1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Gaddafi anadi "Jihad" dhidi ya Uswisi.

26 Februari 2010

Chanzo:Marufuku kwa minara misikitini.

https://p.dw.com/p/MBmu
Kiongozi wa Libya -Moammar Gaddafi anadai jihadPicha: AP

Kiongozi wa Libya, Muamar Gadhafi,amepalilia moto zaidi katika ugomvi kati ya Libya na Uswisi. Muammar Gadhafi jana alinadi vita vya "Jihad" huko Benghazi, Libya, dhidi ya Uswisi kwa hatua ya nchi hiyo kupiga marufuku ujenzi wa minara ya misikiti nchini mwake. Muammar Gadhafi alisema kuwa Muislamu yoyote duniani anaeshirikiana na Uswisi kwa aina yoyote ni " kafiri" na anakwenda kinyume na Uislamu.

Akinadi vita vya "Jihad" katika hotuba yake alioitoa jana mjini Benghazi, katika maadhimisho ya "Maulidi" -siku ya kuzaliwa Mtume Muhammad leo, Kiongozi wa libya alisema, na hapa ninamnukulu,

"Vita vya jihad dhidi ya UswisiUzayoni na dhidi ya uchokozi wa kigeni si ugaidi."

Akaongeza Muammar Gadhafi na ninamnukulu, "Kila Muislamu duniani mwenye mafungamano yoyote na Uswisi, ni kafiri na anakwenda kinyume na Uislamu, kinyume na Mtume Muhammad ,kinyume na Mwenye Enzi Mungu na Koran." Muamar Gadhafi aliuambia umati wa watu katika hotuba yake iliooneshwa moja kwa moja na Televisheni . Isitoshe, akatangaza "Isusieni Uswisi, Susieni bidhaa za Uswisi, Susieni kupanda ndege za Uswisi, meli zake na balozi zake........ mchokozi wa nyumba za Mungu, Allah."

Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni ya Uswisi ambae shirika la habari la Ufaransa, AFP, liliswasiliana nae, alisema hana la kusema juu ya tuhuma hizo.Katika kura ya maoni iliopigwa Uswisi, Novemba mwaka jana, wapiga kura nchini Uswisi waliidhinisha kwa kima cha 57.5% kupigwa marufuku ujenzi wa minara katika misikiti nchini mwao.

Rais Gadhafi, alihutubia jana katika wakati nyeti wa usuhuba baina ya nchi hizi mbili- usuhuba ambao, uliharibika hapo Julai, 2008 pale mtoto wa kiume wa Gadhafi na mkewe, walipokamatwa na kuwekwa kizuizini kwa muda mjini Geneva.Hii ilitokana na watumishi 2 wa nyumbani kulalamika kuwa mtoto huyo wa kiume wa Gadhafi amewanyanyasa.

Mzozo huo ukazidi pale Libya ,ilipojibisha haraka kwa kuwakamata na kuwapokonya pasi zao wafanya biashara 2 wa Kiswisi nchini Libya, Rashid Hamdani na Max Goeldi. Mzozo huu ukachafuka zaidi mwaka jana pale biashara fulani kati ya nchi hizi mbili ilipovunjika. Wafanya biashara hao wawili wa Uswisi, wakahukumiwa kuwa walikaa nchini Libya kupindukia muda wa viza zao na eti ,kwakijishughulisha na biashara zisizo halali nchini.

Hukumu ya Hamdani , ikafutwa hapo Januari, mwaka huu, na amerejea nyumbani Uswisi wakati Goeldi, alijisalimisha kwa serikali wiki hii na anatumika kifungo cha miezi 4.Majadiliano yanaendelea kati ya Libya na Uswisi, huku Uswisi ikidai kuachwa huru kwa Goeldi.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Uswisi, Micheline Calmy-Rey, amewaambia maripota kwamba, mazungumzo yamebaki kuwa magumu.Kupiga marufuku ujenzi wa minara misikitini nchini Uswisi, kulipingwa na serikali ya Uswisi, sehemu kubwa ya vyama vya kisiasa na wanaviwanda ;na yalikuwa matokeo ya kura ya maoni yasiotazamiwa.

Serikali ya Uswisi yenye wakaazi wengi mno wa kikristo, ikajaribu kuwatuliza nyoyo Waislamu laki 4 humo nchini, wengi wa asili ya Kituruk na kutoka eneo la Balkan kwamba, matokeo ya kura ile ya maoni haina maana kuikataa jamii ya Waislamu, dini yao au mila na utamaduni wao.Uswisi,ina misikiti jumla ya 200,lakini, ni minne tu yenye minara.

Mwandishi:Ramadhan Ali /AFPE

Uhariri: Miraji Othman