1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Euro 2022: Ujerumani yafuzu kuingia kwenye robo fainali

Zainab Aziz Mhariri: Chilumba Rashid
13 Julai 2022

Timu ya kina dada wa Ujerumani imefaulu kuingia kwenye robo fainali katika mashindano ya kandanda ya kugombea ubingwa wa mataifa ya Ulaya kwa wanawake baada ya kuilaza Uhispania mabao 2-0.

https://p.dw.com/p/4E33H
Frauen Fußball EM 2022 | Deutschland vs Spanien
Picha: LISI NIESNER/REUTERS

Kilele cha uhondo wa soka hapo jana usiku lilikuwa pambano kati ya Uhispania na Ujerumani. Hapakuwa na haja ya kupiga ramli ili kujua matokeo.Licha ya kuingia na matuamaini ya juu kwenye uwanja wa mji wa Brentford, wahispania hawakufua dafu mbele ya Ujerumani.

Klara Buhl wa timu ya kina dada wa Ujerumani akishangilia baada ya kufunga bao la kwanza.
Klara Buhl wa timu ya kina dada wa Ujerumani akishangilia baada ya kufunga bao la kwanza.Picha: DYLAN MARTINEZ/REUTERS

Akina dada wa Uhispania walijiuma vidole katika dakika ya tatu baada ya mlinda lango wao kufanya kosa ambalo hatalisahau maisha yake yote. Alitoa zawadi kwa Ujerumani. Golikipa huyo alitaka kutoa pasi kwa beki wake lakini boli lilienda moja kwa moja kwenye miguu ya fowadi wa Ujerumani karibu na lango la Uhispania na akaujaza mpira wavuni. Maafa kwa wahispania yaliendelea katika dakika ya 36 ambapo wajerumani walijipatia goli la pili la kichwa.

Ushindi huo maana yake Ujerumani itaingia mapema katika robo fainali ambapo itakutana na Finland hapo jumamosi. Leo jioni Uswisi itakumbana na Sweden na waholanzi watakuwa na miadi na timu ya akina dada wa Ureno.

Mchezaji wa Ujerumani Alexandra Poppjezi namba 11 akishangilia baada ya kufunga bao la pili akiwa na wachezaji wenzake.
Mchezaji wa Ujerumani Alexandra Poppjezi namba 11 akishangilia baada ya kufunga bao la pili akiwa na wachezaji wenzake.Picha: LISI NIESNER/REUTERS

Katika mechi ya ufunguzi kina dada wa Denmark waliangukia patuputu pale walipoumbuliwa na Ujerumani kwa kipigo cha mabao manne kwa bila, lakini hapo jana walipania katika mchezo wao dhidi ya timu ya Finland ambao pia waliadhibiwa na Uhispania kwa kubandikwa mabao manne kwa moja, katika mchezo wao wa kufungua dimba. 

Mkakati wa Denmark

Mkakati wa Denmark ulikuwa ni kudhibiti kabumbu huku wakishambulia mbinu ambazo hawakuweza kuzitumia katika mchezo wao wa kwanza na Ujerumani katika timu za kundi B. Hapo jana wanasoka wa Denmark waliyaonesha yote hayo na kuweza kuibuka kidedea. Waliwakausha akina dada wa Finland wanaotokea nchi ya maziwa 1000. Hukumu baada ya kupulizwa kipenga cha mwisho inasema Denmark moja Finland - nunge!. Denmark iliouna upenyo katika dakika ya 72 na kuutumia. Na hivyo akina dada wa Denmark wanaendeleza matumiani ya kusonga mbele katika mashindano hayo ya ubingwa wa wanawake wa mataifa ya Ulaya.