1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Elimu kwa wote: Elimu katika ulimwengu wa Kiarabu

21 Juni 2012

Vijana ndio kundi kubwa la watu walioshiriki katika maandamano ya ulimwengu wa Kiarabu. Hii ni kwa sababu hawana nafasi za ajira, licha ya kwamba wengi wao wameelimika kuliko hata wazazi wao.

https://p.dw.com/p/15JIK
Irakische Proteste für den arabischen Frühling
Irakische Proteste für den arabischen FrühlingPicha: DW/Karlos Zurutuza

Picha za maandamano yaliyofanyika hivi karibuni katika miji ya Cairo na Tunis zilikuwa zikionyesha wahitimu wa vyuo vikuu waliokuwa wameshikilia vyeti vya taaluma zao mkono mmoja huku mkono mwingine ukiwa umekunjwa kama ngumi. Licha ya kuwa na ujuzi wa hali ya juu, wasomi wengi wa Kiarabu walio vijana wanashindwa kupata ajira. Tatizo la ukosefu wa ajira haliwaathiri vijana hawa pekee yao.

Katika ulimwengu wa Kiarabu ulio wa kihafidhina, ni vigumu sana kwa kijana kuingia katika uhusiano wa kimapenzi au hata kuwa na familia bila ya kuwa na kipato cha kutosha. Kwa sababu hiyo haishangazi kuona kwamba vijana wasomi waliamua kuonyesha hasira zao kupitia maandamano. Wao wanadai kwamba sera ya elimu na uchumi katika nchi za Kiarabu zilizomo Kaskazini mwa bara la Afrika ndizo zilizowafanya wakose ajira.

Maandamano dhidi ya serikali ya Tunisia
Maandamano dhidi ya serikali ya TunisiaPicha: picture-alliance/dpa

Ukuaji wa kiuchumi bila nafasi za kazi

Hili linashangaza kwani katika miaka iliyopita, nchi za Kiarabu zimekuwa zikiwekeza kiasi kikubwa cha fedha katika nyanja ya elimu na hivyo kuifanya idadi ya wahitimu wa vyuo vikuu ipande kwa kasi. Pamoja na hayo, uchumi wa nchi za Kiarabu umeonyesha kukua kwa kiasi kikubwa katika kipindi cha miaka kumi iliyopita. Lakini serikali zilishindwa kuzielekeza sera zake za viwanda na uwekezaji ili ziweze kutengeneza nafasi za kazi kwa wahitimu wa vyuo vikuu vya nchi hizo.

Mfano mmojawapo ni nchi ya Tunisia ambapo uchumi umekuwa ukiongezeka kwa kiwango kilicho juu ya wastani katika miaka kadhaa iliyopita. Uchumi wa nchi hiyo unategemea zaidi utalii na uuzaji wa nguo na vitambaa katika nchi za Ulaya. Hata hivyo, wasomi vijana wa Tunisia wameshindwa kupata kazi katika sekta ya viwanda au hata katika sekta ya nguo. Mbali na sera za uchumi za Tunisia zinazoegemea upande mmoja, rushwa pamoja na usimamizi mbaya wa shughuli za kiuchumi ni miongoni mwa mambo yanayokwamisha utengenezaji wa ajira kupitia wawekezaji binafsi.

Wanafunzi wa chuo kikuu cha Muscat, Oman
Wanafunzi wa chuo kikuu cha Muscat, OmanPicha: picture-alliance/dpa

Hakuna mabadiliko katika shule na vyuo

Licha ya juhudi kubwa zilizofanywa na mataifa ya Kiarabau katika kuwapa raia mafunzo ya kusoma na kuandika, mataifa hayo yameshindwa kubadili mifumo ya shule na mafunzo ya kazi ili iweze kuendana na sera za kazi. Hii ndio sababu katika nchi nyingi kuna idadi kubwa ya wanasayansi, madaktari na wahandisi huku kukiwa na uhaba wa waandishi wa habari, wanasoshiolojia na wataalamu wa masuala ya siasa.

Katika wakati huu ambapo panatokea mabadiliko ya kihistoria, nchi za Kiarabu zinahitaji hasa wataalamu watakaoweza kujenga kwa upya taasisi muhimu katika jamii kama vile vyama vya siasa, vyombo vya habari pamoja na vyama vya wafanyakazi. Ili kuuondoa ulimwengu wa Kiarabu katika nafasi yake ya kuwa mnunuzi tu katika soko la dunia, ni muhimu pawepo na demokrasia na uwazi zaidi na pia wanafunzi wapewe nafasi ya kusikilizwa.

Sonja Hegasy, Vizedirektorin des Zentrums Moderner Orient in Berlin; Copyright: Oliver Möst
Sonja Hegasy wa kituo cha masuala ya Mashariki ya KatiPicha: Oliver Möst

Lakini meneja msaidizi wa kituo cha masuala ya Mashariki ya Kati kutoka Berlin, Bi Sonja Hegasy, anaeleza: "Tatizo kubwa ni kwamba suala la kuwapa wanafunzi nafasi kutoa maoni yao linazuiwa kwa nguvu zote na utawala wa zamani, licha ya kwamba sasa kuna mwamko katika ulimwengu wa Kiarabu." Mfano mmojawapo ni chuo kikuu cha kijerumani kilichopo Cairo, Misri. Chuo hicho kimetishia kuwawekea vizuizi wanafunzi watakaoamua kujiunga pamoja kwa ajili ya kutoa maoni yao.

Mwandishi: Loay Mudhoon
Tafsiri: Elizabeth Shoo
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman