1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Fayulu, Kabila wajitoa uchaguzi DRC

13 Julai 2023

Wanasiasa wawili muhimu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Martin Fayulu na Joseph Kabila, wametangaza kutowania urais kwenye uchaguzi wa Disemba wakidai kuwa tume ya uchaguzi inaendesha mchakato usio wa kidemokrasia.

https://p.dw.com/p/4TraI
Martin Fayulu
Picha: Nicolas Maeterlinck/BELGA/picture alliance

Baada ya Tume Huru ya Uchaguzi (CENI) kutupilia mbali madai ya viongozi wa upinzani kuhusu mchakato wa uchaguzi, Martin Fayulu, mmoja wa viongozi hao tayari amethibitisha hatua yake ya kujiondoa kwenye kinyang'anyiro cha uchaguzi.

Miongoni mwa madai waliyoyatowa walipokutana na mkuu wa CENI, Denis Kadima, siku chache zilizopita, upinzani ulisisitiza kuwa daftari la uchaguzi likaguliwe na kampuni huru yenye umaarufu na ujuzi wa kimataifa, lakini CENI iliyatupilia mbali masharti hayo.

Soma zaidi: Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kufanya uchaguzi mkuu Desemba 2023.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Kinshasa, Fayulu alikataa kabisa kushiriki katika kile alichokielezea kuwa ni maandalizi ya udanganyifu ya uchaguzi na akatishia hata kuwahamasisha Wakongo kudai mamlaka yao kupitia maandamano.

"Hatutawasilisha maombi yetu ya ugombeaji kwani tunakataa kumsindikiza Felix Tshisekedi na muungano wake katika udanganyifu mpya wa uchaguzi. Tunawakumbusha Wakongo kwamba kwa mujibu wa katiba, tuna wajibu wa kuzuia aina yoyote ya udikteta." Alisema mwanasiasa huyo ambaye uchaguzi uliopita alitazamiwa na wengi kushinda.

Kabila amuunga mkono Fayulu

Msimamo huo wa Fayulu unaungwa mkono na muungano wa FCC ambao kiongozi wake Joseph Kabila, rais wa zamani wa nchi hiyo, tayari ametangaza kujiondoa katika mchakato ambao ameuelezea kuwa sio wa kidemokrasia.

Kombobild DR-Kongo Politiker Joseph Kabila und Joseph Katumbi
Joseph Katumbi na Joseph Kabila, wanasiasa wa upinzani nchini DRC

Wafuasi wa FCC, muungano wa kisiasa wa rais wa zamani, Joseph Kabila, wameridhishwa na msimamo wa Fayulu ambapo Ferdinand Kambere, mmoja wa viongozi wa muungano huo, amempongeza kwa kuuchagua upande wa raia akikataa kama tu Kabila, kushiriki mchakato unaosema unakwenda kinyume na demokrasia.

Soma zaidi: Marekani yataka wanajeshi MONUSCO waondoke baada ya uchaguzi

"Kila mara mtu anapofuata njia halali, yaani anakataa kuaminisha mchakato unaohatarisha demokrasia nchini mwetu. Sisi kama FCC tunaridhika kwani tunapinga muelekeo wowote wa kidikteta. Mapambano haya tutayaendesha pamoja na wananchi hadi mwisho." Alisema Kambere.

Tshisekedi kunufaika na ususiaji wa wapinzani

Hata hivyo, baadhi ya wachambuzi wanaamini kuwa kujiondoa kwenye mchakato hakutabadili chochote kile katika mpango wa uchaguzi nchini Kongo.

DR Kongo Der Präsident der Demokratischen Republik Kongo Félix Tshisekedi
Rais Félix Tshisekedi wa DRCPicha: Giscard Kusema, der Kommunikationsmanager der Kongo-Präsidentschaft

"Kujiondoa Martin Fayulu kunawapunguzia watawala usumbufu. Ni jambo linalowaridhisha na hivyo mchakato unaendelea bila shaka kama wanavyozidi kusema. Haina athari kwa utawala ila inawafanyia kazi kuwa rahisi." Alisema Profesa Nkere Ntanda, mwalimu kwenye Chuo Kikuu cha Kinshasa, UNIKIN.

Soma zaidi: Uhusiano wa Rwanda na Kongo waghubika siasa kabla ya uchaguzi

Hayo yanajiri huku muungano wa Rais Tshisekedi, USN, ukiendelea kusisitiza kwamba uchaguzi utafanyika kama ulivyopangwa mnamo Desemba 20 ama wapinzani waususie ama washiriki.

Imeandaliwa na Jean Noel Ba-Mweze/DW Kinshasa