1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Fabius kuwasilisha mswada mpya wa mazingira

9 Desemba 2015

Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Laurent Fabius ameahidi kuwasilisha mswada mpya wa mkataba juu ya kupambana na athari za mabadiliko ya tabia nchi leo alasiri.

https://p.dw.com/p/1HJcW
Mwenekiti wa mkutano,Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Laurent Fabius
Mwenekiti wa mkutano,Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Laurent FabiusPicha: picture-alliance/Pacific Press via ZUMA Wire/J. Raa

Waziri Fabius ametoa mwito kwa nchi zote wa kuziweka kando tofauti zao ili mkataba hatimae upatikane.

Wakati zimebakia siku chache hadi kumalizika mkutano wa mjini Paris ,Waziri Fabius ambae ni mwenyekiti wa mkutano ,amesema leo atauwasilisha mswada mpya mfupi wa mkataba juu ya kupambana na mabadiliko ya tabia nchi.

Ameahidi kuwasilisha mswada mpya utakaokuwa mfupi na vipengele vichache ndani yake. Amesema hata ikiwa imani ya nchi zote itapatikana bado, "tutapaswa kupunguza tafauti zetu" ili mwafaka upatikane

Wajumbe kutoka nchi karibu 200 wanajadiliana juu ya njia za kukabiliana na athari zinazotokana na mabadiliko ya hali ya hewa kwenye mkutano huo wa mjini Paris ulioandaliwa na Umoja wa Mataifa.

Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Fabius amesema hali ni nzuri kwenye mkutano huo na kwamba sasa kilichobakia ni kufanya bidii ili mkataba unaosubiriwa na dunia upatikane.

Mkutano wa mjini Paris unazingatiwa kuwa fursa ya mwisho kwa binadamu ya kuweza kuepusha madhara makubwa kabisa yanayotokana kuongezeka joto duniani, hali inayosababisha ukame, mafuriko, dhoruba na kupanda kwa vina vya bahari na hivyo kutishia kuzizamisha sehemu fulani duniani.

Kazi bado inahitaji kufanyika ili kulifikia lengo kamili

Mwenyekiti wa mkutano Waziri Fabius amesema kuwasilishwa mswada mpya wa mkataba, itakuwa hatua muhimu , lakini lengo kamili litakuwa bado halijafikiwa. Siku ya mwisho ya kupatikana mkataba ni Ijumaa na wajumbe wanafanya bidii kuyatatua masuala magumu ili mkataba kamili upatikane hadi siku hiyo.

Maajabu ya asili
Maajabu ya asiliPicha: Fotolia/Christopher Meder

Nchi zinatafautiana juu ya namna ya kuzisaidia nchi zinaoendelea ili ziweze kuyakabili madhara yanayotokana na ongezeko la joto duniani. Mataifa pia yanatafautiana juu ya namna ya kuugawa mzigo wa gharama baina ya nchi tajiri na masikini.Nchi pia zinatafautina juu ya vigezo vya kupima maendeleo katika kupunguza utoaji wa gesi zinazoharibu mazingira.

Akizungumza pembezoni mwa mkutano , waziri wa mambo ya nje wa Marekani, John Kerry amesema ingawa bado pana masuala magumu ya kutatuliwa,anayo matumaini .

Wachunguzi wanasema hali mpya ya matumaini imejitokeza kwenye mkutano wa mjini Paris , miaka sita baada ya kushindikana kwa juhudi za kuupata mkataba kwenye mkutano uliofanyika mjini Copenhagen.

Mwandishi:Mtullya Abdu./afp,rtzre

Mhariri:Iddi Ssessanga