1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

G7 kuachana na makaa ya mawe ifikapo 2035

Tatu Karema
30 Aprili 2024

Mawaziri wa nishati na mazingira wa kundi la nchi tajiri kiviwanda (G7) wamekubaliana kuhusu muda wa mwisho wa matumizi ya makaa ya mawe ifikapo mwaka 2035 baada ya mkutano wao nchini Italia.

https://p.dw.com/p/4fLGa
Waziri wa Mazingira wa Italia, Gilberto Pichetto Fratin.
Waziri wa Mazingira wa Italia, Gilberto Pichetto Fratin.Picha: Giulio Lapone/Photoshot/picture alliance

Haya yamesemwa jana na maafisa wa Uingereza na Italia katika uamuzi uliothibitishwa jioni ya Jumatatu (Aprili 29) na wizara ya masuala ya kiuchumi ya Ujerumani.

Msemaji wa wizara hiyo amesema kuwa nchi hiyo ilitekeleza jukumu muhimu katika uamuzi wa kuweka wazi tarehe ya mwisho ya uzalishaji wa umeme kwa kutumia makaa ya mawe kwa nchi zote za G7.

Soma zaidi: Nchi tajiri zatumia mabilioni kuendeleza sekta ya nishati asilia

Awali, Waziri wa Nishati wa Uingereza Andrew Bowie alikuwa ametangaza makubaliano hayo, akiliambia shirika la habari la CNBC pembezoni mwa mkutano huo wa mawaziri wa G7 kwamba wamekubaliana kuacha matumizi ya makaa ya mawe katika nusu ya kwanza ya miaka ya 2030.

"Haya ni makubaliano ya kihistoria ambayo hayakuweza kufikiwa wakati wa mkutano wa mwaka jana wa COP 28 mjini Dubai," alisema.

Mawaziri hao wa G7 walitarajiwa kutoa tamko la mwisho siku ya Jumanne (Aprili 30).