1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

FIFA:Vilabu vya Ulaya havitalipwa fidia

Admin.WagnerD25 Februari 2015

Shirikisho la soka duniani FIFA limetunisha misuli yake tena leo (25.02.2015) kwa kutangaza vilabu vya soka havitalipwa fidia kwa kuwapoteza wachezaji na kuvurugika kwa ligi kutokana na kuahirisha kombe la dunia 2022.

https://p.dw.com/p/1EhBl
Jerome Valcke
Katibu Mkuu wa FIFA, Jerome ValckePicha: picture-alliance/Alessandro Della Bella

Siku moja baada ya kamati maalumu ya FIFA kuvikasirisha vilabu vya Ulaya kwa kupendekeza michuano ya kuwania kombe la dunia la kandanda mwaka 2022 nchini Qatar ichezwe wakati wa msimu wa baridi, badala ya msimu wa joto mwezi Juni na Julai kama ilivyo kawaida, katibu mkuu wa FIFA Jerome Valcke aliwaambia waandishi wa habari mjini Doha kwamba hakutakuwa na fidia yoyote ya fedha itakayolipwa kwa sababu ya kuvurugika kwa ligi za kitaifa.

Valcle alisema, "Ukiniuliza mimi kuhusu fudia; Hakutakuwa na fidia yoyote. Kuna miaka saba ya kupanga upya masuala ya soka ulimwenguni kote kwa ajili ya michuano hii ya kombe la dunia."

Mashirikisho kadhaa ya kandanda ya Ulaya yamepinga uamuzi huo huku mwenyekiti wa timu ya Bayern Munich ya Ujerumani, Karl-Heinz Rummenigge, ambaye pia ni mwenyekiti wa shirikisho la vilabu vya Ulaya, akisema vilabu na ligi za kitaifa hazipaswi kuachiwa mzigo wa hasara itakayotokana na kuahirishwa kwa kombe la dunia.

Rummenigge FC Bayern Archiv 17.09.2013
Mwenyekiti wa Bayern Munich, Karl-Heinz RummeniggePicha: picture-alliance/dpa

Kuahirishwa kwa kombe dunia kutoka Juni na Julai hadi msimu wa baridi barani Ulaya mwezi Novemba na Desemba kutazivuruga ligi za mataifa ya Ulaya na mashindano ya bara zima, ikiwemo ligi ya mabingwa wa Ulaya na ligi ya Ulaya. Tarehe kamili za michuano hiyo iliyopendekezwa kuchezwa kwa siku 28 badala ya siku ya 32, zitaamuliwa na kamati tendaji ya FIFA katika mkutano utakaofanyika mjini Zurich Machi 19 na 20 iwapo mapendekezo yataridhiwa.

Kombe la Mataifa ya Afrika kuahirishwa

Wakati huo huo, FIFA ilisema mashindano ya kuwania kombe la kandanda la mataifa ya Afrika mwaka 2023 nchini Guinea yameahirishwa kutoka mwezi Januari hadi Juni kutokana na mpango wa kuahirisha michuano ya kombe la dunia nchini Qatar.

Katibu mkuu wa FIFA, Jerome Valcke, alisema, "Mashirikisho ya soka ya Afrika yamekubali kwa kauli moja hayatandaa mashindano ya kombe la mataifa ya Afrika mwezi Januari mwaka 2023. Badala yake watayaahirisha hadi mwezi Juni ili kuepusha kuwaachia wachezaji wa Kiafrika kwenda kushiriki michuano ya kombe la dunia na wiki mbili baadaye kwenda katika michuano ya kombe la mataifa ya Afrika."

Fußballnationalmannschaft Guinea
Timu ya taifa ya Guinea ilipopimana nguvu na Iran, Tehran 2014Picha: BEHROUZ MEHRI/AFP/Getty Images

Msemaji wa shirikisho la soka la Afrika CAF, Junior Binyam alisema katika barua pepe kwa shirika la habari la Associated Press kwamba hajajulishwa rasmi kuhusu uamuzi huo wa FIFA kuahirisha fainali za kombe la mataifa ya Afrika, lakini CAF itaunga mkono mapendekezo yoyote ya kamati maalumu ya FIFA.

Kwa upande mwingine FIFA ilisema bado kuna matatizo kuhusiana na hali ya wafanyakazi wa kigeni wanaojenga viwanja vya soka kwa ajili ya kombe la dunia mwaka 2022 nchini Qatar. Katibu mkuu wa FIFA Jerome Valcke alisema wanaendelea na mazungumzo na shirika la kazi la kimatiafa, ILO, kuhusu suala la haki za wafanyakazi.

Mwandishi: Josephat Charo/AFPE/APE/DPAE

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman