1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Enzi mpya katika uhusiano kati ya Urusi na Marekani

Oumilkher Hamidou25 Juni 2010

Rais Dimtri Medwedjew amekamilisha ziara yake nchini Marekani na kutiliana saini pamoja na rais Obama mkataba wa kununua ndege 50 chapa ya Boeing

https://p.dw.com/p/O2ql
Rais Barack Obama na kiongozi mwenzake Dmitry Medwedjew wakitembea katika bustani Lafayette mjini WashingtonPicha: AP

Baada ya kupiga hatua muhimu mbele katika siasa yao ya usalama, Marekani na Urusi zinataka hivi sasa kuimarisha ushirikiano wao katika sekta ya kiuchumi pia.Katika mkutano pamoja na kiongozi mwenzake wa Urusi, Dimitri Medwedjew, jana alkhamisi katika ikulu ya Marekani-White House,mjini Washington,rais Barack Obama ameahidi kupigania Urusi ijiunge na shirika la biashara la kimataifa, WTO.Na hata katika uhusiano wa kibinafsi, viongozi hao wawili wanaonyesha kupiga hatua muhimu mbele.

Hakuna kinachoweza kudhihirisha zaidi mageuzi katika uhusiano kati ya Marekani na Urusi kama matembezi ya muda mfupi yaliyofanywa na rais Barack Obama na kiongozi mwenzake wa Urusi Dimitri Medwedew.Badala ya kula chakula cha usiku ikulu ya Marekani ,wakati wa mkutano wao,walisitisha mazungumzo na kuongozana huku wakifuatwa na magari ya polisi hadi katika mkahawa mmoja katika kitongoji cha mji mkuu Washington. Mikono ya mashati wamepandisha kidogo na kuketi bila ya makoti wakila Hamburger. Medwedjew alisema baadae katika mkutano pamoja na waandishi wa habari na kutafsiriwa na mkalimani wake tunanukuu:"Ulikuwa mkahawa halisi wa kimarekani. Pengine kwa upande wa afya, chakula hakikuwa kizuri sana,lakini kilikua na ladha kweli kweli na mtu alikua anahisi hasa, hapa kweli niko Marekani."Mwisho wa kumnukuu rais wa urusi Dimtri Medwedew.

Nafasi ya mbele kabisa ya mada walizozungumzia haijashikiliwa na suala la makombora wala si kupunguza silaha au masuala ya usalama. Safari hii masuala ya uhusiano wa kiuchumi kati ya Marekani na Urusi ndio yaliyotangulizwa mbele. Rais Barack Obama alikua na furaha kutangaza makubaliano ya biashara ya ndege yenye thamani ya matrilioni ya Dala.

"Biashara ya ndege 50 chama ya Boeing, zenye thamani ya Dala trilioni 4, itasaidia kubuni nafasi 44 elfu za kazi"

Rais Barack Obama amesifu pia ile hali kwamba hata mvutano kuhusu nyama ya kuku inayopelekwa Urusi umemalizika-biashara hiyo pia inaipatia Marekani trilioni za Dola.

Barack Obama und Dimitri Medwedew
Viongozi wa madola mawili makuu ya dunia wanakwenda kula Hamburger katika mkahawa mmoja huko Arlington,karibu na WashingtonPicha: AP

Wakati huo huo, rais Obama ameahidi kupigania Urusi ikubaliwe kuwa mwanachama wa shirika la biashara la dunia-WTO-jambo analosema kua ni la maana kwa Urusi, Marekani na kwa uchumi wa dunia pia.

Suala la kuwekewa vikwazo Iran, mzozo wa Mashariki ya kati na hali nchini Korea ya kaskazini na Kirgistan, nayo pia wameyazungumzia-amesema rais Dimtri Medwedjew. Hakuna makubaliano yoyote, lakini yaliyofikiwa.

Rais Dimitri Medwedjew amekamilisha ziara yake nchini Marekani kwa kuhudhuhuria mkutano wa kiuchumi kati ya nchi yake na Marekani mjini Washington.

Ameshaondoka Washington kuelekea Toronto ambako pia anapanga kukutana tena na rais Barack Obama-itakua mara yao ya nane kukutana tangu Barack Obama alipokabidhiwa hatamu za uongozi nchini Marekani.

Mwandishi: Paulert,Rüdiger/Washington ARD/ Hamidou Oummilkheir

Imepitiwa na: Miraji Othman