1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Fainali bora kabisa za kombe la dunia, wamesema wataalamu

3 Julai 2014

Magoli 154 yamekwishatinga nyavuni hadi sasa, fainali za kombe la dunia nchini Brazil zimekuwa moja ya fainali zenye msisimko mkubwa kuliko zote.

https://p.dw.com/p/1CVK9
Kolumbien Bogota Jubel WM 2014 Fans
Mashabiki wa Colombia wakifurahia ushindiPicha: Guillermo Legaria/AFP/Getty Images

Kuna mchanganyiko wa sababu zilizosababisha hali hiyo ,ambapo ni pamoja na washambuliaji wenye uwezo mkubwa, mafunzo mazuri na hali bora ya kimwili kwa wachezaji, pamoja na sheria mpya zilizoanzishwa na shirikisho la kandanda duniani FIFA kuwalinda nyota wa mchezo huo.

Ni watu wachache ambao wangekuwa na shaka kuwa kombe la dunia linalofanyika katika nchi ambayo mapenzi ya kandanda ni makubwa hayatakuwa na msisimko.

Neymar vs James Rodriguez Kombobild Torjäger Duell
Kulia ni James Rodriguez wa Colombia na Neymar wa Brazil (kushoto)Picha: picture-alliance/dpa

Ni burudani ya pekee

Lakini ile hali ya thamani ya kiburudisho inayotolewa na mashindano haya nchini Brazil imewasisimua hata wataalamu.

"Kombe hili la dunia ni la hali ya juu kabisa kutokana na ubora wake katika kutandaza kandanda na burudani," amesema Gerard Houllier.

"Nimeshangazwa mno na kiwango cha ubora katika mchezo," ameongeza Sunday Oliseh.

Fußball WM 2014 Brasilien Ottmar Hitzfeld
Kocha Ottmar Hitzfeld wa Uswisi ambaye ameamua kufikisha mwisho muda wake wa kufundisha soka kwa jumlaPicha: AFP/Getty Images

Watu hao wawili wanafahamu kile wanachokizungumza : Houllier ni kocha wa zamani wa timu ya Liverpool raia wa Ufaransa ambaye amefuatilia fainali tisa za kombe la dunia. Oliseh ni mchezaji wa zamani wa kati ambaye amecheza mara 63 katika kipindi cha muda wa miaka tisa ya uchezaji wake kandanda na timu ya taifa ya Nigeria ambapo ni pamoja na kushiriki katika fainali za kombe la dunia mwaka 1994 na 1998.

Wote hivi sasa ni wajumbe waandamizi wa shirikisho la kandanda duniani FIFA katika kundi la uchunguzi wa masuala ya kiufundi.

WM 2014 Achtelfinale USA Belgien Tor
De Bryune wa Ubelgiji baada ya upachika baoPicha: Reuters

Ikiwa magoli 154 tayari yameshatinga nyavuni hadi sasa , na ikiwa michezo minane bado haijafanyika , kombe la dunia mwaka 2014 linaweza kuzipiku rekodi zilizopita za magoli 171 iliyowekwa tangu mashindano hayo yalipopanuliwa na kuongezwa timu kuwa 32 mwaka 1998.

Wastani wa magoli uko juu

Wastani wa sasa wa magoli 2.8 kwa kila mchezo uko juu kuliko ilivyokuwa katika mashindano yaliyopita.

Ni maelezo gani yanayoweza kuambatana na burudani safi namna hiyo ya magoli pamoja na michezo ambayo inatia shauku kubwa na kujing'ata vidole.

Jibu ni jumla ya mambo mbali mbali, kwa mujibu wa wataalamu. Kwanza ni kwamba mashindano haya ya Brazil yamebarikiwa kuwa na kizazi cha washambuliaji hatari," anasema Houllier.

WM 2014 Achtelfinale Argentinien - Schweiz Jubel
Messi akimpongeza Di Maria baada ya kuweka wavuni bao la ushindi dhidi ya UswisiPicha: picture-alliance/AP Photo

Kila mmoja jicho lake liko kwa mshambuliaji wa Argentina Lionel Messi na Neymar wa Brazil. Lakini mashindano haya yametoa nyota wengine wapya duniani kama vile James Rodriguez, ambaye ni mfungaji bora kwa hivi sasa akiwa na magoli matano kutokana na michezo minne.

Goli lake la kwanza dhidi ya Uruguay katika uwanja wa Maracana, ambapo aliudhibiti mpira kwa kifua na kuachia kombora lililotinga nyavuni kutoka nje ya mita 30, limepata sifa kuwa moja ya goli zuri kabisa hadi sasa katika mashindano haya.

WM 2014 Achtelfinale Frankreich Nigeria
Wachezaji wa Ufaransa wakishangiriaPicha: Getty Images

Mbinu za kushambulia zinaleta burudani zaidi

Moja ya sababu kwanini mashabiki wameweza kushuhudia mambo mengi na magoli mengi ni kwamba timu nyingi zinacheza na washambuliaji wawili, na hata watatu, badala ya mfumo wa mshambuliaji mmoja ulioonekana mara nyingi hapo zamani. Inaonekana kuwa makocha wametambua kuwa mbinu za ushambuliaji zinaleta matunda, wanadai wataalamu hao.

WM 2014 Achtelfinale Brasilien Chile (Neymar beim Elftmeterschießen)
Neymar akionesha ufundi wake dhidi ya CroatiaPicha: Reuters

Sababu ya pili ni kasi ya mchezo huo. Michezo mingi nchini Brazil imechezwa kwa kasi kubwa bila ya muda wa kupumua, huku timu zikiwa tayari kuchukua fursa ya kosa lolote linalofanywa na wapinzani na kuwaadhibu. Kocha mmoja wa timu ya taifa amemweleza Houllier kuwa "haya yamekuwa mashindano ya kasi zaidi kuliko kombe la dunia lolote."

Leo jioni(04.07.2014) viwanja vitawaka moto tena huko Brazil wakati Ujerumani itakapokumbana na Ufaransa na Brazil ina miadi na Colombia.

Mwandishi : Sekione Kitojo/ dpae

Mhariri : Josephat Charo