1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

EU yakataa kutoa uanachama wa haraka kwa Ukraine

Iddi Ssessanga
11 Machi 2022

Viongozi wa Umoja wa Ulaya waliokutana nchini Ufaransa Alhamisi wamekataa kutimiza matakwa ya Ukraine ya kuingizwa haraka katika umoja huo, huku wakijadiliana kuhusu njia za kuisaidia nchi hiyo iliyovamiwa na Urusi.

https://p.dw.com/p/48KNo
Ukraine-Konflikt - EU-Gipfel in Versailles
Picha: Chigi Palace Press Office/IMAGO/ZUMA Wire

Mataifa ya Umoja wa Ulaya yameungana kikamilifu kuunga mkono upinzani wa Ukraine, na kupitisha vikwazo vya kiuchumi visivyo na kifani dhidi ya Urusi katika muda wa wiki mbili zilizopita.

Lakini viongozi wamegawanyika kuhusu jinsi Brussels inaweza kuchukua hatua kwa haraka kuikubali Ukraine kama mwanachama, na jinsi jumuiya hiyo ya mataifa 27 inavyoweza kukata uhusiano wa nishati na Moscow.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy ameomba nchi yake ipatiwe uanachama wa haraka wa Umoja wa Ulaya kama uthibitisho wa kuungwa mkono na washirika wake wa Umoja wa Ulaya.

Ukraine-Konflikt - EU-Gipfel in Versailles
Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula vonder Leyen akiwa mkutano wa kilele wa wakuu wa mataifa ya umoja huo mjini Versailles, kujadili mzozo wa Ukraine, Machi 10,2022.Picha: Eric Lalmand/BELGA/dpa/picture alliance

Soma pia: Wito watolewa Urusi kuchunguzwa kwa uhalifu wa kivita

Makubaliano kuhusu hatua hiyo, hata hivyo, hayatafikiwa wakati wa mkutano wa kilele wa siku mbili unaofanyika katika kasri la Versailles magharibi mwa Paris, ambako rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alimkaribisha mwenzake wa Urusi Vladimir Putin mnamo 2017.

Baada ya masaa tisa ya mazungumzo ya mgogoro, wakuu wa nchi na serikali walimaliza siku ya kwanza ya majadiliano kwa makubaliano juu ya lugha inayotambua "shauku ya Ukraine ya kujiunga na Umoja wa Ulaya", lakini waliacha kwenda mbali zaidi katika mchakato huo.

"Ilikuwa fursa ya kuonyesha uungwaji mkono usioyumba, thabiti kwa Ukraine, yaani, kujitolea kifedha, mali," rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya Charles Michel alisema. "Ni wazi kwamba Ukraine ni mwanachama wa familia ya Ulaya na tunataka kuunga mkono juhudi zote za kuimarisha na kuunganisha uhusiano na Ukraine."

Kwa sasa, Ukraine ina "Mkataba wa Ushirikiano'' tu na Umoja wa Ulaya, ambao unalenga kufungua masoko ya Ukraine na kuileta karibu na Ulaya. Inajumuisha mapatano makubwa ya biashara huria na kusaidia kufanya uchumi wa Ukraine kuwa wa kisasa.

Soma pia: Putin atangaza operesheni za kijeshi Ukraine

Jaribio la Ukraine la kupata uanachama wa haraka imepata uungwaji mkono wa hali ya juu kutoka nchi za Ulaya Mashariki, lakini maafisa wa Umoja wa Ulaya wamesisitiza kuwa mchakato huo unaweza kuchukua miaka, huku umoja kati ya wanachama wa sasa ukihitajika kuruhusu mgeni katika klabu hiyo.

Ukraine-Konflikt - EU-Gipfel in Versailles
Rais wa Ufaransa Macron akisalimiana na kansela wa Ujerumani Olaf Scholz mjini Versailles, Ufaransa, Machi 10, 2022. Picha: Chema Moya/IMAGO/Agencia EFE

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alisema EU lazima itume "ishara kali'' ya kuunga mkono Ukraine, lakini akafutilia mbali uwezekano wa nchi hiyo kujiunga na umoja huo hivi karibuni.

Je, tunaweza kufungua leo utaratibu wa kujiunga (na EU) na a nchi iliyoko vitani? Sidhani hivyo,'' Macron alisema. "Je, tufunge mlango na kusema (kwa Ukraine): 'Kamwe?' Hiyo itakuwa si haki.''

Waziri Mkuu wa Uholanzi Mark Rutte alisema alimuambia Zelenskyy kwamba kukubaliwa kwa Ukraine katika Umoja wa Ulaya hakuwezi kuharakishwa.

Soma pia: Ukraine yaiomba Ujerumani silaha za kujilinda dhidi ya Urusi

"Hakuna kitu kama uidhinishwaji wa haraka, utaratibu wa haraka,'' Rutte alisema. "Pia inabidi tuzingatie mataifa ya Balkan Magharibi, ambayo wakati mwingine yamekuwa yakifanya kazi kwa zaidi ya muongo mmoja ili kuwa taifa linaloomba uanachama. Fikiria Albania na Makedonia. Hebu tuone kile tunachoweza kufanya kwa maana ya vitendo.''

Hakuna muafaka mazungumzo ya Uturuki

Baada ya mazungumzo na mwenzake wa Urusi Sergei Lavrov nchini Uturuki, waziri wa mambo ya nje wa Ukraine Dmytro Kuleba amesema hakuna maendeleo hata juu ya usitishaji mapigano wa saa 24, ingawa Lavrov alisema Moscow itaendelea kuzungumza.

Vikosi vya Urusi vilikuwa vinaizingira miji mikubwa isiyopungua minne nchini Ukraine siku ya  Alhamisi, ambapo magari ya kijeshi yalikuwa yakielekea upande wa kaskazini-mashariki mwa mji mkuu Kyiv, ambako viunga vyake vikiwemo Irpin na Bucha vimehimili siku kadhaa za mashambulizi makubwa.

Soma pia: Urusi,Ukraine washindwa kufikia mwafaka huko Uturuki

Meya wa Kyiv Vitali Klitschko amesema nusu ya wakaazi wamekimbia, na kuongeza kuwa mji huo umegeuzwa kuwa ngome.

Mji wa kusini uliozingirwa wa Mariupol wakati huo huo umekabiliwa na mashambulizo mapya ambapo rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy ameituhumu Urusi kwa kuanzisha mashambulizi ya vifaru dhidi ya njia ya kitu inayotumika kujaribu kufikisha chakula, maji na dawa mjini humo.

Türkei | Kuleba, Lawrow, Cavusoglu - Außenministertreffen in Antalya
Waziri wa mambo ya nje wa Uturuki Mevlut Cavusoglu, waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov na waziri wa mambo y nje wa Ukraine Dymtro Kuleba wakihudhuria mkutano wa Urusi-Uturuki-Ukraine mjini Antalya, Machi 10, 2022.Picha: Cem Ozdel/AA/picture alliance

Mashambulizi hayo ambayo Zelenskiy ameyaelezea katika taarifa ya vidio kuwa ugaidi wa wazi, yamekuja siku moja baada ya kupiga mabomu hospitali ya watoto mjini humo, ambayo maafisa wamsema yaliuwa watu watatu, akiwemo msichana modogo.

Zelenskiy amelitaja shambulio la Urusi dhidi ya hospitali kuwa "uhalifu wa kivita", msimamo ambao umeungwa mkono na maafisa wa Umoja wa Ulaya.

Jeshi la Urusi hata hivyo limesema shambulio la hospitali lilikuwa "uchokozi uliopangwa" na Ukraine.

Vikwazo zaidi kwa kuwalenga raia

Waziri wa fedha wa Marekani Janet Yellen amesema kuzidi kulengwa kwa raia kunaweza kuisukuma Washington na washirika wake wa Ulaya kuimarisha zaidi vikwazo visivyokifani dhidi ya Moscow, huku Ikulu ya Wahite House ikikosa kile ilichokiita matumizi ya kifedhuli ya nguvu dhidi ya raia.

Serikali ya Ukraine imesema karibu watu 100,000 wameondolewa katika muda wa siku mbili, kutoka maeneo ya mji wa kaskazini-mashariki wa Sumy, kaskazini-magharibi mwa Kyiv na mji wa mashariki wa Izyum.

Soma pia: Urusi na Ukraine zakubaliana kusitisha mapigano kwa siku nzima

Urusi ilisema Alhamisi kwamba pia itafungua njia za kiutu za kila siku kuondoa raia kwenda maeneo ya Urusi, lakini Kyiv imesisitiza hakuna njia za uondoaji zinapaswa kuelekea Urusi.

Wagonjwa wa Ukraine wakimbilia Poland

Shirika la wakimbizi la Umoja wa Mataifa linakadiria kuwa zaidi ya wakimbizi milioni 2.3 wameondoka Ukraine tangu Urusi ilivyoushtua ulimwengu kwa kuivamia nchi hiyo Februari 24, na karibu Waukraine milioni 1.9 wamegeuka wakimbizi wa ndani.

Kwa ujumla, watoto wasiopungua 71 wameuawa nchini Ukraine tangu kuanza kwa vita, na zaidi ya 100 wamejeruhiwa. Hali mjini Mariupol ni mbaya hasa, ambapo siku 10 za mashambulizi zimesababisha vifo vya raia zaidi ya 1,200 kwa mujibu wa meya wa mji huo.

Baraza la usalama kujadili madai ya Urusi

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa linatarajiwa kukutana kujadilia madai ya Urusi juu ya mipango ya siri ya Marekani kuunda maabara za siri nchini Ukraine, kwa ajili ya kutengeneza silaha za kibayolojia.

Marekani imekanusha madai hayo na kuonya kwamba Urusi inataka kutumia madai hayo kama kisingizio cha kutumia silaha za aina hiyo dhidi ya Ukraine.

Soma pia: Urusi inahujumu makubaliano ya Nyuklia ya Iran ?

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy pia amekanusha madai hayo katika hotuba yake ya usiku wa kuamkia leo na kuyataja kama ishara mbaya.

Zelenskiy amesema ana wasiwasi sana kwa sababu wanaamini kwamba ukitaka kujua mipango ya Urusi, basi ndiyo kile ambacho Urusi inawatuhumu wengine kukifanya.

Marekani yaionya Urusi kuhusu mali ya mashirika ya kigeni

Ikulu ya White House inaionya Urusi dhidi ya kuchukua hatua za kukamata mali za makampuni ya Marekani na ya kimataifa ambayo yametangaza mipango ya kusimamisha shughuli nchini Urusi au kujiondoa katika soko la Urusi kujibu uamuzi wa Vladimir Putin wa kuvamia Ukraine.

Raia wa Ukraine wazidi kukimbia nchi

Jen Psaki, msemaji wa ikulu, alikuwa akijibu ripoti katika vyombo vya habari vya Urusi na vyombo vingine vya habari kuhusu pendekezo la kutaifisha mali za makampuni makubwa ya kigeni ambayo yanaondoka Urusi.

Psaki anasema Alhamisi kwenye Twitter kwamba hatua kama hiyo itakuwa ya kurudi nyuma mwaka wa 1917 na kwamba Urusi italazimika kuishi kwa miongo kadhaa na kutokuwa na imani kwa wawekezaji. Anasema Urusi pia inaweza kukabiliwa na madai ya kisheria kutoka makampuni ambayo mali zao zimekamatwa.

Soma pia: Waukraine wakimbia huku marufuku ya mafuta ya Marekani ikikaribia

Psaki anasema Ikulu ya Marekani inasimama pamoja na makampuni ya Marekani ambayo yanafanya kile alichokiita ``maamuzi magumu'' kuhusu mustakabali wa shughuli zao nchini Urusi.

Gazeti la Urusi Izvestia liliripoti Alhamisi kwamba serikali na ofisi ya mwendesha mashtaka mkuu walikuwa wakizingatia pendekezo la kutaifisha makampuni ya kigeni ambayo yametangaza kujiondoa Urusi kwa sababu ya vita vya Ukraine.

Gazeti hilo lilisema lilikuwa na orodha ya takriban kampuni 60, zikiwemo IKEA, McDonald's, Apple, Microsoft, IBM na Porsche, miongoni mwa nyengine.

Makala hiyo ilisema baadhi walikuwa wakihimiza tahadhari. Mtaalamu mmoja aliyenukuliwa alionya dhidi ya hatua za haraka, akisema baadhi ya biashara zilikuwa zikifanya chini ya shinikizo kutoka kwa serikali zao na kwamba itakuwa vibaya kuhitimisha kwamba wamefunga milango yao kwenye soko la Urusi milele.

Wanafunzi wa Tanzania wajificha nchini Ukraine

Marekani yapanga kufuta hadhi ya Urusi ya upendeleo wa kibiashara

Rais Joe Biden atatangaza Ijumaa kuwa, pamoja na Umoja wa Ulaya na kundi la mataifa saba yalioendelea zaidi duniani, G7, Marekani itachukua hatua ya kufuta hadhi ya "taifa linalopendelewa zaidi" kibiashara ya Urusi kutokana na uvamizi wake nchini Ukraine.

Soma pia: Maoni: Msaada wa NATO na Magharibi kwa Ukraine hautoshi

Hayo ni kwa mujibu wa chanzo kinachofahamu suala hilo ambacho kilizungumza kwa sharti la kutotajwa jina ili kuhakiki tangazo hilo.

Hatua ya Biden inakuja wakati shinikizo lisiloegemea vyama limekuwa likiongezeka mjini Washington kutaka kubatilisha kile kinachojulikana rasmi kama ``mahusiano ya kudumu ya kibiashara ya kawaida'' na Urusi. Hatua hiyo ingeruhusu Marekani na washirika wake kuziweka ushuru bidhaa za gesi ya Kirusi.

Baraza la Seneti lapitisha bajeti kuisadia Ukraine

Baraza la Seneti la Marekani limetoa idhini ya mwisho ya bunge kwa mfuko wa dharura wa dola bilioni 13.6 wa msaada wa kijeshi na kibinadamu kwa Ukraine iliyozingirwa na washirika wake wa Ulaya. 

Hatua hiyo ilipita kwa 68-31. Bunge lilipitisha mswada huo wa muafaka kwa urahisi siku ya Jumatano. Rais Joe Biden anatarajiwa kuutia saini.

Ukraine-Konflikt - Mariupol
Wazima moto wakimsaidia mwanamke kutoka kwenye ghorofa lililoharibiwa na mashambulizi mjini Mariupol, Ukraine, Machi 10, 2022.Picha: Evgeniy Maloletka/AP Photo/picture alliance

Takriban nusu ya kiasi cha dola bilioni 13.6 zilikuwa kwa ajili ya kuipatia Ukraine silaha na vifaa vingine pamoja na gharama za wizara ya ulinzi, Pentagon, kutuma wanajeshi wa Marekani katika mataifa mengine ya Ulaya Mashariki yanayohofia vita kwenye taifa jirani.

Soma pia:Biden: Putin alijidanganya anaweza kusambaratisha NATO 

Sehemu ya kilichobaki inajumuisha misaada ya kibinadamu na kiuchumi, kuimarisha ulinzi wa washirika wa kikanda na kulinda ugavi wao wa nishati na mahitaji ya usalama wa mtandao.

Wanademocat na Warepublican wamepambana mwaka huu wa uchaguzi juu ya kupanda kwa mfumuko wa bei, sera ya nishati na vikwazo vya janga la muda mrefu.

Lakini wameungana juu kupeleka msaada kwa Ukraine, ambayo ni uthabiti wake wa kustajabisha dhidi ya Urusi umekuwa msukumo kwa wapiga kura wengi.

Chanzo: Mashirika