1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

EU yajadili mkataba wa kulinda mazingira

Thelma Mwadzaya12 Desemba 2008

Mkutano wa viongozi wa Umoja wa Ulaya umeingia siku yake ya pili na ya mwisho mjini Brussels nchini Ubelgiji.Viongozi hao wanajadili mikakati mbadala ya kupambana na athari za mabadiliko ya hali ya anga

https://p.dw.com/p/GEgh
Viongozi wa Umoja wa Ulaya wanaokutana mjini Brussels,UbelgijiPicha: AP

Kwa upande mwingine mataifa masikini wanachama wa Umoja huo yanapinga vikali mapendekezo hayo kwa kuhofia athari katika sekta zao za nishati.

Rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa aliye mwenyekiti wa zamu wa Umoja wa Ulaya amewasilisha mapendekezo maalum yanayosubiri idhini ya nchi wanachama.Kikao hicho cha siku mbili kinachofanyika mjini Brussels,nchini Ubelgiji kinakamilika hii leo.Suala linalozua mvutano katika ajenda ya kikao hicho ni hatua ya kupunguza viwango vya gesi za viwanda kwa asilimia 20 ifikapo mwaka 2020.


Kwa mujibu wa rasimu ya mpango huo viongozi hao wa Umoja wa Ulaya wameahidi kuchukua hatua za kupunguza viwango vya gesi za viwanda kwa asilimia 20 ifikapo mwaka 2020.Hata hivyo kulingana na wanadiplomasia hao maelezo kamili ya hati yenyewe bado hayajabainika jambo linalowatia hofu makundi ya wanaharakati wa mazingira.


Rasimu yenyewe inaidhinisha mpango wa Umoja wa Ulaya unaolenga kuukwamua uchumi wa Jumuiya hiyo unadorora.Baadhi ya nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya wanapinga mapendekezo ya kupambana na tatizo hilo.Itakumbukwa kuwa ni miaka 80 tangu msukosuko wa fedha wa aina hii kushuhudiwa. Kulingana na makundi ya wanaharakati wa mazingira Umoja wa Ulaya huenda ukapunguza uaminifu wake endapo mkataba huo mpya utapunguzwa makali.Mkataba wa Kyoto unamalizika mwaka 2012.Majadiliano maalum yanayolenga kuunda mkataba mpya yamepangwa kufanyika mwaka ujao.

Kulingana na rasimu ya mpango huo Umoja wa Ulaya utafadhili mipango ya kupambana na athari za mabadiliko ya hali ya anga itakayoanzishwa katika mataifa masikini wanachama wa jumuiya hiyo.


Mataifa tisa yaliyokuwa sehemu ya Muungano wa Sovieti wa zamani huenda yakaupinga mkataba huo endapo vituo vyao vya kuzalisha nishati vinavyotumia makaa ya mawe vitafungwa kwasababu ya athari zake katika mazingira.Mpango huo mpya una azma ya kutoa msukumo zaidi katika juhudi za kuzalisha vilevile matumizi ya nishati mbadala.Chini ya mfumo uliopo sekta za nishati za mataifa hayo zimesamehewa kulipia vibali vinavyoyaruhusu utoaji wa viwango fulani vya gesi zinazoharibu mazingira katika shughuli zao za kuzalisha nishati, katika kipindi kitakachoanza mwaka 2013 hadi 2020.


Hata hivyo haijabainika iwapo wawakilishi wa mataifa hayo ya Ulaya mashariki yataunga mkono mapendekezo hayo mapya katika sehemu ya mwisho ya kikao cha viongozi wa Umoja huo.

Kikao hicho cha siku mbili kinakamilika hii leo.