1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

EU kuirai Hungary kuhusu msaada kwa Ukraine

1 Februari 2024

Viongozi wa Umoja wa Ulaya Alhamis watajaribu kumrai Waziri Mkuu wa Hungary Viktor Orban kujiunga na mpango wa kuifadhili Ukraine ila wako tayari pia kuendelea na mpango wao iwapo watashindwa kumridhisha Orban.

https://p.dw.com/p/4buGH
Moldova | Mkutano wa Kilele Umoja wa Ulaya Bulboaca | Zelenskiy na Orban
Viongozi wa Umoja wa Ulaya pamoja na Volodymyr Zelenskiy wa UkrainePicha: Ludovic Marin/AFP/Getty Images

Mpango huo unajumuisha kuisaidia Ukraine kuyatimiza mahitaji yake ya kati ya mwaka 2024 hadi 2027 kwa kuipa yuro bilioni 33 kama mkopo na bilioni 17 zengine ambazo haitohitajika kuzilipa.

Fedha hizo zitatoka kwenye bajeti ya Umoja wa Ulaya ili kuiwezesha Ukraine kifedha wakati inapopambana na uvamizi wa Urusi.

Hakuna uhakika kuhusu msaada wa Marekani kwa Ukraine

Mkutano wa kilele ulioitwa Alhamis kwa ajili ya suala hilo ndio fursa ya mwisho ya kufikia makubaliano kabla kuuwacha mpango wa kutumia bajeti ya Umoja wa ulaya kama njia ya kuifadhili Ukraine.

Uhispania | Mkutano wa Kilele Umoja wa Ulaya Granada | Zelenskiy na Orban
Waziri Mkuu wa Hungary Viktor Orban(kushoto) na Rais Zelenskiy wa Ukraine(kulia)Picha: Ludovic Marin/AFP/Getty Images

Hatua hii ni muhimu wakati ambapo kuna ati ati kuhusiana na ufadhili kutoka Marekani kwasababu ya mivutano iliyoko katika bunge kuhusu kufadhiliwa kwa Ukraine.

Umoja wa Ulaya umekuwa ukiisaidia Ukraine tangu Moscow ilipoivamia mwaka 2022, ila imekuwa ni kupitia makubaliano ya serikali za umoja huo ambayo yanahitaji uidhinishwaji wa kitaifa kila mwaka na gharama yake ni kubwa kuliko ufadhili kupitia bajeti ya Umoja wa Ulaya.

Ukraine kuishiwa na fedha za matumizi serikalini

Ili kuitumia bajeti ya Umoja wa Ulaya, nchi zote 27 wanachama wa Umoja huo zinastahili kuridhia na Hungary iliyo na mahusiano ya karibu na Urusi, inataka kura ya turufu kuhusu kutolewa kwa fedha hizo kila mwaka. Wanachama wengine 26 wa Umoja wa Ulaya wameyakataa hayo matakwa ya Hungary na wamekuwa katika njia panda tangu Desemba.

Rais wa Urusi Vladimir Putin katika hospitali ya kijeshi
Rais wa Urusi Vladimir PutinPicha: Kristina Kormilitsyna/dpa/picture alliance

Umoja wa Ulaya hauwezi kusubiri zaidi kwa kuwa Ukraine inatarajiwa kuishiwa na fedha za kuendesha shughuli za kitaifa mnamo mwezi Machi.

Rasimu ya mapendekezo ya mkutano huo wa Alhamis iliyoonekana imeonyesha kuwa, ili kuyakubali kwa kiasi fulani matakwa ya Hungary, viongozi hao watapendekeza kufanyika kwa mjadala kila mwaka kuhusiana na jinsi msaada wa Umoja wa Ulaya unavyotumiwa na Ukraine, bila kuipa Hungary haki ya kuitisha kura ya turufu ya kupinga utoaji wa fedha hizo.

Haijulikani iwapo Orban atakubaliana na mpango kama huo. Balozi wa Orban katika Umoja wa Ulaya hapo Jumatano katika mkutano wa maandalizi aliwaambia wenzake wa Ulaya kwamba, Budapest bado inataka nguvu za kura ya turufu.

Vyanzo: DPAE/Reuters