1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Finali ya champion League:nani ataibuka bingwa ?

21 Mei 2010

Bayern munich au Inter Milan ?

https://p.dw.com/p/NU2V
Makocha 2: Jose Mourinho na Louis van Gaal Montage:nani atampiku mwenzake leo ?Picha: AP/Montage DW

Pale firimbi ikilia leo usiku katika uwanja wa dimba wa Bernabeu Stadium mjini Madrid,Spain, kuziita uwanjani kwa finali ya Champions League- Bayern Munich,mabingwa wa Ujerumani na Inter Milan, mabingwa wa Itali,kila moja itakuwa inaania taji lake la 3 msimu huu ili kuandika historia.

Isitoshe, leo si finali tu kati ya timu hizo 2 bali pia ni finali za mbinu za dimba kati ya kocha wa Bayern Munich,mdachi Louis Van Gaal na mreno Louis Mourniho wa Inter Milan. Endapo mtego wa Mourniho ukimnasa van Gaal,kuna uvumi kwamba, Mourinho, atabakia Madrid kuwa kocha wa Real Madrid na akina Kaka na Cristiano Ronaldo. Mashabiki nchini Kenya wanamshangiria stadi wao anaeichezea Inter Milan : Macdonald Mariga:

Sababu nyengine, ni kwavile mashabiki wengi wa Kenya na Afrika mashariki kwa jumla, ni wapenzi wa Manchester United iliopigwa kumbo nje ya finali ya ya leo (jumamosi) na mabingwa wa Ujerumani,Bayern Munich,na hivyo, wakenya wanailalia dago Inter kuwalipizia kisasi chao kwa Manu kutolewa nje mikono mitupu msimu huu.

Firimbi ikilia leo usiku basi, ukweli utadhihiri na uongo utajitenga.Mastadi 2 wa Holland ambao wakiichezea Real Madrid hapo zamani, wanarudi nyumbani uwanjani Bernebeu Stadium:Upande wa Inter Milan, ni Wesley Sneider na wa Bayern Munich, ni Arjen Robben.

Alipowasili Madrid hapo alhamamisi, Robben, ambae ndie aliekuwa ufunguo wa ushindi wa B. Munich hadi kuwasili finali hii, alidai eti wao wanaiangalia finali hii ya champ- league kuwa sawa na mpambano mwengine wowote ule. Aliongeza kusema kwamba, ari ya mchezo ya Bayern Munich, ni kubwa kabisa na kwamba, wamefurahia kuwapo Madrid.

Hamasa na jazba nyingi kabla ya finali hii, zilituwama juu ya uvumi kuwa kocha wa Inter Milan ,Jose Mourinho, ataaga Serie A,Ligi ya Itali - baada ya firimbi ya mwisho kulia kesho na kuwa kocha wa Real Madrid. Isitoshe, Mourinho , alipalilia kuni katika moto wa uvumi huo alipowataka mara tu baada ya kuwasili Madrid, mashabiki wa Real, kuishangiria kesho timu yake ya Inter.Inter Milan, iliizaba Siena bao 1:0 Jumamosi iliopita na kutawazwa mabingwa wa Itali .Kabla ya hapo, walitwaa Kombe la Taifa.

Bayern Munich nayo kwa upande wake, iliikomea Jumamosi iliopita katika Uwanja wa olimpik wa Berlin, Weder Bremen, mabao 4:0 na kuvaa taji la pili.Baada ya ushindi huo,kocha wa Bayern Munich, mdachi van Gaal akanadi:

"Sisi ndio timu bora kabisa nchini Ujerumani na pengine hata ulaya nzima."

Kwa hivyo, ikiwa kila kitu kitaenda sawa kwa van Gaal ,ataivika Bayern Munich ,taji la tatu usiku wa leo na halkadhalika, Jose Mourinho,kwa upande wa Inter Milan na kwa wapenzi wa MaCdonald Mariga, nchini Kenya.

Mwandishi:Ramadhan Ali/DPAE

Uhariri:Aboubakary Liongo