1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Erdogan atishia kuvishambulia vikosi vya Syria

Grace Kabogo
12 Februari 2020

Waasi nchini Syria wameidungua helikopta ya jeshi la Syria kaskazini mwa nchi hiyo na kuwaua watu wote waliokuwemo ndani, huku serikali ikiendeleza mashambulizi kwenye mko wa Idlib ambao unaodhibitiwa na waasi.

https://p.dw.com/p/3XeMu
Syrien | Von der Türkei unterstützte syrische Kämpfer
Picha: Getty Images/AFP/A. Watad

Taarifa za wanaharakati pamoja na vyombo vya habari zimeeleza kuwa majeshi ya serikali pia yamewaua raia saba katika shambulizi la anga lililofanyika jana katika jimbo la Idlib. Shirika la habari la Uturuki, Anadolu, limeripoti kuwa rubani na watu wengine wawili waliokuwemo ndani ya helikopta hiyo wameuawa, huku wanaharakati wa upinzani wakisema kuwa ni wafanyakazi wawili tu ndiyo walikuwemo ndani ya helikopta.

Raia wauawa

Kwa mujibu wa idara ya uokozi ya White Helmets, saa chache baadae shambulizi la anga la Syria lilipiga katika mji wa Idlib na kuwaua watu saba na kuwajeruhi wengine kadhaa. Aidha, shirika la kutetea haki za binaadamu nchini Syria limesema kuwa shambulizi hilo limewaua raia 12, nusu kati ya hao wakiwa watoto, huku wengine 30 wakiwa wamejeruhiwa.

Wakati hayo yakijiri, Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan ametishia kuvishambulia vikosi vya Syria sehemu yoyote ile bila kuzingatia makubaliano ya amani, iwapo wajeshi wake watadhuriwa kwa namna yoyote ile. Erdogan ameyatoa matamshi hayo leo katika mkutano wa chama tawala bungeni na ameishutumu Urusi ambayo ni mshirika wa Syria kwa kufanya mauaji katika jimbo la Idlib.

Türkei Präsident Erdogan
Rais wa Uturuki, Recep Tayyip ErdoganPicha: picture-alliance/AA/M. Kamaci

''Serikali ya Syria pamoja na vikosi vya Urusi na wanamgambo wanaoungwa mkono na Iran wanaoendesha shughuli zao katika jimbo la Idlib, wanawashambulia na kuwaua raia pamoja na kusababisha umwagikaji mkubwa wa damu,'' alifafanua Erdogan.

Erdogan ametoa onyo hilo baada ya wanajeshi kadhaa wa Uturuki kuuawa na vikosi vya serikali ya Syria kaskazini magharibi mwa jimbo la Idlib.

Putin na Erdogan wazungumza

Wakati huo huo, ikulu ya Urusi imesema rais wa nchi hiyo Vladmir Putin na Rais Erdogan leo wamejadiliana hatua za kuchukua kupunguza mzozo wa Syria. Viongozi hao wamezungumza kwa njia ya simu na kufafanua kuwa makubaliano kati ya Urusi na Uturuki yanapaswa kutekelezwa kikamilifu. Urusi itapeleka ujumbe wake nchini Uturuki kujadiliana kuhusu hali ya Idlib.

Mapambano kwenye jimbo hilo yanapamba moto wakati ambapo majeshi ya serikali yanakaribia kuichukua barabara kuu inayodhibitiwa na waasi ambayo inaliunganisha eneo la kusini na kaskazini mwa Syria na iwapo vikosi vya serikali vitafanikiwa, barabara hiyo itarejea mikononi mwa Rais Bashar Al-Assad kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2012.

Huku vikisaidiwa na Urusi na Iran, vikosi vya Syria vimekuwa katika mashambulizi ya wiki kadhaa huko Idlib na kwenye maeneo ya karibu na jimbo la Aleppo hali inayosababisha mzozo wa kibinaadamu ambapo watu 700,000 wamelazimika kuyakimbia makaazi yao na kuelekea eneo la kaskazini karibu na mpaka wa Uturuki.

(AP, AFP, DPA, Reuters)