1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Erdogan awashupalia wakosoaji

8 Juni 2013

Waziri Mkuu wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amesema Umoja wa Ulaya ni kigeugeu, baada ya umoja huo kuikosoa serikali yake kwa kutumia nguvu kubwa ya polisi dhidi ya waandamanaji.

https://p.dw.com/p/18m50
Waziri Mkuu wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan na kamishna wa Umoija wa Ulaya, Stefen Füle
Waziri Mkuu wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan na kamishna wa Umoija wa Ulaya, Stefen FülePicha: Reuters

Kauli ya Erdogan imefuatia wito wa kamishna wa Umoja wa Ulaya anayehusika na kupanuka kwa umoja huo Stefan Füle, (aliye na Erdogan juu pichani) wa kuwepo kwa uchunguzi wa wazi na wa haraka juu ya namna polisi ya Uturuki ilivyotumia nguvu kupindukia katika kupambana na waandamanaji wanaoipinga serikali.

Füle amesema maandamano ya amani ni njia halali ya watu kueleza maoni yao, na kuongeza kuwa matumizi ya nguvu za ziada kuwakandamiza waandamanaji hayana nafasi katika nchi ya kidemokrasia kama Uturuki, ambayo inaazimia kujiunga na Umoja wa Ulaya. Alikuwa akizungumza katika mkutano mjini Istanbul, ambao ulihudhuriwa na waziri mkuu wa Uturuki Recep Erdogan.

Erdogan ajibu mapigo

Erdogan hakutafuna maneno katika kujibu ukosoaji huo kwa serikali yake. ''Katika nchi yoyote ya Ulaya, yatokeapo maandamano ya fujo dhidi ya mpango wa kulibomoa jengo, wahusika hukabiliana na hatua kali zaidi'', alisema. Erdogan aliyalinganisha maandamano yanayoikabili serikali yake na vuguvugu lililojulikana kama ''Occupy Wall Stree'' lililotokea nchini Marekani mwaka 2011 na kuenea katika miji kadhaa ya Ulaya. Ubalozi wa Marekani nchini Uturuki umejibu kupitia mtandao wa Twitter, ukisema hakuna mtu aliyeuawa na polisi katika vuguvugu hilo.

Waziri Mkuu wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan
Waziri Mkuu wa Uturuki Recep Tayyip ErdoganPicha: Reuters

Jana, Kansela wa Ujerumani Angela Merkel alijiunga na wakosoaji wa matumizi makubwa ya nguvu ya polisi nchini Uturuki, akisema anaamini tatizo lililopo litashughulikiwa kwa kufanya mazungumzo na vijana.

Dalili ya maridhiano

Maandamano hayo ambayo yanaingia siku ya 8 mfululizo, yalianza pale polisi walipokabiliana vikali na waandamanaji wachache, walioanzisha kampeni ya kupinga ujenzi wa jumba la biashara katika bustani ya Gezi mjini Istanbul. Maandamano hayo sasa yamegeuka na kuwa ya kumpinga waziri mkuu Recep Tayyip Erdogan na chama chake cha kiislamu, AKP. Waandamanaji wanasema utawala wa waziri mkuu huyo unazidi kuwa wa kiimla.

Maandamano dhidi ya serikali ya Erdogan yameendelea kwa siku ya 8 mfululizo
Maandamano dhidi ya serikali ya Erdogan yameendelea kwa siku ya 8 mfululizoPicha: Reuters

Kinyume na ukaidi alioonyesha Erdogan siku za nyuma, jana Ijumaa alilegeza msimamo wake, na kusema yuko tayari kusikiliza mapendekezo yoyoyte yatakayotolewa kwa njia ya kidemokrasia. Kabla ya hapo alikuwa ameyataka maandamano kusimamishwa mara moja, akiwaita waandamanaji watu wenye misimamo mikali, na waporaji.

Wito wake umepuuzwa na waandamanaji hao, na kwa usiku wa nane mfululizo wamekesha katika uwanja wa Taksim mjini Istanbul, wakipiga ngoma na zumari. Maandamano mengine yameendelea katika mji mkuu wa Uturuki Ankara. Hakuna visa vya makabiliano vilivyoripotiwa.

Mwandishi: Daniel Gakuba/AFPE

Mhariri: Sekione Kitojo