1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Fazul Mohammed nguzo ya Al-Qaida iliyoanguka

12 Juni 2011

Wachambuzi wanasema kifo cha mwanamgambo na kiongozi wa al Qaeda katika eneo la Afrika Mashariki Fazul Mohammed kilichotokea nchini Somalia kinaelezwa kuwa ni pigo kubwa katika utekelezaji wa operesheni za mtandao huo.

https://p.dw.com/p/11Yxu
Kiongozi wa al-Qaeda aliyeuwawa Fazul Abdullah MohammedPicha: picture-alliance/dpa

Kuuawa kwa mwanamgambo wa ngazi za juu wa kundi la kigaidi la al-Qaeda Fazul Mohammed unaliingiza kundi hilo katika majonzi makubwa ikiwa ni mwezi mmoja kufuatia kifo cha Osama bin Laden. Lakini dhima yake ya hivi karibuni kama mkufunzi wa wanamgambo wapya huenda imeacha kitisho kikubwa.

Polisi nchini Somalia jana ilitangaza kwamba Fazul Mohamed, aliekuwa akisakwa muda mrefu na aliekuwa mtaalamu wa kupanga mashambulizi, kujificha, kukwepa kukamatwa na hodari wa lugha aliuawa katika mji mkuu wa Somalia Mogadishu.

Kufuatia tangazo hilo, Marekani ilisema Fazul Mohammed anaejulikana pia kama Harun, ni mshukiwa mkuu kuhusiana na mashambulizi ya 1998 katika balozi za Marekani katika majiji ya Dar es salaam na Nairobi, ambapo watu 240 walipoteza maisha yao.

Inaaminiwa kuwa mzaliwa huyo wa Komoro alipanga shambulio la mwaka 2002 dhidi ya hoteli inayomilikiwa na Israel nchini Kenya na kusababisha vifo vya watu 15.

Lakini katika miaka ya hivi karibuni, baadhi ya wasomi na wataalamu wa masuala ya usalama waliamini kwamba Fazul Mohamed alikuwa akitumia muda mwingi kutoa mafunzo kwa wanamgambo sawa na kuaanda mipango ya kushambulia nchi za magharibi.Alikuwa akitoa mafunzo kwa vijana wa Kisomali na Waislamu wengine waliokwenda Somalia kupata ujuzi wa kijeshi.

Profesa Nelly Lahoud wa kituo cha kukabiliana na ugaidi katika chuo cha kijeshi cha West Point nchini Marekani anasema, Fazul Mohammed alikuwa mtu muhimu katika kupanga operesheni za mtandao wa al-Qaeda. Amesema kifo chake ni hasara kubwa kwa mtandao huo ingawa jukumu lake la hivi karibuni, kama mkufunzi bila shaka limenufaisha kundi.

Profesa Lahoud aliechunguza kitabu kilichoitwa "Vita dhidi ya Uislamu: Hadithi ya Fazul Harun" ambacho huelezea maisha ya Fazul Mohammed, amesema kuwa mwanamgambo huyo ametoa mchango mkubwa kwa mtanadao wa al Qaeda. Kwa maoni yake, Fazul Mohamed aliihisi kuwa aliwajibika kuwapa wenzake ujuzi aliokuwa nao.

Serikali ya Somalia imesema mamia ya wapiganaji wa kigeni walijiunga na mtandao huo wa kigaidi, wakitokea nchi mbalimbali kama Afghanstan, Pakistan, nchi za Ghuba na za Magharibi zikiwemo Marekani na Uingereza.

Baadhi yao wamekuwa viongozi wa makundi ya wanamgambo kama vile al Shabaab.

Maafisa wa usalama katika nchi za Magharibi pia walikuwa wakishuku kuwa Fazul Mohammed alikuwa akiratibu harakati zao pamoja na wanamgambo wa tawi la al Qaeda nchini Yemen. Hilo ni tawi lililohusika na mashambulizi makali yaliyofanywa na mtandao huo katika nchi za magharibi, miaka ya hivi karibuni.

Maafisi wa usalama waliomchunguza Fazul Mohammed wanasema alikuwa mtu makinifu na mjanja na aliezungumza lugha za Kiarabu, Kikomoro, Kiswahili na Kiingereza.

Muaustralia Leah Farrell alie mtaalamu wa masuala ya al-Qaeda, amesema ni kifo cha Fazul Mohamed kitaathiri uwezo wa al-Qaeda kuwepo katika kanda hiyo pamoja na operesheni zake katika nchi za kigeni.

Baadhi wa wataalamu wa masuala ya usalama, wanashuku kwamba mafunzo yaliyotelowa na Fazul Mohammed yamesaidia kupanga shambulio lililofanywa na kundi la al-Shabab mjini Kampala, Uganda mwaka 2010. Shambulio hilo limesababisha vifo vya watu 79 waliokuwa wakitazama fainali ya kombe la dunia.

Hilo lilikuwa shambulio la kwanza kabisa kufanywa na al Shebab katika nchi ya kigeni, kulipiza kisasi baada ya Uganda kuchangia wanajeshi katika kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Afrika nchini Somalia-AMISOM. Katika shambulio lingine, wanamgambo wa al-Shabaab walishambilua kambi kuu ya jeshi la Umoja wa Afrika Septemba 2009, mjini Mogadishu. Wanajeshi 17 waliuawa katika mashambulio mawili ya mabomu yaliyotegwa katika gari.

Hillary Clinton
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Hillary ClintonPicha: AP

Kufuatia kifo cha Fazul Mohammed, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Hillary Clinton alikaribisha habari hiyo akiwa ziarani nchini Tanzania. Aliwaambia waandishi wa habari kuwa kifo cha Fazul Abdullah Mohamed ni " pigo kubwa" kwa al-Qaeda na washirika wake katika kanda hiyo.

Mwandishi: Sudi Mnette / RTR

Prema Martin