1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

FIFA yatangaza vita dhidi ya ubaguzi wa rangi

1 Juni 2013

Shirikisho la soka ulimwenguni – FIFA limetangaza hatua kali za kupambana na matukio ya kibaguzi, kuchunguza uhalali wa maafisa wake wa ngazi ya juu na likampa mwanamke muhula wa miaka minne katika bodi yake

https://p.dw.com/p/18i9F
Fussball 63. FIFA Kongress auf Mauritius 2013 30.05.2013 FIFA Praesident Joseph S. Blatter (Schweiz) eroeffnet den Kongress FOTO: Pressefoto ULMER/Markus Ulmer xxNOxMODELxRELEASExx
Sepp Blatter 63. FIFA Kongress MauritiusPicha: picture alliance / Pressefoto ULMER/Markus Ulmer

Hata hivyo baadhi wanasisitiza kuwa FIFA haifanyi ya kutosha. Rais wa shirikisho hilo Sepp Blatter, hata hivyo ametoshelezwa na hatua hizo kufuatia kashfa zilizoshuhudiwa katika miaka kadhaa ya nyuma. Akizungumza katika kikao cha wajumbe wa FIFA mjini Port Louis, Mauritania, Blatter amesema kuwa ana furaha FIFA hatimaye imejinyanyua baaada ya kukabiliwa na changamoto chungu nzima.

Lakini mkuu wa jopo la mageuzi linalolishauri shirikisho la FIFA amesema bado kuna mengi ya kufanywa. Profesa huyo Mswisi Mark Pieth amesema FIFA ni lazima itangaze hadharani mishahara na marupurupu ya maafisa wake wanaopata donge nono na kuweka kiwango cha juu cha umri na muhula wa kuhudumu kwa maafisa wake wakuu. Pia, wachunguzi huru hawajajumuishwa katika kamati kuu ya FIFA inayofanya maamuzi.

Matukio ya ubaguzi wa rangi katika viwanja vya kandanda yameendelea kushuhudiwa
Matukio ya ubaguzi wa rangi katika viwanja vya kandanda yameendelea kushuhudiwaPicha: Getty Images

Hatua kali dhidi ya ubaguzi wa rangi

FIFA imechukua hatua kuhusiana na ubaguzi wa rangi, na sasa timu zitakabiliwa na adhabu kali kwa kupatikana na hatia ya tukio baya la kibaguzi, ikiwa ni pamoja na kupokonywa pointi na kushushwa daraja.

Hatua hizo zimeidhinishwa kwa wingi na zinafuatia matatizo ya karibuni nchini Italia na England. Kulingana na sheria hizo mpya, makosa makubwa au ya kurudiwa yatakayofanywa na klabu au mashabiki wake yatasababisha pia kupigwa marufuku timu kushiriki katika vinyang'anyiro fulani ikiwa ni pamoja na ligi ya mabingwa Ulaya – Champions League.

Mwanamke wa kwanza achaguliwa

Katika suala jingine, Lydia Nsekera wa Burundi amepigiwa kura ya kujiunga na kamati kuu ya FIFA kama mwanamke wa kwanza kuwahi kuwa mwanachama wa kudumu kwa muhula wa miaka minne, wakati wanawake wengine wawili wakiwekwa katika kamati hiyo kwa mwaka mmoja. Nsekera alihudumu katika bodi hiyo kwa kipindi cha muda mwaka uliopita.

Kamati kuu imepanuliwa hadi wanachama 27. Rais wa shirikisho la soka Marekani Sunil Gulati ameanza muhula wake katika kamati hiyo hapo jana. Gulati amechukua nafasi ya Chuck Blazer ambaye alihudumu kwenye kamati hiyo tangu mwaka wa 1997 na akasimamishwa uwanachama mapema mwezi Mei baada ya kutuhumiwa kwa madai ya ubadhirifu wa takribani dola milioni 21.

Mwandishi: Bruce Amani/

Mhariri: Sekione Kitojo