1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Finali ya kombe la dunia la klabu bingwa Tokyo

19 Desemba 2008

Manchester United ina miadi na Quito jumapili kwa finali .

https://p.dw.com/p/GJe3
Manchester United wakishangiria ubingwa wa Ulaya hapo.Picha: picture-alliance/ dpa

Finali ya Kombe la klabu bingwa za dunia ni kesho jumapili kati ya mabingwa wa ulaya Manchester United na la Liga de Quito ya Ecuadaor. Manchester ilikata tiketi yake ya finali ya kesho kwa kuizaba Gamba Osaka ya Japan kwa mabao 5-3 wakati Quito ilinguruma mbele ya Pacucha ya Mexico kwa mabao 2-0.

Wakati Bundesliga -ligi ya Ujerumani imekwenda likizoni kwa siku kuu za X-masi na mwaka mpya huku Hoffenheim ikiwa imewapiku mabingwa Bayern Munich kwa kuparamia wao kileleni, Premier League inaendelea.

Katika medani ya riadha na ringi ya mabondia,malkia wa kenya Pamela Jelimo, alietwaa msimu huu kitita cha dala milioni moja katika mbio za mita Golden League,mbio zake za mita 800 zimefutwa mwakani.Na mbabe wa zamani wa wezani wa juu ulimwenguni mzee Evander Holyfield anarudi ringini usiku wa leo kupambana na mrusi Nikolai Valuev mjini Zurich.

Kesho ni finali ya Kombe la dunia la klabu bingwa mjini Tokyo, Japan kati ya mabingwa wa ulaya Manchester United na Liga de Quito ya Ecuador.

Wakati Quito imeilaza Pacucha ya Mexico mabao 2-0 kukata tiketi yao ya finali ya kesho, manchester ilitamba mbele ya wenyeji majapani Gamba Osaka kwa mabao 5-3.Tayari katika kipindi cha mapumziko,Manu ikiongoza kwa mabao 2 -moja la Nemanja Vidic na jengine la Cristiano Ronaldo.

Wakati Manchester inapania kuwa mabingwa wa kwanza wa Uingereza kuvaa taji kesho la kombe la dunia la klabu bingwa, Ligi ya nyumbani inaedelea mwishoni mwa wiki hii huku Liverpool ikiwa kileleni.Kesho (jumapili)asie na mwana aeleke jiwe,kwani Liverpool ina miadi na Arsenal wakati New Castle United ikipambana na Tottenham Hotspur.West Bromwich Albion inaikaribisha nyumbani Manchester City.

Leo lakini, Blackburn Rovers wanaonana na Stoke City wakati Bolton Wanderers wanapapurana leo na portsmouth,Fulham na Middlesbrough.Chelsea iliopo nyuma ya Liverpool ina miadi keshokutwa jumatatu na Everton.

Mabingwa wa Itali, Inter Milan hawna shaka tena ya kuupitisha mwaka huu wa 2008 wakiwa kileleni mwa Serie A-ligi ya itali na kuwaacha mbali mahasimu wao Juventus.Kwani, Milan tayari imefungua mwanya wa pointi 6 kileleni kati yake na Juventus turin.Ukisalia mpambano 1 kabla likizo ya wiki 3 ,timu hii ya kocha mreno Jose Mourinho tayari ina pointi 39 kutoka mechi 16.

Ama katika la Liga-ligi ya Spain, mabingwa real Madrid wana miadi leo na Valencia iliopigwa kumbo nje ya kombe la ulaya la UEFA hivi majuzi.Espanyol inakutana na Atletico Madrid.Viongozi wa ligi FC Barcelona wana miadi kesho na Villareal wakati Real betis wanakutana na Athletic Bilbao.

Mwaka wa 2008 utakumbukwa kwa kumtawaza malia wa mbio wa Kenya wa mbio za mita 800 Pamela Jelimo bingwa wa Olimpik huko Beijing na kwa kutunzwa baadae kitita cha dala milioni 1 kutoka ushindi wake katika mashindano ya Golden League.Shirikisho la riadha ulimwenguni IAAF,lakini limefuta mbio zake za mita 800 katika orodha ya mashindano na hivyo,kumnyima Pamela nafasi nyengine ya ushindi.

Katika ringi ya mabondia, mbabe wa zamani wa wezani wa juu ulimwenguni,mzee Evander Holyfield aliewahi kutafunwa sikio na Mike Tyson, anarudi leo usiku ringini mjini Geneva kupambana na mrusi Nikolai Valuev.Holyfield ana umri wa miaka 46 na wengine wanajiuliza ataka nini tena ?Jaribio la holyfield la kuania taji la WBA limewagawa mashabiki wa ringi ya mabondia.