1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ferguson astaafu kama kocha wa Manchester United

8 Mei 2013

Mkufunzi maarufu sana aliyewahi kupata mafanikio makubwa nchini Uingereza, Sir Alex Ferguson atajiuzulu kama kocha wa klabu ya Manchester United mwishoni mwa msimu huu wa 2012/2013

https://p.dw.com/p/18U0Y
26 May 1999: Manchester United manager Alex Ferguson and keeper Peter Schmeichel with the trophy after a 2-1 victory over Bayern Munich in the UEFA Champions League Final at the Nou Camp in Barcelona, Spain. \ Mandatory Credit: Phil Cole /Allsport
Manchester United Sir Alex Ferguson RücktrittPicha: Getty Images/Phil Cole /Allsport

Ferguson alishinda mataji 13 ya Ligi kuu ya soka England wakati wa uongozi wake wa misimu 26 katika klabu hiyo. Klabu imetoa taarifa leo iliyomnukuu Ferguson akifafanua kuwa msimu huu wa 26 ndio utakaokuwa wake wa mwisho. Kocha huyo mwenye umri wa miaka 71 amesema ametafakari sana kuhusu uamuzi wa kustaafu kwake.

Amesema ameonelea ni muhimu kuondoka katika klabu hiyo wakati ikiwa katika hali nzuri na anaamini ametimiza hilo. Fergie amewapokonya Manchester City taji la Premier Legaue msimu huu na kulirejesha katika uwanja wa Old Trafford ikiwa ni taji la 20 la klabu hiyo. Kocha huyo ambaye sasa atasalia kama mkurugenzi mkuu na mjumbe wa klabu ya Manchester United, amesema ana matumaini kuwa amejiuzulu kama mkufunzi wakati klabu hiyo ikiwa katika hali nzuri kabisa.

Nani atakayemrithi Fergie?

United hawajatoa dalili zozote za ni nani atakayevivaa viatu vya Sir Alex Ferguson wakati kukiwa na uvumi kuwa meneja wa Everton David Moyes huenda akaijaza nafasi hiyo ya katika uwanja wa Old Trafford.

Sir Alex Ferguson aliiongoza Manchester United kutwaa taji la 20 la Premier League mwezi Aprili
Sir Alex Ferguson aliiongoza Manchester United kutwaa taji la 20 la Premier League mwezi ApriliPicha: Reuters

Kocha wa Real Madrid Jose Mourinho, ambaye aliweka uhusiano mzuri wa utani wakati alipokuwa kocha wa mahasimu wa United, Chelsea, pia amepigiwa upatu kupewa nafasi hiyo.

David Gill ambaye aliweka ushirikiano wa kiwango cha juu cha mafanikio na Fregie kama Afisa Mkuu Mtendaji ikiwa ni pamoja na ushindi wa mataji matatu katika msimu mmoja wa mwaka 1999 – Premier League, Champions League na Kombe la FA, amepeana salamu za pongezi na heri njema kwa kocha huyo.

Amesema imekwua heshima kubwa na furaha yeye kufanya kazi na Alex kwa takribani miaka 16, kipindi ambacho mataji mengi yamewekwa kabatini.

Ferguson anatarajiwa kufanyiwa upasuaji wa mfupa wa nyonga mwishoni mwa msimu huu lakini kabla ya uvumi kuanzishwa jana Jumanne, hakukuwa na dalili kuwa angejiuzulu.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP

Mhariri: Yusuf Saumu