1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Erdogan, Putin wazidisha ushirikiano kwa Syria

Mohammed Khelef
10 Machi 2017

Rais Tayyip Erdogan wa Uturuki yuko ziarani nchini Urusi kuzungumzia masuala ya Syria, huku Umoja wa Mataifa ukivilaumu vikosi vyake kwa mauaji ya zaidi ya Wakurdi 2,000 kusini mashariki mwa nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/2YyHK
Russland Wladimir Putin und Recep Tayyip Erdogan in Moskau
Picha: picture-alliance/abaca/S. Karacan

Rais Vladimir Putin wa Urusi alimpokea mgeni wake mchana wa leo katika ikulu ya Kremlin, akisema kwamba ushirikiano wa pande hizo mbili katika kuumaliza mzozo wa Syria una mafanikio makubwa.

"Tumefurahi sana kwamba mafungamano baina ya nchi zetu mbili yanarejeshwa tena kwa haraka. Katika siku za hivi karibuni tumekuwa tukiyapandisha mahusiano haya katika kiwango ambacho kinastahiki. Tunalifanyia kazi suala la kutatuwa migogoro mikubwa sana, na wa kwanza ni wa Syria," alisema Putin.

Kwa pamoja, Uturuki na Urusi ziliwezesha kufikiwa kwa makubaliano ya kusitisha mapigano nchini Syria mnamo mwezi Disemba, ambayo yalisaidia kupunguza kiwango cha mapigano kati ya majeshi ya Rais Bashar Assad na upinzani, na kisha wakawezesha kufanyika kwa duru mbili za mazungumzo kati ya upande wa Assad na maadui zake. Duru ya tatu inatazamiwa wiki ijayo.

Uturuki na Urusi pia ziliunganisha operesheni zao dhidi ya kundi lijiitalo Dola la Kiislamu nchini Syria, na licha ya mashambulizi ya ndege za Urusi kuwauwa wanajeshi watatu wa Uturuki mwezi uliopita kwa bahati mbaya, uhusiano wa pande hizo mbili haukutetereka.

Hata hivyo, ukiacha ushirikiano wao dhidi ya IS, nchi hizi zinaunga mkono pande tafauti kwenye vita hivi, ambapo Urusi inamsaidia Assad kuwashinda waasi, Uturuki inawasaidia waasi kumshinda Assad. 

Uturuki yashutumiwa kwa mauaji ya Wakurdi

USA | United Nations High Commissioner for Human Rights Zeid Ra'ad al Hussein
Mkuu wa Kamisheni ya Haki za Binaadamu ya Umoja wa Mataifa, Zeid Ra'ad al-Hussein anasema Uturuki imewauwa zaidi ya watu 2,000 wengi wao wakiwa Wakurdi.Picha: imago/Xinhua

Mkutano huu wa Putin na Erdogan unafanyika katika siku ambayo Kamisheni ya Haki za Binaadamu ya Umoja wa Mataifa imetoa ripoti inayolikosoa jeshi la Uturuki kwa mauaji ya watu wapatao 2,000 kusini mashariki mwa nchi hiyo, ambako yanapambana na wapiganaji wa Kikurdi.

Msemaji wa mkuu wa kamisheni hiyo, Rupert Colville, anasema picha za satalaiti zinathibitisha kiwango kikubwa cha mateso na ukandamizaji uliofanywa na jeshi la Uturuki, na kwamba hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa dhidi ya waliotenda hayo.

"Picha za satalaiti za kabla na baada ya matukio hayo, ambazo zinajumuisha ripoti kutoka miji ya Nusaybin na Sur na viunga vyao, zinaonesha mitaa ikiwa imeteketezwa kabisa. Tunatiwa hofu zaidi na matokeo ya uchambuzi wa picha hizi, ambayo yanaashiria kuwepo kwa kiwango kikubwa kabisa cha uharibifu wa majengo kwa kutumia silaha nzito nzito," alisema Colville.

Mkuu wa Kamisheni hiyo, Zeid Ra'ad al Hussein, anasema kuwa katika kipindi cha kati ya Julai 2015 hadi Disemba 2016, operesheni za kijeshi za Uturuki zilihusika na uharibifu mkubwa wa makaazi ya watu na uvunjaji wa haki za binaadamu, ambapo Wakurdi 500,000 wamelazimishwa kuyakimbia makaazi yao. 

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/AP
Mhariri: Iddi Ssessanga