1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Fedha nyingi kampeni za urais Marekani

15 Oktoba 2012

Wiki chache kabla ya uchaguzi wa rais Marekani, mamilioni ya fedha yanamiminika kwenye kambi za wagombea wawili wakuu, huku makampuni makubwa yakimpendelea Romney wakati Obama akichangiwa zaidi na walala hoi.

https://p.dw.com/p/16QCr
US Flagge, Obama, Romney -> Bitte nur für das Special verwenden 2012_08_30_USWahl.psd
Uchaguzi wa Rais Marekani 2012.

Rais Barack Obama anaweza asipende kuomba pesa, lakini mamia ya watu walio tayari kulipa zaidi ya dola 40,000 kuwepo katika hafla za uchangiaji zinazohudhuriwa na watu mashuhuri kwa heshima yake, inaonyesha wapo wengi waliyo tayari kuingia ndani kabisa ya mifuko yao kwa niaba yake.

Tangu Mei, Rais Obama amehudhuria hafla 69 za uchangiaji, kila moja ikiwa na kiingilio cha maelfu ya dola. Mpinzani wake, Mitt Romney, amefanya hafla 105 za udhamini katika mbio za kukusanya pesa, ambazo tayari zimekusanya zaidi ya dola bilioni 1.3.

Wakati kiasi kinaonekana kuwa kikubwa, uchaguzi wa mwaka huu haupaswi kugharimu zaidi ya ule wa mwaka 2008 kwa kuwa rais hakugharamia kampeni ili achaguliwe kuwa mgombea wa chama chake.

Romney ampiku Obama kwa fedha

Kufikia Agosti 31, Obama alikuwa amekwisha changisha dola milioni 432, hii ikiwa chini ya dola milioni 746 alizokusanya miaka minne iliyopita, kwa mujibu wa takwimu za Tume ya Uchaguzi ya Marekani. Kwa kulinganisha, Romney alikusanya dola milioni 274, kiasi ambacho ni chini ya dola milioni 288 alizokusanya John McCain. Lakini namba haziishii hapo.

Mgombea wa Democrats, Rais Barak Obama.
Mgombea wa Democrats, Rais Barak Obama.Picha: Reuters

Juu ya juhudi za kukusanya michango, zipo fedha zinazokusanywa katika hafla za kitaifa za vyama vya Democratic na Republican - milioni 233 kwa Democrats na milioni 283 kwa Republicans.

Pia kuna makundi huru yasiyoengema chama au kamati zenye ushawishi wa kisiasa ambazo zimekusanya dola milioni 36 kwa Obama na dola milioni 97 kwa Romney. Na wakati Obama bado hajafikia viwango vya mafanikio ya mwaka 2008, bado anaendelea kuwa kinara wa michango midogo midogo. Asilimia 37 ya hundi zinazotumwa kwa kampeni yake ni zile zenye kiasi cha chini ya dola 200.

Hazina ya mpinzani wake tajiri inapokea asilimia 16 tu ya hundi za namha hiyo, kwa mujibu wa takwimu zilizokusanywa na mtandao wa opensecrets.org.

Lakini chama cha Republicans kinaziba pengo kati yake na Obama kwa mamilioni ya fedha kutoka matajiri binafsi, ambao wako huru kuchangia bila kikomo, kwa kamati za kampeni baada kubadilishwa kwa sheria zinazodhibiti ufadhili wa kampeni hivi karibuni.

Katika matangazo ya kambi ya Romney yaliyorushwa mwezi Septemba, ni nusu tu yalilipiwa na kambi yake, kwa mujibu wa takwimu za kampuni ya Kantar Media ambazo zilichambuliwa na kituo cha utafiti cha Wesleyan, kinachotathmini matumizi ya matangazo ya kisiasa.

Matangazo mengine yalilipiwa na mashirika yaliyo huru kukusanya fedha kutoka kwa watu binafsi, mashirika na vyama vya wafanyakazi. Hii ni kufuatia uamuzi wa mahakama ya juu ya Marekani iliyotoa ruhusa kwa kuchangia kiasi chochote cha fedha kwa makundi ya kisiasa yasiyo na upande, ili mradi tu makundi yawe huru na wagombea.

Makampuni makubwa yamsaidia Romney

Kuna makundi ya aina mbili ya nje - kamati yenye ushawishi wa kisiasa, maarufu kama Super PACs ambayo yanatakiwa kuweka wazi majina ya wachangiaji wake, na makundi ya mashirika yanayohusika na ustawi wa kijamii kama vile makanisa na makundi ya mazingira. Haya hayalazimishwi kutaja wafadhili wake lakini yanaruhusiwa kutumia nusu ya matumizi yake katika harakati za kisiasa.

Mgombea wa Republicans, Mitt Romney.
Mgombea wa Republicans, Mitt Romney.Picha: Reuters

Wanaoongoza katika kuichangia kamati ya ushawishi ya Republican ni pamoja na bilionea Harold Simmons, Afisa Mtendaji Mkuu wa makampuni ya Contran aliyetoa kiasi cha dola milioni 10. Anafuatiwa na Bob Perry, kiongozi wa kampuni ya ujenzi ya Perry Homes aliechangia dola milioni 6, na orodha inaendelea kwa dazen kadhaa za wafanyabiashara wahafidhina walio na uwezo wa kuongeza rasilimali za kambi yao mara mbili ndani ya siku moja.

Lakini athari kubwa itaonekana katika uchaguzi wa wabunge ambako msukumo mdogo wa milioni kadhaa unaweza kukamilisha mbio, aslisema Michael Malbin, mkurugenzi mtendaji wa taasis ya udhamini wa kampeni. Kundi la American Crossroads ambalo wadhamini wake wanabaki kuwa siri, limeweka nusu ya matumizi yake kwa ajili ya chaguzi za wabunge, likitumaini kubakiza wingi katika Congress na kuzuiwa ajenda ya Obama endapo atachaguliwa tena.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/AFPE
Mhariri: Sekione Kitojo