1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

G8 zazisitiza haja ya kuimarisha uhusiano wa maendeleo.

Mohammed Abdul-Rahman29 Machi 2007

Mawaziri wakubaliana kuongeza msaada kwa bara la Afrika

https://p.dw.com/p/CHHD

Mawaziri wa maendeleo na ushirikiano wa kimataifa wa nchi 8 zilizoendelea kiviwanda-kundi linalojulikana kama G8,wamekubaliana tena kwamba nchi zao hazina budi kuuimarisha ushirikiano wa maendeleo na kutekeleza ahadi zao za kuongeza msaada rasmi wa maendeleo. Haya yametokana na mkutano wa mwanzoni mwa juma hili mjini Berlin ambao matokeo yake ni pamoja na wito wa kuongezwa maradufu msaada kwa bara la Afrika katika kipindi cha miaka 3 ijayo.

Katika mkutano wao huo wa Berlin, mawaziri hao wa maendeleo na ushirikiano wa kimataifa kutoka Uingereza, Canada, Ufaransa, Ujerumani, Italia, Japan , Urusi na Marekani, walitoa tangazo la pamoja wakisema serikali zao hazina budi kujitolea kuongeza maradufu msaada wao kwa bara la Afrika hadi ifikapo 2010.

Mawaziri hao walikubaliana katika mkutano wao uliotangulia ule wa kila mwaka wa viongozi wao wa taifa na serikali utakaofanyika katika mji wa Ujerumani wa Heiligendamm Juni 6 hadi 8, kwamba wataendelea kuzingatia misingi ya lile tangazo la Paris lilopitishwa Machi 2 mwaka 2005 ambalo ni makuablaino ya kimataifa kati ya serikali na mashirika ya misaada ya kimataifa juu ya kuongezwa juhudi za kustawisha usimamizi wa misaada.Makubaliano hayo yameweka utaratibu na muongozo wa hatua zinazopaswa kuchukuliwa kuimarisha sio tu misaada yenyewe bali pia kuzingatia taathira zake katika maendeleo.

Mbali na kutoa wito wa kukamilishwa kile kinachoitwa” ukamilisho unaotilia mkazo maendeleo” katika mazungumzo ya biashara ya Doha, mawaziri hao wa kundi la G8 mataifa yalioendelea kiviwanda, wamezitaka serikali za nchi za Afrika, Amerika kusini na kusini mashariki ya Asia, nazo zitowe mchango wao kuunga mkono umuhimu wa kuwepo kwa utaratibu wa dharura utakayoyafanya maendeleo kuwa jambo linalowezekana, kama mchango wa kufikiwa malengo ya milenia. Malengo yaliokubaliwa mwaka 2000 ni manane ikiwa ni pamoja na kupunguza umasiikini na kuboresha huduma za afya na elimu kukiwa shabaha ya masuala kadhaa –yote yakipangwa kufikiwa hadi ifuikapo 2015.

Kile kinachoitwa duru ya majadiliano ya maendeleo ya Doha, yanayofanyika chini ya nguzo ya shirika la biashara duniani, yanalenga katika kupunguza vizingiti vya biashara duniani na kurahisisha ubadilishanaji wa bidhaa na huduma duniani. Mabishano makubwa kuhusu mtindo wa nchi za umoja wa ulaya na Marekani wa kufidia wakulima wao na dai la makampuni makubwa kutaka nafasi zaidi katika masoko ya nchi masikini, ni masuala yaliokwamisha mazungumzo hayo.

Mizozo hii imelikumbanisha kundi hilo la nchi nane zilizoendelea kiviwanda na zile zinazoendelea kama Brazil China, India na Afrika kusini. Bado makubaliano hayaelekea kuwa karibu.Mashirika yasiokua ya kiserikali yameelezea shaka shaka kama kweli ahadi iliotolewa Belin itatekelezwa. Sayid Reinhard Hermle, mkuu wa zamani wa chama cha mashirika ya maendeleo ya kijerumani yasio ya kiserikali alisema nchi zilizoendelea kiviwanda zilitoa ahadi kama hizo miaka ya nyuma, lakini zilibakia karatasini.

Katika mkutano wao huko Gleneagles Scotland 2005, ziliahidi msaada wa maendeleo wa dola bilioni 50, lakini bado ziko mbali mno na utekelezaji wa ahadi yao. Baada ya mkutano wao wa Berlin, ukisubiriwa mkutano wa Viongozi wa nchi hizo za G8 mwezi Juni, kinachofutiliwa kwa makini ni kuona kama sasa kweli utakua umefika wakati wa mataifa hayo yalioendelea kiviwanda kuheshimu ahadi walizotoa.