1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Erwin Huber ajiuzulu

Hamidou, Oumilkher30 Septemba 2008

Chama cha CSU chatafuta viongozi wepya baada ya zilzala ya jumapili

https://p.dw.com/p/FRZF
Mwenyekiti aliyejiuzulu Erwin Huber mbele ya makao makuu ya chama cha CSU mjini MünchenPicha: AP



Mwenyekiti wa chama cha Christian Social Union -CSU,Erwin Huber amejiuzulu hii leo kutokana na kushindwa vibaya chama hicho katika chaguzi za bunge katika jimbo la Bavaria jumapili iliyopita.Nafasi yake huenda ikashikiliwa na waziri wa kilimo Horst Seehofer.


Baada ya kikao cha dharura cha viongozi wa ngazi ya juu wa chama cha CSU,kilichoendelea usiku kucha mjini München,mwenyekiti wa chama cha CSU Erwin Huber amesema atakabidhi wadhifa wake huo mkutano mkuu wa chama utakapoitishwa October 25 ijayo.Hadi wakati huo lakini anasema ataendelea na shughuli zake kikamilifu.Anakipatia fursa chama cha CSU ya kua na uongozi mpya .Msemaji wa chama hicho amesema pia hata katibu mkuu Christine Haderthauer atajiuzulu mara tuu baada ya mwenyekiti mpya kuchaguliwa.Hadi wakati huo na yeye pia ataendelea na wadhifa wake.



Kwa mujibu wa waziri wa uchumi wa serikali kuu ya Ujerumani,Michael Glos aliyeshiriki katika kikao hicho cha dharura sawa na waziri mkuu wa zamani wa jimbo la Bavaria Edmund Stoiber,waziri wa serikali kuu anaeshughulikia kilimo na masuala ya wanunuzi Horst Seehofer ndie atakaekabidhiwa wadhifa wa mwenyekiti wa chama cha CSU.


Kabla ya hapo,waziri mkuu wa zamani wa jimbo la Bavaria Edmund Stoiber alisema:


"Chama cha CSU hakina tena haiba iliyokua nayo kwa miongo kadhaa iliyopita."


Mwenyekiti anaeacha wadhifa wake Erwin Huber amesisitiza mjini München,"katika kipindi cha miezi 13 ya madaraka yake lengo lake lilikua kuleta utulivu na kukiimarisha chama cha CSU."Chama kimejipatia viongozi kadhaa vijana na wanawake pia wamekabidhiwa nafasi muhimu chamani" amesema Erwin Huber aliyezungumzia pia kuhusu mpango wa malipo ya kodi uliopewa jina "pesa nyingi kwa wote.Amesisitiza kwamba mpango huo umelenga kuipa msukumo wa kudumu sera ya kijamii ya chama cha Christian Social Union .


 Mwenyekiti huyo wa CSU anaeacha madaraka yake Erwin Huber amesema ataendeklea kuwajibika kisiasa na atalitumikia kwa hali na mali jimbo la Bavaria na chama chake cha CSU.


  Licha ya zilzala iliyopiga Bavaria kufuatia uchaguzi wa jumapili iliyopita,waziri mkuu wa jimbo hilo,Günther Beckstein ataendelea angalao kwa sasa na wadhifa wake.


Chama cha CSU kimeshindwa vibaya sana katika uchaguzi wa jumapili iliyopita,kikiondoka na asili mia 43 tuu ya kura  na kupoteza wingi mkubwa wa viti bungeni,kwa mara ya kwanza tangu miaka 46 iliyopita.


Zilzala hiyo inaweza pia kukitikisa chama ndugu cha CDU cha kansela Angela Merkel uchaguzi mkuu utakapoitishwa mwakani.