1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ESSEN : Wito kufufuwa mazungumzo ya biashara duniani

11 Februari 2007
https://p.dw.com/p/CCTN

Mawaziri wa fedha na wakuu wa Benki Kuu wa nchi wanachama wa Kundi la Mataifa Saba yenye Maendeleo Makubwa ya Viwanda Duniani wametowa wito wa kufufuliwa kwa mazungumzo ya biashara duniani yaliokwama.

Mwishoni mwa mkutano wao wa siku mbili katika mji wa magharibi mwa Ujerumani wa Essen kundi hilo limetowa taarifa ambapo kwayo wamehimiza uregezaji zaidi wa masharti ya biashara na kupunguza hatua za kulinda masoko.Kile kinachojulikana kama Duru ya Doha mazungumzo ya biashara duniani yalizinduliwa hapo mwaka 1991 kwa lengo la kuondokana na vikwazo vya biashara lakini jitihada hizo zimetibuliwa na mizozo juu ya ruzuku za kilimo na ushuru.

Waziri wa Fedha wa Ujerumani Peer Steinbrück awali alionya kwamba kusambaratika kwa hazina kuu yoyote ile ya fedha iliotengwa kwa dharura kunaweza kukasababisha taathira kubwa kwa sekta ya fedha duniani.

Serikali ya Ujerumani imekuwa ikitetea kwa muda mrefu kuzidi kuratibiwa kwa fedha hizo.