1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Eti kweli vikosi vya ausalama vya Libya vimepatiwa mafunzo na polisi wa Ujerumani?

Marx, Bettina (DW Berlin) 7 Aprili 2008

Bunge la shirikisho linakutana jumatano ijayo kujadili kadhia hiyo

https://p.dw.com/p/DdMS
Eti kikosi maalum cha polisi kutoka jimbo hili la mto Rhine kinasemekana kuwapatia mafunzo wanajeshi wa ulinzi wa LibyaPicha: picture-alliance/Bildfunk


Kisa cha kupatiwa mafunzo vikosi vya usalama vya Libya na wataalam wa kutoka Ujerumani kinazidi kuhanikiza humu nchini.Kuna eti eti za kila aina ,lakini ukweli bado haujulikani.Kimoja ni dhahir:kisa hicho kinahitaji kufafanuliwa.


Kisa cha kupatiwa mafunzo vikosi vya usalama vya Libya na askari polisi wa Ujerumani kinazidi kutatanisha.Gazeti la "Bild am Sonntag" limeripoti kansela wa zamani Gerhard Schröder ndie aliyekubaliana na kiongozi wa mapinduzi ya Libya Muammar Al Gaddafi kuhusu mpango huo.Alipokutana  na Gaddafi mwaka 2004,Gerhard Schröder alimuahidi msaada huo wa mafunzo.Alitaka kumshukuru kwa msaada wa Libya katika kukombolewa familia Wallert iliyokua ikishikiliwa mateka nchini Philippinnes.Familia  hiyo ya kijerumani ilitekwa nyara na waasi wa kiislam mwaka 2000  na kushikiliwa kwa miezi kadhaa nchini Philippines.Waliachiwa huru baada ya mazungumzo tete ya muda mrefu.


Gazeti la "Berliner Tagesspiegel" limeripoti kwa upande wake hata wizara ya ulinzi ilihusika na kisa hicho.Mkuu wa askari kanzu wanaomlinda kiongozi wa vikosi vya jeshi la Ujerumani Wolfgang SCHNEIDERHAN aliwapatia mafunzo walinzi wa kiongozi wa mapinduzi ya Libya Muammar Gaddafi kati ya mwaka 2005 na 2006.Wizara ya ulinzi ya serikali kuu ya Ujerumani iliamuru kati kati ya mwaka 2006 uchunguzi ufanywe kuhusu kisa hicho.


Awali ilitajikana kwamba polisi wa kutoka jimbo la Northrhinewestfalia,waliohusika na kisa hicho,walifanya hivyo kutokana na kandarasi pamoja na kampuni moja la kibinafsi bila ya kuwaarifu wakuu wao kazini.Waliwapatia mafunzo wanajeshi wa usalama wa Libya katika wakati walipokua likizo na kulipwa fedha taslim.Mwanesheria mkuu wa jimbo la Northrhinewestaflia mjini Dusseldorf anaachunguza kisa hicho.Msemaji wake Johannes Mocken anaelezea:


"Hatuna ushahidi wowote kama idara ya upelelezi ya Ujerumani BND imehusika na kisa hicho.Na hatujapata habari zozote kuhusiana na madai eti mazungumzo yalifanyika katika ofisi za ubalozi wa Ujerumani mjini Tripoli."


Katika ripoti za vyombo vya habari ilitajwa kwamba idara ya upelelezi BND iliarifiwa kisa hicho.Msemaji wa BDN amekanusha ripoti hizo.Kwa mujibu wa jarida la "Der Spiegel",hata ubalozi wa Ujerumani mjini Tripolis uliarifiwa.Mwenyekiti wa kundi la wabunge wa chama cha Christian Democratic Union-CDU,Wolfgang Bosbach anataka uchunguzi ufanywe.


"Sitokua tena na lakusema ikidhihirika kama kweli idara ya upelelezi BND imehusika na kisa hicho na ubalozi wa Ujerumani mjini Tripoli kukiunga mkono."

Wanasiasa wa kutoka vyama vyote vya kisiasa wanataka taasisi ya uchunguzi wa bunge PKG ishughulikie kadhia hiyo hivi sasa.Jumatano ijayo bunge la shirikisho Bundestag linapanga kujadili kadhia hiyo.