1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Erdogan kukutana na Macron Ufaransa

John Juma
5 Januari 2018

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan anazuru Ufaransa leo Ijumaa (05.01.2018) kufanya mazungumzo na mwenyeji wake Rais Emmanuel Macron. Mazungumzo hayo yanalenga kuimarisha uhusiano kati ya Uturuki na Ulaya.

https://p.dw.com/p/2qNyb
Frankreich Türkei Präsidenten Emmanuel Macron und Recep Tayyip Erdogan
Picha: picture-alliance/Abacca/S. Lefevre

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan anazuru Ufaransa leo Ijumaa kufanya mazungumzo na mwenyeji wake Rais Emmanuel Macron. Mazungumzo hayo yanalenga kuimarisha uhusiano kati ya Uturuki na Ulaya, baada ya vita vya maneno katika mwaka 2017. Kando na hilo, waziri wa mambo ya nje wa Uturuki Mevlut Cavusoglu ametaka mwanzo mpya wa mahusiano kati ya nchi yake na Ujerumani, kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na nishati.

Ziara ya Recep Tayyip Erdogan nchini Ufaransa itakuwa ya kwanza tangu jaribio la mapinduzi dhidi yake mnamo Julai 2016. Aidha ni moja kati ya ziara chache ambazo amefanya barani Ulaya tangu jaribio hilo la kijeshi.

Ajenda kuu: Uhusiano wa Uturuki na Ulaya

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan
Rais wa Uturuki Recep Tayyip ErdoganPicha: picture-alliance/dpa/AP/H. Dridi

Mazungumzo kati ya Erdogan na Emmanuel Macron ambapo pia watakula mlo wa mchana pamoja katika ikulu ya Elysee, yatagusia suala la Syria na uhusiano kati ya Uturuki na Umoja wa Ulaya. Lakini Macron anatarajiwa kuelezea pia wasiwasi wake kuhusu hatua za Erdogan baada ya mapinduzi yaliyoshindwa.

Katika mahojiano na kituo cha televisheni cha Ufaransa LCI siku ya Alhamisi, Erdogan alisema amekuwa na mwanzo mwema na rais mpya wa Ufaransa. Akizungumza na waandishi w ahabari kuhusu ziara hiyo Erdogan amesema:

"Ninaipa ziara hii umuhimu mkubwa kwani tutazungumzia masuala mengi. Katika ziara hii tutagusia mada kuanzia uhusiano kati ya nchi mbili hadi masuala ya kanda nzima. Na bila shaka tutaendelea na mashauriano siku za baadaye. Ninaamini ziara hii ni muhimu zaidi kuhusu ushirikiano kati ya Uturuki na Ufaransa na pia kwa amani ya kanda na dunia nzima".

Ziara ya Erdogan Ufaransa yakosolewa

Hatua ya kumkaribisha Erdogan imekosolewa vikali na wafuasi wa siasa za mrengo wa kushoto nchini Ufaransa, kufuatia hatua yake ya kuwakamata maelfu kwa maelfu ya maafisa, wasomi, waandishi wa habari na wanaharakati nchini mwake.

Meya wa Paris ambaye ni msoshialisti Anne Hidalgo amesema ana wasiwasi kuhusiana na hali ya haki za kibinadamu na demokrasia ya ndani nchini Uturuki.

Maafisa wa polisi wakikabiliana na waandamanaji mjini Ankara Uturuki
Maafisa wa polisi wakikabiliana na waandamanaji mjini Ankara UturukiPicha: Reuters/U. Bektas

Hata hivyo ikulu ya Ufaransa imekuwa ikisisitiza haja ya kuyaendeleza mazungumzo na Uturuki bila ya kuficha mitizamo yao tofauti. Macron ameitaja Uturuki kuw amshirika muhimu katika kuikabili mizozo ikiwemo ya Syria.

Macron amesema katika mazungumzo hayo, pia atayaangazia masaibu ya waandishi wa habari wa Uturuki ambao wamefungwa.

Amnesty International: Erdogan aambiwe watetezi wa haki za kibinadamu si magaidi

Shirika la Amnesti International ambalo mkuu wake nchini Uturuki Taner Kilic alifungwa, limesema Macron anapaswa kuwa imara kumueleza Erdogan kuwa watetezi wa haki za kibinadamu si magaidi.

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amekuwa akikosoa hatua ya kamatakamata inayofanywa na utawala wa Erdogan.

Katika tukio tofauti, waziri wa mambo ya nje wa Uturuki Mevlut Cavosoglu ametaka kuwe na mwanzo mpya wa uhusiano kati ya Uturuki na Ujerumani, kwa nia ya kuimarisha ushirikiano wao kiuchumi haswa katika sekta ya uchukuzi na nishati ikiwa uhusiano wao utaimarika. Nchi hizo zimekuwa na uhusiano mbaya.

     

Mwandishi: John Juma/AFPE/RTRE

Mhariri: Gakuba, Daniel