1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Castro resigns

Abdulrahman, Mohamed19 Februari 2008
https://p.dw.com/p/D9g6
Rais Fidel Castro wa CubaPicha: DW-TV

Kiongozi mkongwe wa  Cuba Fidel Castro amejiuzulu mapema leo asubuhi kama Rais wa  taifa hilo  baada ya kushika wadhifa huo kwa karibu nusu karne.Castro alielezea uamuzi wake huo katika barua iliochapishwa na Shirika rasmi la habari la nchi hiyo.


Fidel Castro alisema katika barua hiyo iliochapishwa pia katika gazeti la chama cha kikoministi linalotoka kila siku Granma, kwamba hatokubali  muhula mwengine, wakati bunge litakapokutana Jumapili ijayo na akasisitiza " Sitokubali au kushawishi kuuendelea kuwa rais wa baraza la taifa  au kamanda mkuu wa majeshi.


Baraza jipya la taifa  litakutana Jumapili ijayo ikiwa ni  kwa mara  ya kwanza tangu Januari, kulichagua baraza tawala la taifa, akiwemo wadhifa wa rais  ambao umekua ukishikiliwa na  Castro. Tangazo la  Castro mwenye umri wa miaka  81 kwa hivyo , linamaliza utawala wake wa karibu nusu karne, na kumuweka nafasi ya usoni nduguye Raul mwenye umri wa miaka 76 kuchukua nafasi yake


Harakati za  Castro hadi kufikia kukamata hatamu za uongozi zilianzia Desemba 2, 1956, wakati akiwa pamoja na wana mapinduzi wenzake akiwemo Che Guevara, walipoanza uasi dhidi ya utawala wa  Batista  kwa kufika kusini mashariki mwa kisiawa hicho kwa meli baada ya kuwa uhamishoni waliokoandaa uasi huo.


Miezi  ishirini na tano baadae wakamuangusha batista na Castro akatangazwa Waziri mkuu

Castro  anayeitwa  na  wafuasi  kwa jina  la "Fidel au El Comandante" na aliyewahi kusomea sheria akajiweka karibu na  Urusi ya zamani na kambi ya mashariki,  nchi zilizouunga mkono utawala wake wa kikoministi hadi kusambaratika kwa uliokua muungano wa kisovieti 1989.


Muda wote alikua na uhasama na  Marekani. pamoja na hayo amewashuhudia Marais 10 wa Marekani wakiingia madarakani na kutoka, licha ya  shinikizo la  zaidi ya miongo minne  kwa sababu ya sera yake ya mapinduzi.

Katika kuungwa mkono  na Urusi  kwa hali na mali,  dola hilo mkubwa  liliweka hata  makombora ya kinuklea, katika kuisaidia Cuba kukabiliana na kitisho cha Marekani  1962, baada ya kushindwa jaribio la kukivamia kisiwa hicho lililofanywa na  wacuba uhamishoni lina kuungwa mkono na shirika la ujasusi la Marekani-CIA Aprili 1961.Cuba ikavunja uhusiano wa kibalozi na Marekani.


Castro alikua pia  kwa muda mrefu  Kiongozi  mwenye usemi miongoni mwa mataifa ya ulimwengu wa tatu katika  mvutano baina ya  mashariki na magharibi. Alituma wanajeshi 15,000 kuiasaidia serikali ya Angola 1975 ya chama cha MPLA na kutuma pia wanajeshi Ethiopia 1977 wakati wa utawala wa Mengistu Haile Mariam.


Baada ya kuporomoka kwa iliokua Urusi ya zamani uchumi wa Cuba nao ulikaribia kuporomoka na Castro akalazimika kuruhusu  watalii wa kigeni kuizuri nchi hiyo pamoja na kuanzisha marekebisho madogo ya kiuchumi. Licha ya vikwazo vya kiuchumi vya Marekani  Cuba  imeendelea kuhimili hali ngumu, hadi tangazo la kujiuzulu kwa Fidel Castro hii leo.