1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Freiburg yailaza Eintracht Frankfurt

Bruce Amani
6 Machi 2017

Matumaini ya Eintracht Frankfurt kucheza kandanda la Ulaya msimu ujao yamepata pigo jana baada ya kichapo cha 2-1 nyumbani dhidi ya Freiburg.

https://p.dw.com/p/2YitV
Deutschland Eintracht Frankfurt - SC Freiburg
Picha: picture alliance/dpa/T. Wagner

Ushindi huo umeisogeza Freiburg katika nafasi ya nane na kuiacha Frankfurt hoi katika nafasi ya sita huku kukiwa na mechi 11 zilizosalia msimu kukamilika. Huyu hapa mfungaji wa mabao yote mawili ya Freiburg Florian Niederlechner "Kocha na kikosi chake cha kiufundi walitupanga vizuri. watu wanabidi watambue hilo na kusifu pia. ulikuwa mchango bora kabisa, tumefanikiwa kusawazisha maramoja. baadaye tukapata motisha na kila mmoja kumpigania mwenzake. kwa maana hiyo tulipata nguvu na kuweza kuugeuza mchezo. heko kwetu" Alisema Florian  

Deutschland Eintracht Frankfurt v SC Freiburg - Bundesliga
Florian Niederlechner alitikisa wavu mara mbiliPicha: Getty Images/Bongarts/A. Grimm

Katika mpambano mwingine, Hamburg ilipata ushindi katika dakika za mwisho mwisho wa bao moja kwa sifuri dhidi ya Hertha Berlin, na kuimarisha nafasi zao za kuepuka shoka la kushushwa ngazi. Ulikuwa ni ushindi wake wa sita msimu huu.

Vinara Bayern Munich walijiimarisha kileleni kwa tofauti ya pointi saba baada ya kupata ushindi wa 3-0 ugenini dhidi ya Cologne siku ya Jumamosi. Matokeo hayo yamewapa fursa Bayern kupumua kidogo mbele ya nambari mbili RB Leipzig, ambao walikabwa kwa sare ya 2-2 na Augsburg Ijumaa usiku. Philip Lahm ni nahodha wa Bayern "Wakati tukiuleta mchezo wetu, inakuwa vigumu sana kwa mpinzani yeyote. Na kisha itakuwa vigumu kwetu kutokuwa mabingwa wa Ujerumani, lakini tunapaswa kuendelea kucheza vyema. kuna mechi za katikati ya wiki, hivyo lazima mchezo wetu uwe juu kila baada ya siku tatu, wakati kukiwa na mechi muhimu, lakini kwa sasa mambo yanaonekana kuwa mazuri tu".

Deutschland 1. FC Köln - Bayern München
Bayern sasa wanaongoza kwa tofauti ya pointi sabaPicha: picture alliance/dpa/F. Gambarini

Nambari tatu kwenye msimamo wa ligi Borussia Dortmund iliinyeshea mvua ya mabao Bayer Leverkusen, huku mshambuliaji Pierre-Emerick Aubameyang akifunga mawili katika ushindi wao wa 5-2. Aubameyang sasa ana mabao 21 mawili mbele ya Robert Lewandowski wa Bayern lakini ushindi wa BVB uligubikwa na tukio la kuumia kiungo mshambuliaji Marco Reus. "kimsingi wakati unajihisi hivyo, Leverkusen ilikaribia kufunga bao la kuwasizisha tena, na tuna mabao mawili, ambayo yalikuwa muhimu sana kwetu leo, katika siku ambazo mambo hayakwendei vyema, basi bila shaka lazima utumie vyema nafasi zako".

Kocha wa Leverkusen Rodger Schmidt alisema walicheza vyema licha ya kichapo hicho kikubwa "Baada ya mapumziko tulifanya mambo kuwa 2-1 na kisha tukafunga tena na kuwa 3-2, na ukawa mchezo wa kusisimua. Dortmund bila shaka ikaongeza kasi lakini kwa jumla nahisi ulikuwa mchezo mzuri kutoka kwetu, hata ingawa matokeo ya 6-2 ni kichapo kikubwa.

Deutschland Borussia Dortmund v Bayer 04 Leverkusen | Roger Schmidt
Roger Schmidt alikabiliwa na shinikizo kabla ya kutimuliwaPicha: Getty Images/Bongarts/M. Rose

Na hayo ndiyo yalikuwa maneno yake ya mwisho maana kufuatia kichapo hicho, Leverkusen hawakuchelewa kumtimua Schmidt ambaye kwa muda mrefu amekuwa chini ya shinikizo.

Hoffenheim wanaoshikilia nafasi ya nne kwa sasa nao pia waliwabumburusha Ingolstadt mabao 6-2, mchuano uliowapa matumaini vijana hao wa kocha chipukizi Julian Nagelsmann. Msikilize nahodha wa Hoffenheim, Sebastian Rudy "pia nadhani kuwa mwishowe matokeo yalikuwa makubwa mno, lakini ulikuwa mpambano uliokuwa sawa kwa timu zote mbili hadi dakika ya 60 ambapo Ingolstadt walikuwa kifua mbele. lakini tukajituma na kuanza kupambana na mwishowe ushindi huo ulistahili. lakini ulikuwa juu mno.

Katika matokeo mengine, Darmstadt ilipoteza dhidi ya Werder Bremen kwa mabao 2-0. Wolfsburg ilitoka sare ya 1-1 na Mainz wakati Borussia Moenchengladbach ilipanda nafasi mbili juu hadi ya nane baada ya ushindi wa kuridhisha wa 4-2 nyumbani dhidi ya Schalke. Kichapo hicho kiliiangusha Schalke katika nafasi ya 13

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/Reuters
Mhariri:Yusuf Saumu