1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Eritrea yakosolewa kwa Ukiukaji wa haki za binadamu

16 Machi 2015

Jopo la Umoja wa Mataifa la uchunguzi kuhusu ukiukaji wa haki za binadamu limebainisha kuwepo Eritrea kwa mifumo ya wazi ya ukiukaji wa haki za binadamu pamoja na ukosefu wa utawala wa sheria.

https://p.dw.com/p/1EreW
Rais wa Eritrea Issaias Afewerki,
Rais wa Eritrea Issaias Afewerki,Picha: picture-alliance /dpa

Jopo hilo limetoa ripoti leo (16.03.2015) inayoonyesha hali mbaya ya haki za binadamu nchini humo.

Rekodi mbaya ya haki za binadamu ndiyo chanzo kikubwa kinachotajwa kuwashinikiza watu wengi kuihama nchi hiyo ya upembe wa Afrika.Eritrea ni nchi ya pili katika nchi zinazosababisha wimbi kubwa la wakimbizi baada ya Syria wanaosafiri kila siku kupitia bahari ya mediterania kuelekea Ulaya.

Mwenyekiti wa jopo hilo la Uchunguzi la Umoja wa Mataifa Mike Smith ameliambia baraza la haki za binadamu la Umoja huo kwamba wengi wa raia wa Eritrea wamepoteza matumaini ya maisha ya baadae na ndio sababu wengi wanataka kuitoroka nchi hiyo.Aidha amesema mbele ya baraza hilo akiwasilisha ripoti hiyo juu ya hali ilivyo kwamba watu kukamatwa na kutiwa jela ni jambo la kawaida linalowakumba wengi wake kwa waume wakubwa kwa wadogo ikiwemo hata watoto.

Mkimbizi wa Kieritrea aliyepitia mateso chini ya mikono ya wasafirishaji watu
Mkimbizi wa Kieritrea aliyepitia mateso chini ya mikono ya wasafirishaji watuPicha: 2013 Tom Dale for Human Rights Watch

Lakini ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa inapingwa na balozi wa Eritrea katika Umoja huo Tefamicaeal Gerahtu ambaye ameliambia baraza la haki za binadamu kwamba ripoti hiyo imeandikwa chini ya misngi ya kutokuwepo ushahidi,na haiwezi kuaaminika.Mwenyekiti wa Jopo lililoandaa ripoti hiyo Smith anasema Eritrea iliyojitangazia uhuru wake kutoka Ethiopia mwaka 1993 ilikuwa inatumia mvutano wake wa muda mrefu na majirani zake kusini kama silaha au sababu ya kupuuza sheria ya haki za binadamu na kubakia katika mtindo wa kiimla ulioandamana na utawala wa kijeshi na ukandamizaji wa kikatili.

Akitoa mfano mwenyekiti huyo ameeleza kwamba imefikia mahala ambapo inaundwa mitandao ya kijaasusi ambayo inapenya ndani zaidi katika maisha ya kawaida ya watu ambapo kwamba mtu huyo aliyepewa kazi hiyo na usalama wa taifa anaweza kushindwa hata kufahamu kwamba na mwanawe vile vile anafanya kazi kama hiyo.

Matokeo ya hali hiyo mauaji ya kinyama,kutoweka kwa watu pamoja na visa vya watu kutiwa ndani vimekuwa vikifanyika kwa lengo la kuwazima wakosoaji wote pamoja na kuwapa funzo pamoja na wengine,na hasa kwakuwa mtu anapofanyika ukatili huo haelezwi ni kwasababu gani anajikuta katikaa hali hiyo,na ni kwa muda gani unashikiliwa na wapi.

Wakimbizi wakieritrea nchini Yemen
Wakimbizi wakieritrea nchini YemenPicha: picture-alliance/dpa

Shirika la Umoja huo wa Mataifa linalowahudumia wakimbizi UNHCR linasema kwamba kufikia Julai mwaka 2014 kiasi waeritrea 357,000 walikuwa wameikimbia nchi hiyo kiwango ambacho ni sawa na takrina asilimia 7 ya idadi jumla ya wakaazi wanaokadiriwa kuwa milioni 5.Na shirika hilo linasema idadi ya wanaohatariha maisha yao katika safari ya kukimbilia Ulaya kutoka nchi hiyo imeongezeka tangu wakati huo.

Kwa mujibu wa Smith katika muda wa miezi minne ya mwanzo ya jukumu lao jopo lake liliwahoji kiasi watu 400 katika nchi tano na kupokea maelezo ya watu 140.Na ni kutokana na ushahidi uliotolewa na watu hao Smith anasema ni bayana upo utaratibu wa wazi wa ukiukaji wa haki za binadamu katika nchi hiyo ya Upembe wa Afrika.

Mwandishi :Saumu Mwasimba

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman.