Beijing juu ya Nukilia kwamba nchi za magharibi zinabidi kuendelea na hatua ya kufanya mazungumzo na nchi za Iran na Korea kaskazini kuhusiana na miradi yao ya Kinuklia .

Symbolbild Atomstreit Korea
Korea kaskazini ilirusha roketi yake na kuzusha hisia kali katika nchi za magharibiPicha: DW/AP

Pia amesema anamatumaini kwamba Korea kaskazini nchi ambayo iliwatimua waangalizi wa shirika hilo la Iaea wiki iliyopita itawaalika tena hivi karibuni na kuepusha mvutano na kwamba Iran kwa upande wake itaupokea mkono wa urafiki ulionyooshewa hivi karibuni na Marekani kwa kuweka wazi mipango yake ya Kinuklia ikiwa ni pamoja na kuwaruhusu waangalizi wa shirika hilo kufanya ukaguzi wa kina.

''Ili shirika hili liweze Kupiga hatua Iran inabidi itoe maelezo ya kuridhisha na kuruhusu kuangalia stakabadhi,maeneo pamoja na kuhojiwa wahusika katika masuala yote yaliyosalia''

Aidha Elbaradei ametoa ujumbe wake kwa nchi za Korea kaskzini na Iran akisema kwamba ushirikiano ndio jambo muhimu katika kuitatua migogoro ya kinuklia.Ama kuhusu Iran kiongozi huyo aliongeza kusema-

''Kwa mara nyingine naitolea mwito Iran kutekeleza mapendekezo yote yaliyotolewa ili kujenga imani kuhusu mpango wake wa kinuklia mapema iwezekanavyo na kuitatua hali ya mvutano iliyopo hivi sasa''

Korea kaskazini na Iran zimetakiwa kutambua kwamba njia pekee ya kuyatatua masuala ya Nuklia sio kupitia maguvu.

Kwa upande mwingine IAEA limesema haliwezi kusimamia moja kwa moja mazungumzo juu ya mivutano ya Nuklia na Korea kaskazini na Iran nchi ambazo Utawala wa zamani wa Marekani ukiongozwa na Goerge W Bush uliziweka katika kundi la mihimili ya maovu.

Hata hivyo matamshi ya Elbaradei leo hii huenda yakaongezea nguvu miito iliyotolewa awali ya kutaka kuzingatiwa subira na mazungumzo katika pande zote zinazohusika.

Aidha amefahamisha kuwa na matumaini kwamba Korea Kaskazini itajiunga katika mazungumzo ya pande sita pamoja na Marekani,Japan,Urussi,Korea Kusini pamoja na China.

Korea Kaskazini iliwatimua waangalizi wa shirika la IAEA wiki iliyopita na kutangaza kujiondoa katika mazungumzo hayo pamoja na kutishia kuanzisha upya shughuli za kinu chake cha kinuklia cha Yongbyong ambacho ilikubali kukifunga baada ya kuafikiana na nchi za magharibi kwamba badala yake itapewa msaada wa kiuchumi.

Mohamed El Baradei ameutaka ulimwengu kuiangalia Korea Kaskazini kama nchi yenye nguvu za Kinuklia na hivyo basi ni lazima ishawishiwe kurudi katika meza ya mazungumzo haraka iwezekanavyo. Matamshi hayo ambayo ameyatoa kandoni mwa mkutano wa kimataifa unoendelea juu ya Nuklia yameishutua Marekani ambayo haiitambua nchi hiyo kama nchi yenye nguvu za kinuklia.

Mwandishi: Saumu Mwasimba/IPS

Mhariri- Mohd Abdul-Rahman