1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ennahda hakina mizizi ya Taliban

26 Oktoba 2011

Mzozo wa madeni barani Ulaya na matokeo ya uchaguzi nchini Tunisia ni mada kuu zilizoshughulikiwa na wahariri wa magazeti ya Ujerumani, Jumatano ya hii leo.

https://p.dw.com/p/Rt3t
Abgeordnete sitzen am Freitag (21.10.11) im Bundestag in Berlin. Der Bundestag beriet am Freitag unter anderem ueber einen Antrag der Gruenen zur Euro-Stabilisierung. (zu dapd-Text) Foto: Axel Schmidt/dapd
Bunge la Ujerumani, BerlinPicha: dapd

Basi tukianza na mzozo wa madeni unaoendelea kugonga vichwa vya habari, gazeti la DER NEUE TAG linasema:

"Ionekanavyo, bunge la Ujerumani hii leo litapiga kura kuliunga mkono pendekezo la kuongeza fedha katika mfuko wa kuzisaidia nchi zilizokumbwa na madeni makubwa katika kanda inayotumia sarafu ya euro barani Ulaya. Kwa kufanya hivyo, Kansela Angela Merkel atakwenda kwenye mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya akiwa na mamlaka dhahiri. Baadhi ya nchi za Ulaya zina wasiwasi kuwa Umoja wa Ulaya unazidi kuzipokonya nchi wanachama mamlaka ya kitaifa. Lakini ukweli uliopo ni kwamba, bara la Ulaya halina chaguo jingine ikiwa linataka kuwa na usemi katika jukwaa la kisiasa ulimwenguni. Mkutano wa viongozi wa Umoja wa Ulaya utakaofanywa leo jioni huenda likawa tukio muhimu kabisa kwa bara la Ulaya."

Lakini gazeti la REUTLINGER GENERAL-ANZEIGER linasema, moja ni dhahiri kabisa: mkutano huo wala hautomaliza matatizo ya madeni. Linaongezea:

"Kinachofanywa hivi sasa ni kujipatia tu wakati wa kukabiliana na masoko ya fedha na athari za biashara za masoko hayo. Kwani majuma manne yaliyopita tu, bunge la Ujerumani lilipitisha uamuzi wake kuunga mkono mfuko huo wa msaada. Hilo tena, lisijekuwa jambo la mara kwa mara, ama sivyo nguvu za kidemokrasia zitapungua bungeni."

Sasa tunageukia mada nyingine iliyoshughulikiwa na wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo hii. Matokeo ya uchaguzi uliofanywa nchini Tunisia jumapili iliyopita. Gazeti la STUTTGARTER ZEITUNG linaeleza hivi:

"Wakati umebadilika. Mwanzoni mwa mwaka huu umma ulisimama kidete kujiamulia hatima yao. Umma huo unaostahili kuheshimiwa na kutambuliwa kwa kufanya hilo. Anaetambua kilichotekelezwa na wapiga kura na hata uchaguzi wenyewe, basi anapaswa pia kutambua nani aliepigiwa kura zaidi: chama cha kiislamu cha Ennahda. Bila shaka chama hicho kitakodolewa macho. Sasa chama hicho cha kiislamu kinawajibika kutekeleza ahadi zilizotolewa: yaani kuheshimu haki za binadamu na hasa haki za wanawake na pia kuhifadhi kile kilichokuwa kizuri katika kipindi kilichopita."

epa02979458 Supporters of Islamist Ennahda party attend a announcement by members of their party to media at the party's headquarters in Tunis, Tunisia, on 24 October 2011. Tunisia's moderate Islamist party Ennahda claimed victory in the country's historic first free elections, saying that unofficial results gave it the lion_s share of the vote. 'The first confirmed results show that Ennahda has obtained first place nationally and in most districts,' the party's campaign manager, Abelhamid Jelassi, told a press conference a day after the first democratic elections in the birthplace of the Arab Spring. EPA/STR +++(c) dpa - Bildfunk+++
Wanawake wa Tunisia hawatokubali kunyanganywa haki zaoPicha: picture-alliance/dpa

Gazeti la BADISCHE ZEITUNG likiandika kuhusu mada hiyo hiyo linasema:

"Chama cha Ennahda hakina mizizi ya Taliban, bali ni chama cha kiislamu kinachofuata siasa za wastani. Hata baada ya uchaguzi chama hicho hakijatoa matamshi ya kusababisha mtengano. Lakini ikumbukwe kuwa uwezo wao pia una mipaka, kwani wanawake wa Tunisia hawana uoga na wala hawatokubali kunyanganywa tena haki zao. Vile vile, nafasi za ajira zinazohitajiwa sana nchini Tunisia hutegemea uwekezaji wa kigeni na maingiliano na mataifa ya kigeni. Kwa hivyo, hata kikitaka, chama cha kiislamu hakina uwezo wa kuunda taifa jingine kama lile la Saudi Arabia."

Mwandishi:Martin,Prema

Mhariri: Othman Miraji