1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Enzi ya ushirikiano mpya kati ya Bara la Afrika na Amerika ya Kusini

28 Septemba 2009

Viongozi wa zaidi ya nchi 60 kutoka Bara la Afrika na Amerika ya Kusini katika mkutano wao nchini Venezuela wamekubaliana kuanzisha mfumo mpya wa fedha. Lengo ni kujiimarisha kimataifa na kuendeleza uchumi wao.

https://p.dw.com/p/JqeR
Venezuela's President Hugo Chavez gestures during a news conference with foreign media members at Miraflores presidential palace in Caracas, Monday, Nov. 24, 2008. Chavez's allies won a majority in Venezuela's Sunday local elections, but the opposition made important gains, capturing the Caracas mayor's office and two of the most populous states. (AP Photo/Fernando Llano
Rais wa Venezuela,Hugo Chavez.Picha: AP

Mkutano wa pili wa viongozi kutoka nchi za Bara la Afrika na Amerika ya Kusini uliomalizika siku ya Jumapili, umesisitiza kuanzisha muungano utakaozipa nchi hizo, usemi zaidi katika mashirika ya kimataifa kama vile Shirika la Fedha la Kimataifa IMF pamoja na kuimarisha ushirikiano kati ya nchi za kanda hizo mbili katika sekta za uchumi, nishati, mazingira, teknolojia na afya.

Rais wa Venezuela Hugo Chavez alieongoza mkutano huo amesema kuwa kumefunguliwa ukurasa mpya katika historia ya Amerika ya Kusini na Bara la Afrika. Ushirikiano na umoja ndio iwe misingi ya uhusiano wao wa kiuchumi. Miongoni mwa mikataba iliyotiwa saini na nchi saba za Amerika ya Kusini ni makubaliano ya kuanzishwa benki ya kanda hiyo ya kusini "Bank of the South." Benki hiyo itaanzishwa kwa mtaji wa dola bilioni 20 na itasimamia gharama za miradi ya pamoja ya kiuchumi katika nchi za Amerika ya Kusini na Bara la Afrika.

Mageuzi katika mashrika ya kimataifa ni mada iliyojadiliwa kwa urefu katika mkutano huo. Kiongozi wa Libya Muammar Gaddafi ametoa mwito wa kuanzishwa shirika la kujihami la kanda ya kusini kama mfano wa NATO ifikapo mwaka 2011. Nae Rais wa Brazil Luiz Lula da Silva anaeazimia kuifanya nchi yake ngome ya viwanda, amesema kuwa karne ya 21 huenda ikawa karne ya Bara la Afrika na Amerika ya Kusini. Amezihimiza nchi za kanda hizo kuwa na msimamo mmoja katika majadiliano ya biashara duniani maarufu kama "Doha Development Round." Kuruhusiw nchi za Kiafrika katika masoko ya kilimo ya Ulaya ndio iwe sehemu ya makubaliano ya majadiliano hayo yaliyokwama. Lengo ni kuwaondoa mamilioni ya watu kutoka maisha ya umasikini na kuimarisha uchumi kote duniani.

Rais Chavez ambae nchi yake ni muuzaji mkubwa kabisa wa mafuta katika Amerika ya Kusini amependekeza kuanzishwa kampuni kubwa ya kimataifa itakayozipatia mafuta nchi za kanda hizo mbili. Kiongozi huyo mwenye sera kali za mrengo wa kushoto na alieitumia fursa ya mkutano huo kukosoa ushawishi wa Marekani na Ulaya katika nchi zinazoendelea, amethibitisha kuwa anaunga mkono mpango wa kujenga kiwanda cha kusafishia mafuta nchini Mauritania. Vile vile amependekeza kujenga kiwanda kingine nchini Equitorial Guinea ili mafuta yaweze kuuzwa kwa bei iliyo nafuu.

Ushirikiano katika sekta ya nishati kati ya kanda hizo mbili, eneo linalozalisha asilimia 24 ya mafuta duniani ilikuwa mada kuu katika mkutano huo wa kilele. Venezeuela imetia saini mikataba minane pamoja na nchi za Kiafrika kushirikiana katika sekta ya nishati. Miongoni mwa nchi hizo ni Afrika Kusini,Sudan na Cape Verde. Mkutano wa tatu wa nchi za Bara la Afrika na Amerika ya Kusini utafanyika nchini Libya.

Mwandishi: P.Martin/AFPE

Mhariri: Othman,Miraji