1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JangaEthiopia

Ethiopia yakanusha Tigray kunyemelewa na baa la njaa

30 Desemba 2023

Serikali ya Ethiopia imekanusha tahadhari iliyotolewa na viongozi wa Tigray kwamba jimbo hilo lililoharibiwa kwa vita limo ukingoni kutumbukia kwenye baa kubwa la njaa.

https://p.dw.com/p/4ajGt
Ethiopia | Tigray | Baa la Njaa
Mkaazi wa Tigray akipekua masalia ya nafaka katikati kwa kitisho cha ukosefu wa chakula kwenye jimbo hilo la kaskazini mwa Ethiopia.Picha: Million Haileselassie Brhane/DW

Siku ya Ijumaa, rais wa mpito wa jimbo la kaskazini mwa Ethiopia Getachew Reda, alisema asilimia 91 ya wakaazi wake wamo kwenye "kitisho cha kukosa chakula na kupoteza maisha".

Aliifananisha hali ilivyo na ile iliyolikumba eneo la kaskazini mwa Ethiopia mnamo miaka ya 1980 ambapo karibu watu milioni moja walikufa kwa kukosa chakula.

Hata hivyo serikali mjini Addis Ababa imekanusha madai hayo huku ikikiri kwamba watu milioni kadhaa kaskazini mwa Ethiopia wameathiriwa na ukame wa muda mrefu pamoja na marufiko yaliyoshuhudiwa hivi karibuni.

"Taarifa kwamba janga linaloikumba hivi sasa jimbo la Tigray linaelekea kuwa baa kubwa la njaa na ukame unaofanana na ule wa mwaka 1984-85 ni uongo mtupu," amesema Legesse Tulu, msemaji wa serikali ya Ethiopia.

Licha ya kukanusha, amesema maeneo kadhaa ya Tigray na majimbo jirani ya Amhara na Afar, takribani watu milioni 3.8 "wanashuhudia kitisho cha ukame".

Amesema wengine milioni 1.1 wameathiriwa na mafuriko na kuongeza kwamba serikali ya shirikisho tayari imewapatia msaada unaohitajika.

Viongozi wa Tigray waomba msaada kutoka Addis na jumuiya ya kimataifa

Ethiopia | Tigray | Mzozo wa ukosefu chakula
Viongozi wa jimbo la Tigray wanasema takribani watu milioni moja wa jimbo hilo wamo kwenye kitisho cha baa la njaa.Picha: Million Haileselassie Brhane/DW

Getachew alisema kupitia mtandao wa kijamii wa X kwamba Tigray inakajongelewa na "janga la kibinadamu" kutokana na ukame na taathira za vita ambazo bado zinaendelea kushuhudiwa.

Mzozo kati ya vikosi vya serikali ya shirikisho na wapiganaji wa Tigray ambao ulizuka Novemba 2020 uliwauwa mamia kwa maelfu ya watu na karibu watu wengine milioni moja walipoteza makaazi.

Getachew amesema serikali ya jimbp la Tigray imetangaza hali ya janga kwenye maeneo yaliyo chini ya himaya yake lakini haina rasimali za kutosha kukabiliana na hali hiyo.

Imeomba serikali ya shirikisho iingilie kati kusaidia pamoja na kuirai jumuiya ya kimataifa kutoitupa mkono Tigray.

Shirika la Misaada la Marekani, USAID na Shirika la Mpango wa Chakula wa Umoja wa Mataifa, WFP, yalisitisha msaada wote wa chakula kwa Ethiopia mnamo mwezi June, kwa madai ya kuwepo "mtandao mpana na unaoendeshwa kwa ustadi"  kuiba shehena ya mahitaji yaliyotolewa.

Kitisho cha baa la njaa Tigray
Wakaazi wa Tigray wanatumia masalia ya nafaka kama chakula Picha: DW

Hata hivyo hivi sasa juhudi za kuanza kupeleka tena msaada zimeanza japo kwa mwendo wa kobe.

Getachew alikuwa taswira ya wapiganaji wa Tigray waliokuwa wakipambana na serikali wakati wa vita. Hivi sasa anaongoza serikali ya mpito iliyoundwa Novemba 2022 kufuatia mkataba wa amani uliotiwa saini mjini Pretoria, Afrika Kusini.

Ni vigumu kueleza kwa uhakika hali halisi jimboni Tigray kwa sababu serikali mjini Addis Ababa inazuia vyombo vya habari kwenda eneo hilo.