1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Enzi za Compaoré zakaribia kikomo Burkina Faso

31 Oktoba 2014

Rais Blaise Compaoré wa Burkina Fasso ameahidi kipindi cha mpito lakini anakataa kujiuzulu katika wakati ambapo jeshi limeshatwaa madaraka mnamo mkesha wa machafuko makubwa dhidi ya utawala wake.

https://p.dw.com/p/1DeuQ
Waandamanaji mjini OugadougouPicha: Reuters/Joe Penney

Mamia ya waandamanaji wameteremka majiani asubuhi hii mjini Ougadougou,mji mkuu wa Burkina Faso wakimtaka rais Blaise Compaore ajiuzulu,siku moja tu baada ya jeshi kulivunja bunge na kutangaza serikali ya mpito. "Hatumtaki,tunataka ang'oke madarakani. Yeye si rais wetu" amesema Ouedraogo Yakubo,ambae ni miongoni mwa waandamanaji waliokusanyika katika uwanja mashuhuri wa Place de la Nation-au uwanja wa taifa karibu na makao makuu ya jeshi.

Blaise Compaore,aliyeingia madarakani tangu mwaka 1987 aliivunja serikali hapo awali akisema yuko tayari kujadiliana kipindi cha mpito hadi mhula wake utakapomalizika mwaka 2015. Marekani imesifu utayarifu wa rais Compaore wa kujadiliana - taarifa ya wizara ya mambo ya nchi za nje imesema mjini Washington.

Rais Compaoré alazimika kung'atuka

Hali inatatanisha nchini humo,wakuu wa upande wa upinzani hawajatamka chochote hadi sasa kufuatia uamuzi wa jeshi kutwaa madaraka-uamuzi unaomaanisha Compaore hana njia nyengine isipokuwa kung'atuka.

Blaise Compaore Präsident von Burkina Faso Archiv Juli 2014
Rais Blaise Compaoré (picha ya Julai 2014)Picha: AFP/Getty Images/Sia Kambou

"Hali inatatanisha moja kwa moja" amesema mbunge wa upande wa upinzani Ablassé Compaoré katika mahojiano na kituo cha Radio cha RFI

Machafuko yameangamiza maisha ya watu wasiopungua 30 na zaidi ya 100 kujeruhiwa-unasema upande wa upinzani bila ya kutaja kama ni katika daraja ya taifa au katika mji mkuu Ouagadougou tu.

Milio ya risasi ilihanikiza usiku wa alkhamisi kuamkia ijumaa karibu na kasri la rais. Jengo la bunge limetiwa moto,kituo cha televisheni kimevamiwa,machafuko yameripotiwa mikoani na miito kumtaka rais ajiuzulu imehanikiza- hiyo ndiyo sababu jeshi limeingilia kati. Mkuu wa vikosi vya wanajeshi Nabéré Honoré Traoré amesema katika taarifa iliyosomwa na afisa mmoja wa jeshi wanaunda taasisi ya mpito itakayosimamia madaraka ya rais na bunge lengo likiwa kurejesha nidhamu na kuheshimu katiba.

Miito ya subira inazidi kutolewa

Mpatanishi wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Burkina faso,Ibn Chambas akizungumza na DW amesema:" Panahitajika chaguzi huru na za uwazi barani Afrika. Mwakani chaguzi muhimu zitafanyika nchini Nigeria,Togo,Guinee,Côte d'Ivoire na bila ya shaka Burkina Faso.Tunataraji tutaendelea kujiandaa kwaajili ya uchaguzi wa uwazi,huru na wa kuaminika pia nchini Burkina Faso."

Burkina Faso Ouagadougou Symbolbild Grafik Flagge Fahne Karte
Bendera na ramani ya Burkina Faso nchi ya Afrika magharibi inayopakana na Ghana,Côte d'Ivoire,Mali na NigerPicha: picture-alliance/ANP

Umoja wa Afrika umezitolea wito pande zote zinazohusika zijizuwie huku Umoja wa ulaya ukihimiza mazungumzo yaendelezwe.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP/Reuters

Mhariri:Josephat Charo