1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

EU na Marekani zakutana .

8 Oktoba 2010

Umoja wa Ulaya na Marekani zimefanya mazungumzo hapo jana kujadili kuimarisha ushirikiano wa kupambana na tishio kwa usalama.

https://p.dw.com/p/PZIX
Waziri wa ndani wa Ujerumani Thomas de Maiziere, akizungumza na mweziwe wa Uswidi Tobias Billstroem katika mkutano wa mawaziri wa ndani wa Umoja wa Ulaya mjini Luxembourg.Picha: picture-alliance/dpa

Maafisa wa Umoja wa Ulaya  wameahidi kuchukua hatua yenye ushirikiano zaidi  kupambana na tishio la kigaidi wakati uzito wa tahadhari zilizotolewa na Marekani  juma lililomalizika kuhusu uwezekano wa kutokea mashambulio hayo barani Ulaya  pindi ukithibitishwa.

Ahadi hiyo ilitolewa katika mkutano uliofanyika hapo jana huko Luxembourg kati ya Umoja huo na Marekani.

Naibu waziri wa usalama wa ndani kutoka nchini Marekani Jane Holl Lute, alialikwa  kuhudhuria mkutano wa kawaida wa Umoja wa Ulaya wa mawaziri wake wa masuala ya ndani, mjini Luxembourg  kulijadili suala la ushirikiano wao dhidi tishio hilo la usalama.

Afisa wa Umoja huo anayehusika na kupambana na ugaidi, Gilles De Kerchove aliwaambia waandishi habari baada ya mkutano huo kuwa Lute amedhibitisha ukweli na uwepo wa tishio hilo la kigaidi bila ya kufafanua ni kipi hasa kilicholengwa katika tishio hilo.

Marekani ilitoa tahadhari hiyo baada ya kituo cha habari cha Fox kutoa taarifa kuwa kundi la kigaidi la Al Qaeda  lilikuwa linapanga  mashambulio ya ushirikiano katika maeneo makuu ya utalii mjini Paris Ufaransa, na Berlin Ujerumani, yaliyo mithili ya mashambulio  ya Mumbai ya mwaka 2008 yaliosaabisha vifo vya watu 163.

Waziri wa ndani wa Ubeligiji, AnnemieTurtelboom,ambaye nchi yake ndiyo inayoshikilia urais wa kuzunguka wa Umoja huo wa Ulaya alizipa uzito mdogo mapendekezo  kuwa hatua hiyo ya Marekani iliyojibiwa kwa dharura na Umoja huo wa Ulaya , ilizidishwa kuwa kubwa bure.

Turtelbloom alisema kuwa huo ni mtazamo wa Marekani na Umoja huo una mtizamo wake vilevile na kuwa Marekani ina jukumu la kisheria kutoa taarifa zote walizo nazo kwa raia wake.

Awali waziri wa ndani wa Ujerumani Thomas de Maiziere alisema kuwa hakuna haja ya kuzuwa mshtuko kuhusu taarifa hizo

Kufuatia kauli hiyo,waziri Turtelbloom alisisitiza haja  ya Umoja huo wa Ulaya kushirikiana vyema zaidi  katika kujibu matokeo kama haya.

Ameongeza kuwa wanachama wenzake wengi wa Umoja huo wamesisitiza haja ya kuwa na sauti moja  hivyo serikali zilizo wanachama wa Umoja huo zinapaswa kuitahadharisha taasisi ya pamoja inayohusika namatukio,( SitCen ) kabla ya kutoa tahadhari  kwa raia kuhusu tishio la kigaidi na vile vile kujaribu kuleta uwiano katika viwango vya tishio hilo .

Waziri Turtel Bloom alipendekeza kwamba maafisa wa wizara ya usalama wa ndani ya Marekani  na mawaziri wa   ndani wa Umoja huo wa Ulaya wakutane angalau mara moja kwa mwaka,  na ameahidi pia   ubadilishanaji wa taarifa zaidi katika eneo zima la bahari ya  Atlantik kupitia mfumo wa rekodi za majina ya wasafiri (PNR)  kwa abiria wanaosafiri kwa ndege,  jambo linaloendelea kujadiliwa  hivi sasa.

Mwandishi Maryam Abdalla

Mhariri:  Abdul-Rahman