1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Frontex: Wahamiaji wavumbua njia mpya ya kuingia Ulaya

Zainab Aziz
8 Julai 2018

Mkurugenzi wa shirika la kulinda mipaka ya Ulaya Frontex, Fabrice Leggeri ameonya kuhusu njia mpya itakayotumiwa na wahamiaji wanaoingia nchini Uhispania.

https://p.dw.com/p/310Hz
Libyen Migranten und Flüchtlinge auf einem Schlauchboot
Picha: Getty Images/AFP/A. Solaro

Taarifa hii imetokea huku Tume ya Ulaya ikiwa inajiandaa kuwasilisha mapendekezo mapya kuhusu kuiimarisha mipaka ya nje ya umoja huo. Mkurugenzi huyo wa shirika la Frontex  Fabrice Leggeri amesema kuna njia mpya ambayo huenda ikatumiwa na wahamiaji kuingia katika bara la Ulaya. Leggeri ameliambia gazeti la Ujerumani la ``Die Welt am Sonntag`` kuwa wasiwasi wake mkubwa kwa sasa ni Uhispania.

Rais wa Tume ya Ulaya Jean-Claude Juncker amesema mapendekezo hayo mapya yatawasilishwa mwezi Septemba. Juncker ameongezea kuwa mapendekezo hayo yatahusisha juu ya kuwekwa walinzi 10,000 katika mipaka ifikapo mwaka 2020 wakati ambapo Umoja wa Ulaya unajiandaa kukabiliana na wimbi la wahamiaji ambalo limesababisha mvutano wa kisiasa kati ya nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya.

Inakadiriwa kwamba takriban wahamiaji 6,000 walivuka mpaka kinyume cha sheria kupitia kwenye bahari ya Mediterenia mwezi Juni na kuingia Uhispania. Mpango wa Umoja wa Ulaya unaokusudia kufunga njia zinazotumiwa na wahamiaji kupitia Ulaya unaweza kusababisha shinikizo jipya katika njia ya kutoka Afrika hadi Uhispania.

Mkurugenzi wa shirika la kulinda mipaka ya Ulaya Fabrice Leggeri
Mkurugenzi wa shirika la kulinda mipaka ya Ulaya Fabrice Leggeri Picha: picture-alliance/AP Photo/G. Vanden Wijngaert

Kulingana na Kansela wa Austria Sebastian Kurz, mawaziri wa Mambo ya ndani kutoka Ujerumani, Austria na Italia wanapanga kukutana wiki ijayo katika mji wa Innsbruck ulio magharibi mwa Austria kujadili hatua zitakazofanikisha kuifunga njia ya bahari ya Mediterania inayotumika kuwaingiza wahamiaji barani Ulaya na ambayo ni hatari.

Katika mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya uliofanyika tarehe 28 mwezi uliopita, nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya zilikubaliana kuiongezea makali sera yake ya uhamiaji na kuifanya kuwa ngumu zaidi. Katika siku zijazo meli zitakazowaokoa wahamiaji zitatia nanga katika kituo kikuu cha kuwapokea wahamiaji kitakachokuwa Ulaya.

Serikali ya Italia pia imependekeza kujengwa vituo vya kuwapokea wahamiaji katika nchi za Afrika zile zinazotumiwa kama mahala pa kusafiria kuja Ulaya. Mkuu wa shirika la kulinda mipaka ya Ulaya Fabrice Leggeri amesema anaunga mkono mpango wa kujengwa kwa vituo hivyo, akiongeza kwamba wahamiaji hawatokuwa na dhana kwamba watapelekwa Ulaya baada ya kuokolewa.

Kushoto: Rais wa Tume ya Ulaya Jean-Claude Juncker. Kulia: Kansela wa Austria Sebastian Kurz
Kushoto: Rais wa Tume ya Ulaya Jean-Claude Juncker. Kulia: Kansela wa Austria Sebastian KurzPicha: picture-alliance/APA/picturedesk/G. Hochmuth

Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya nje wa Italia Enzo Moavero ameitembelea Libya. Wizara ya mambo ya nje imeeleza hayo katika mtandao wake wa Twitter na kwamba ziara ya waziri Moavero ni ya kushtukiza.

Moavero alikutana na wawakilishi wa serikali ya Libya kujadili msaada wa Italia kwa taasisi za halali za Libya pamoja na kusisitiza na kuyatia nguvu mazungumzo ya kisiasa na upatanisho wa kitaifa chini ya Umoja wa Mataifa. Vilevile kutafuta ushirikiano katika masuala ya uhamiaji, uchumi na usalama.

Ziara hii ni ya pili nchini Libya kufanywa na viongozi wa serikali mpya ya Italia. Naibu waziri Mkuu ambaye pia ni waziri wa mambo ya ndani  wa Italia Matteo Salvini alizuru nchini humo mnamo tarehe 25 mwezi uliopita wa Juni.

Mwandishi:Zainab Aziz/DPAE/AFPE/p.dw.com/p/30yt0

Mhariri: Jacob Safari